Kiungo Mghana aja na mkwara Simba



James Kotei
 KIUNGO mkabaji wa Ghana, James Kotei amewasili nchini juzi na kutamba kuwa yeye ni wa kusajiliwa Simba na si wa kufanya majaribio
.

Akizungumza baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere akitokea Ghana, Kotei alisema kwa uwezo wake anaamini atasajiliwa Simba na kupata namba.

“Mimi naona kama nimekuja kusajiliwa Simba, sio kufanya majaribio kwa sababu ninao uwezo wa kuchezea Simba kwa kiwango kikubwa tu,” alisema.

Akizungumza Dar es Salaam jana Ofisa habari wa Simba, Haji Manara alisema kiungo huyo wa Medeama ya Ghana atafanya majaribio na benchi la ufundi likiridhika naye atasajiliwa. Mchezaji huyo ni wa pili kwa Simba kutoka Ghana, wiki iliyopita aliwasili kipa Daniel Agyei ambaye amesaini mkataba wa mwaka mmoja.

Katika hatua nyingine, Simba inatarajia kucheza mechi ya kirafiki na timu ya Power Dynamo ya Zambia kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu bara Jumatatu ijayo. Mzunguko wa pili wa Ligi Kuu unatarajiwa kuanza Desemba 17 mwaka huu.

Simba ndio inaongoza msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 35.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Simba, Manara alisema mechi hiyo itachezwa kwenye Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam.

“Ni mechi ya kirafiki ambayo mwalimu aliomba timu ipatiwe mechi ngumu kidogo kabla ya kuanza ligi, hivyo wapenzi na mashabiki wetu waje kushuhudia mechi hiyo ambayo kocha ataitumia pia kuangalia baadhi ya wcahezaji wake wapya,” alisema.

Mpaka sasa Simba imetangaza kumsajili kipa Agyei ambaye hakuna shaka kuwa kocha Joseph Omog atamtumia ili kuona uwezo wake. Endapo Omog ataridhika na Kotei huenda naye akatumia kwenye mechi hiyo kuangalia uwezo wake.

Kikosi cha Simba kiliondoka Dar es Salaam juzi kwenda Morogoro kwa ajili ya kambi ambapo kitarejea Jumapili kwa ajili ya mechi hiyo ya Jumatatu.

“Kocha na benchi lake la ufundi waliomba mechi angalau mbili kabla ya kuanza ligi, hivyo tumetimiza hilo na Dynamo tunatarajia kuwapokea siku moja kabla ya mechi hiyo,” alisema Manara.

Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top