Mkude awashusha presha Simba SC




Nahodha wa Simba, Jonas Mkude
  HATIMAYE nahodha wa Simba, Jonas Mkude ameifuata timu yake kambini Morogoro na kuwatuliza mashabiki na wanachama wa timu hiyo kwa kuwamabia yupo pamoja nao.

Simba iliingia kambini mwanzoni mwa wiki hii huku nahodha huyo akibaki Dar es Salaam hali iliyozidisha hofu kwa mashabiki wa timu hiyo kwamba huenda kiungo wao kweli akaondoka.

Mkude inadaiwa kugoma kuongeza mkataba na wekundu hao wa Msimbazi akitaka kuongezewa dau la Sh milioni 80, jambo ambalo uongozi wa timu hiyo haukukubaliana nao.

Mkataba wake unatarajiwa kumalizika Mei mwakani.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mkude alisema alishindwa kusafiri na timu juzi kutokana na matatizo ya kifamilia na kuwataka mashabiki wa Simba kushusha pumzi kwani hajafikiria kuondoka licha ya watu kuvumisha anataka kuondoka.

“Nilishindwa kusafiri na timu jana (juzi) kwa sababu nilikuwa na matatizo ya kifamilia na viongozi wangu wanajua na haina uhusiano na maneno yanayosemwa na watu kuwa nataka kuondoka, leo (jana) nimejiunga na wenzangu kila kitu kipo sawa,” alisema Mkude.

Kitendo cha Mkude kugomea kuongeza mkataba kimefanya uongozi wa Simba kutafuta kiungo mwingine ambapo tayari Mghana James Kotei amewasili kumalizana na timu hiyo.

Hata hivyo, Mkude jana alisema yupo kwenye mazungumzo ya kuongeza mkataba mpya na timu yake na yanaendelea vizuri, imani yake watafikia pazuri.

Mkude hajakosa mechi yoyote ya ligi kwenye mzunguko wa kwanza na ameonesha kiwango kikubwa na kuwalinda mabeki pamoja na kuanzisha mashambulizi kuanzia katikati ya uwanja.

Hivi karibuni baada ya kufunguliwa dirisha dogo la usajili, Mkude amekuwa akihusishwa kutaka kujiunga na Yanga kitu ambacho amekipinga akisema suala hilo halipo akilini mwake, bali ni kumchonganisha na mashabiki ambao wanamuamini.

Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top