Uamuzi wa kuongezewa muda wa kuwasilisha notisi ya nia ya kukata rufaa dhidi ya dhamana ya Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema, unatarajiwa kutolewa Desemba 20, mwaka huu na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.
Uamuzi huo utatolewa baada ya Lema jana kufanikiwa kuwasilisha maombi yake ya kuongezewa muda wa kuleta notisi hiyo ya rufaa dhidi ya dhamana yake baada ya mahakama hiyo kutupilia mbali pingamizi mbili za mawakili wa Serikali waliokuwa wakitaka maombi hayo yasisikilizwe.
Mbele ya Jaji Dk. Modesta Opiyo wa mahakama hiyo, upande wa Jamhuri ulikuwa ukiwakilishwa na Wakili Hashim Ngole, Matenus Marandu, Elizabeth Swai na Adelaide Kasala huku Lema akitetewa na Wakili Sheck Mfinanga na Faraji Mangula.
Katika maombi hayo namba 69 ya mwaka huu, baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Jaji Dk. Opiyo alisema kuwa atatoa uamuzi huo siku hiyo saa sita mchana.
“Baada ya kusikiliza hoja za pande zote nitatoa uamuzi Jumanne ijayo saa sita mchana, msije asubuhi ili nipate muda wa kupitia hoja zenu,” alisema Jaji Dk. Opiyo.
Awali, akitoa uamuzi wa pingamizi mbili zilizotolewa Desemba 14, mwaka huu na mawakili hao wa Jamhuri, Jaji Dk. Opiyo, aliyesoma uamuzi huo kwa muda wa dakika 50 kuanzia saa 5:30 asubuhi hadi saa 6:20 mchana, alisema ameamua kuzitupa pingamizi hizo baada ya kuziona hazina mashiko ya kisheria.
Alisema kuwa hakuna maombi kama hayo yaliyoacha kusikilizwa mahakamani kwa kushindwa kuonyesha kifungu namba 392 A cha sheria ya uendeshaji wa mashauri ya jinai hivyo akalitupa pingamizi la kwanza la mawakili wa Serikali waliodai maombi hayo hayakufuata utaratibu wa kisheria ikiwemo kutoonyesha vifungu vya sheria waliyoitumia kuleta maombi hayo.
“Baada ya kupitia hoja za pande zote, mahakama imeamua kutupa pingamizi hizo za Jamhuri baada ya kuziona kuwa hazina mashiko kisheria na hata upande wa Jamhuri ulishindwa kurejea shauri lolote ambalo limewahi kufanyiwa uamuzi na mahakama za juu kuhusu suala hilo,” alisema Jaji Dk. Opiyo.
Akizungumzia hoja ya pili ambayo Jamhuri ilidai ya kiapo kinachounga mkono maombi yaliyowasilishwa mahakamani hapo kimekosewa hivyo hakifai kwa sababu wamejumuisha mambo yasiyotakiwa kisheria ikiwemo maoni, mabishano na hitimisho na kubeba hoja za rufaa alisema mahakama hiyo imeondoa aya ya 11 na 12.
Alisema kuwa aya nyingine za 9, 10, 13 na ile ya 17 zitabaki katika hati hiyo ya kiapo kwa sababu hazibebi hoja za rufaa, maoni, mabishano wala hitimisho hivyo mahakama hiyo haiwezi kukataa hati hiyo ya kiapo iliyoambatanishwa na maombi hayo.
Akiwasilisha hoja za maombi ya kuongezewa muda wa kuwasilisha notisi hiyo ili rufaa hiyo iweze kusikilizwa, Wakili Mfinanga, alidai mahakamani hapo kuwa maombi hayo yamewasilishwa mahakamani hapo chini ya kifungu 361(2) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai.
Alidai kuwa uamuzi wanaotarajia kukatia rufaa ni uliotolewa Novemba 11, mwaka huu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha na Hakimu Desderi Kamugisha, ambapo Lema anakabiliwa na kesi namba 440 na 441 za uchochezi dhidi ya Rais Dk. John Magufuli.
Alitaja sababu mbili za msingi za kukatia uamuzi huo rufaa kuwa ni kuiomba mahakama hiyo ipitie makosa ya kisheria yaliyofanywa na mahakama ya chini na kusema kuwa uamuzi huo ulimpa mleta maombi (Lema) dhamana ila kabla hajapewa masharti ya dhamana upande wa Jamhuri ulitoa notisi ya nia ya kukata rufaa.
“Kwa msingi huo mahakama ilisema imefungwa mkono na hawawezi kuendelea na jambo lolote kuhusu suala hilo hata uamuzi wake wa kumpa dhamana haukuwezwa kutimizwa na mahakama haikueleza upande wowote ambao haujaridhika na uamuzi huo una haki ya kukata rufaa,” alidai Mfinanga na kuongeza:
“Kuna vitu muhimu na vitasahihishwa iwapo tutaleta notisi ya nia ya kukata rufaa na rufaa yenyewe kusikilizwa na mahakama yako ambayo ni msimamizi wa haki na sheria ikatoa ruksa ili tuweze kusikilizwa na rekodi ya mahakama ya chini iweze kurekebishwa, ni muhimu mahakama kuzingatia maombi haya pasipo kuzingatia mambo mengine.”
Huku akirejea mashauri mbalimbali ya mahakama za juu, aliendelea kueleza mahakama hiyo kuwa mahakama ikishasema imempa mtu haki ya dhamana lazima itaje masharti ya dhamana.
“Tunaomba mahakama itupatie muda tena mfupi ambao hautazidi hata saa 1:30 kwa ajili ya kuleta notisi hiyo ili mahakama iweze kurekebisha makosa hayo,” alisema.
Akiwasilisha hoja ya pili, Wakili Mangula, alidai mahakamani hapo kuwa tangu kutolewa kwa uamuzi huo hawajapumzika na muda wote walikuwa mahakamani.
Alidai kuwa walikuwa wanaenda mahakamani kwa njia tofauti ili kuiomba mahakama irekebishe makosa hayo ya kisheria.
Alidai kuwa baada ya uamuzi huo kutolewa muda wa kazi ulishaisha na ilikuwa Ijumaa hivyo Novemba 14, mwaka huu walipeleka barua ya malalamiko mahakamani hapo na walipoitwa pande zote mbili katika shauri namba 6 lakini walikumbana na pingamizi zilizowasilishwa na mawakili wa Serikali.
“Novemba 22, mahakama ilitoa uamuzi na kututaka waleta maombi tukate rufaa na hapo mleta maombi alipata haki yake ya kukata rufaa ambayo haikuelezwa mahakama ya chini na tulitoa notisi tukiamini tuko ndani ya muda na hatimaye rufaa ililetwa mbele ya Jaji Mfawidhi Fatuma Masengi,” alidai.
Alieleza mahakama hiyo kuwa katika rufaa hiyo namba 113, walikutana tena na pingamizi la Serikali kuwa wametoa notisi ya rufaa hiyo nje ya muda wa siku moja hivyo hizo ni jitihada walizokuwa wakifanya na si wazembe, wajinga wa sheria kama ilivyodaiwa na wakili wa Serikali.
Akijibu hoja za waleta maombi hao, Wakili Ngole, alidai kuwa ni wazembe, wajinga wa sheria na kuwa hata uamuzi wanaolalamikia mahakamani hapo ambao awali ulimpa mleta maombi dhamana, lakini kabla hajapewa masharti ya dhamana mahakama iliingiliwa mamlaka yake hawajawasilisha na maombi hayo.
Wakili huyo alidai mahakamani hapo kuwa hakukuwa na makosa yoyote ya kisheria kama inavyodaiwa na waleta maombi hao na kudai kuwa baada ya hakimu kusema mahakama inampa mshtakiwa dhamana Jamhuri kwa haki yake walisimama na kuifahamisha mahakama wana nia ya kukata rufaa.
“Ni utaratibu wa kisheria kuwa panapokuwa na notisi ya nia ya kukata rufaa mahakama haiwezi kuendelea na jambo lolote kuhusiana na kesi hiyo, hivyo hakimu asingeweza kuendelea na kesi na inafahamika notisi inasimama badala ya rufaa,” alidai na kuongeza:
“Kwa mujibu wa kifungu 359(1) na 361(1) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai, vinaeleza mtu ambaye hajaridhika na hatua yoyote au uamuzi uliotolewa au kupitishwa anaweza kukata rufaa mahakama za juu.”
Lema anashikiliwa kwa zaidi ya mwezi mmoja katika mahabusu ya Gereza Kuu la Kisongo baada ya kukamatwa Novemba 2, mwaka huu nje ya Viwanja vya Bunge mjini Dodoma ambapo alifikishwa mahakamani Novemba 8, mwaka huu akikabiliwa na mashtaka ya uchochezi dhidi ya Rais Dk. Magufuli.
Post a Comment
Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)