Muro, TFF ngoma bado mbichi, Kesho kwenda TFF tena

Ofisa habari wa Yanga, Jerry Muro
  NGOMA ya Ofisa habari wa Yanga, Jerry Muro na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), bado mbichi na kesho anatarajiwa kupelekwa kwa mara ya pili kwenye kamati ya maadili.
Awali, Jumamosi iliyopita Muro aliwasilishwa kwenye kamati ya Maadili ya Shirikisho hilo ambalo TFF ndio mlalamikaji hata hivyo malalamiko hayo yalitupwa kapuni baada ya barua ya mwito ya Muro iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa kuwa na upungufu.

Kamati iliiagiza TFF kumuandikia upya barua ya mwito Muro ambaye jana iliwasilishwa na mmoja wa maofisa wa TFF kwenye klabu ya Yanga ambapo alikutana na kisiki baada ya watumishi wa klabu hiyo wakiongozwa na katibu muhtasi kugoma kupokea barua hiyo kwa madai ni maagizo ya Muro.

“Katibu muhtasi wa Yanga alimpigia Jerry kumjulisha barua yake na kumuliza kama aipokee au la, Jerry alichofanya ni kumuagiza ampe simu aongee na ofisa wa TFF na ofisa huyo alipopokea simu Muro aliishia kumtukana na kumwambia hakuna kuacha barua hapo,” alisema mtoa habari wetu.

Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas alipoulizwa kuhusu suala hilo alikiri jambo hilo kutokea na kudai kuwa tayari TFF imemjulisha Muro mwito wa kuitwa kwenye kamati ya maadili kesho kupitia barua pepe yake pamoja na kuijulisha klabu yake ya Yanga juu ya mwito huo kupitia kwa katibu wake mkuu Baraka Deusdetit.

Alisema pia kupitia barua pepe hiyo Muro ametahadharishwa kutokukosa kwani kwa kufanya hivyo kesi hiyo itasikilizwa upande mmoja na kutolewa maamuzi. HabariLeo ilipomtafuta Muro kuzungumzia suala hilo alisema kwa kifupi: “Sijapata barua yoyote, mimi nipo Machame nimepumzika najiandaa na sikukuu ya Iddi”.
 
 HABARI KUU LEO BOFYA HAPA 
















Like page yetu ya facebook upate habari kwa urahisi na haraka zaidi BOFYA HAPA


















Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top