Lwandamina hesabu kali

Kocha wa Yanga, George Lwandamina
 

KOCHA wa Yanga, George Lwandamina amesema anakazania suala la ukokotaji mpira kwa wachezaji wake, kama njia rahisi ya kuwasaidia kupata ushindi pindi wanapocheza na timu pinzani. Lwandamina amejiunga na Yanga hivi karibuni na wiki iliyopita ameanza rasmi kukinoa kikosi hicho.

Akizungumza jana, kocha huyo ameeleza umuhimu wa ukokotaji mpira kupitia kwa mawinga na namna ya kuwadhibiti wapinzani. Kocha huyo amekuwa akitatua changamoto moja baada ya nyingine akiamini timu yake itakuwa vile anavyotaka kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili wa ligi.

“Ukokotaji usipotumika vyema, hupoteza uwezo wa timu au washambuliaji kupata magoli, lakini ukitumika ipasavyo ni silaha ya kuwamaliza wapinzani,”alisema.

Alisema ukokotaji wa mpira husaidia kutengeneza nafasi za ufungaji hasa kama wanakutana na mechi ngumu pale ambapo washambuliaji wanadhibitiwa na mabeki.

Hata hivyo alisema, kama mtu atatumia vizuri aina hiyo ya uchezaji ni rahisi kwake kutengeneza nafasi za kufunga lakini kama atashindwa anaweza kutengeneza nafasi na kushindwa kuzitumia na hata kupoteza mwelekeo.

Mbali na ukokotaji, pia ametaja mbinu za ufungaji na upigaji mashuti kama sehemu ya kuwasaidia washambuliaji wake kuwa bora. Kocha huyo anatarajiwa kuja na changamoto mpya za kuendeleza mafanikio ya Hans van Pluijm ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Ufundi katika klabu hiyo.

Kikosi cha Yanga kinaendelea na mazoezi ya maandalizi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania bara kwenye uwanja wa Gymkhana Dar es Salaam ambapo Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit aliliambia gazeti hili jana kuwa hawana mpango wa kutoka nje ya Dar es Salaam.

Yanga ipo nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 33 nyuma ya Simba iliyoa na pointi 35.

Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top