Jicho la 3: MAVUGO ‘AMEKUWA STERINGI’ VS NDANDA SC


Na Baraka Mbolembole

‘Picha limeanza, na tayari, Laudit Mavugo ameteuliwa kuwa steringi!’ Labda ndicho kinachopaswa kusemwa baada ya raia huyo wa Burundi kufunga katika mchezo wake wa kwanza tu wa ligi kuu Tanzania Bara wakati alipoisaidia Simba SC kushinda katika game yake ya ufunguzi wa msimu wa 2016/17 baada ya kuinyuka Ndanda SC mabao 3-1 siku ya juzi Jumamosi.

Ikicheza msimu wa tano pasipo kutwaa ubingwa wa VPL, Simba imeanza msimu mpya kwa kuliondoa ‘jinamizi’ lililokuwa likiwakabili la kushindwa kupata ushindi katika mchezo wa ufunguzi msimu wa 2014/15 walipolazimishwa sare ya kufunganga 2-2 na Coastal Union ya Tanga katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Makosa ya safu ya ulinzi ya Ndanda. Umakini mdogo katika kipindi cha kwanza- kujipanga wakati wa upigwaji wa mipira iliyokufa ndiyo ulizaa goli la kwanza la msimu lililofungwa na Mavugo dakika ya 20’akiunganisha mpira wa faulo uliopigwa na Mohamed Hussein.

Jackson Chove aliweza kuokoa michomo michache na kuendelea kuipa nguvu Ndanda SC ambao walitengeneza mashambulizi mawili tu likiwemo lile lililozaa goli lao la kusawazisha na pekee.

Makosa yaleyale yaliyowagharimu Ndanda na safu ya ulinzi ya Simba ikayafanya na kumruhusu Omary Mponda kusawazisha kwa kichwa akiunganisha mpira wa free kick uliopigwa na wing Kiggi Makasi dakika ya 38’.

Mchezo huo ulianza kwa timu zote kuwa makini. Simba walitawala nafasi ya kiungo na walishambulia sana kupitia kwa walinzi wao wa pembeni. Ndanda walianza kujenga kujiamini baada ya kusawazisha licha ya kutokuwa na michezo yeyote ya kigeni waliweza pia kuwarudisha nyuma Simba na kumshtua kipa wao Vicent Agban.

Kwenye kipindi cha kwanza, Ndanda walionekana kuwabana Simba na kuwafanya washindwe kutengeneza nafasi nyingi za mabao, lakini hali ilikuwa tofauti kwenye dakika 20′ za mwisho za kipindi cha pili, ambapo baada ya kurejea kutoka vyumbani, wachezaji wa Simba walionekana ‘kushiba’ maelezo ya makocha wao Joseph Omog na Jackson Mayanja.

Dakika hizo za mwisho zilishuhudia safu ya ulinzi ya Ndanda ‘ikijichanganya’ na hilo liliwafanya Simba kuwa na uhakika kwamba ilikuwapo nafasi ya kutumia makosa hayo kupata mabao ambayo yangewapa ushindi.

Dakika ya 74’ Muivory Coast, Fredrick Blagnon aliyetokea benchi alifanya kitu kilichoanza kuleta tofauti kwenye mchezo huo. Akicheza game yake ya kwanza ya VPL, aliruka juu zaidi ya walinzi wa Ndanda na kufunga kwa kichwa.

Wakati mashabiki wengine wa Simba wakiamini kuwa mchezo huo ungemalizika kwa sare kufuatia dakika 70′ za soka la kufanana, Shiza Kichuya alikimbia kwa kasi na kwenda kufunga goli la tatu dakka ya 77’.

Simba wameanza na furaha ya aina yake na wachezaji wao wapya wameanza vyema. Licha ya wafungaji wote watatu kuwa ni maingizo mapya kikosi, Jamal Mnyate, Muzamir Yassin, Ahmad Juma, Method Mwanjali pia walikuwa na mchango mkubwa katika ushindi wa timu yao.

Mechi iliyopita ilikuwa nzuri kwa Simba ila sidhani kuwa ‘ni fainali yao kikombe,’ na mechi nyingine dhidi ya Azam FC na Yanga SC zinaweza pia kuwa muhimu.

Simba wana mechi ngumu zinakuja, sawa, lakini wana mechi ambazo hawastahili kupoteza-mechi ambazo kama watashinda, itawaweka wapinzani wao hao tarajiwa kwenye mbio za ubingwa katika matatizo.

Simba wameanza vizuri msimu huu, ila watalazimika pia kuongeza umakini katika nafasi ya kiungo na ile ya ulinzi wa kati.

Wanashambulia sana lakini hawatengenezi nafasi za kufunga kwa wingi. Wanaposhambuliwa beki imekuwa ikicheza vizuri lakini wanapaswa kuongeza kasi zaidi. Kipya nilichokiona ni staa mpya wa timu hiyo akianza kwa kufunga.

Mavugo atafikisha goli kumi? Siwezi kukataa kwamba Simba haitakuwa kwenye vita ya kugombea ubingwa, lakini sina shaka akilini kwamba bado wana-miss vipaji vya kuwawezesha kutwaa ubingwa.

Baada ya kuikabili Azam FC kisha Yanga nitakuwa na majibu kama ‘Mavugo ni staa wa picha za kivita au zile za kihindi.’ Unataka niisifie Simba SC? Kwa kuifunga Ndanda SC, hapana aiseee. Ila nimeona tu kiwango cha kupanda na kushuka.

Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top