Yanga SC wamejitutumua na kufuta makosa yao dhidi ya Prison ya Mbeya na kufanikiwa kuibuka na ushindi mwembamba wa bao pakee la penati katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Katika mchezo huo ambao ulikuwa mkali na wa kusisimua, kila timu ilianza kucheza kwa tahadhari kubwa ili kutoruhusu bao la mapema na kujiweka katika mazingira magumu.
Dakika ya 32, Mbuyu Twite alilimwa kadi ya njano baada ya kumfanyia faulo Benjamin Asukile.
Dakika ya 45 kinda wa Yanga Yusufu Mhilu alikosa bao baada ya shuti lake kupaa nje ya lango la Prisons.
Kipindi cha kwanza kiliisha huku kila upande ukitoka bila kuona lango la mpinzani wake.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kutokana na Prisons kuamua kushambulia hali iliyopelekea mchezo kuwa mgumu kwa pande zote mbili.
Kutokana na hali kuzidi kuwa ngumu Yanga walifanya mabadiliko kwa kumtoa Yusufu Mhilu na nafasi yake kuchukuliwa na Simon Msuva.
Prisons walipata penati baada ya Deus Kaseke kufanya madhambi katika eneo la hatari, lakini penati iliyopigwa na Lambert Sabianka iliokolewa na Beno Kakolanya.
Dakika ya 60 Amissi Tambwe aliingia kuchukua nafasi ya Deus Kaseke.
Yanga walipata penati kufuatia mshambuliaji wao Mzambia Obrey Chirwa kuangushwa kwenye eneo la penati na Simon Msuva kuukwamisha mpira wavuni na kuipa Yanga bao la ushindi.
Mwamuzi alikataa kutoa penati kwa Yanga baada ya Donald Ngoma kufanyiwa faulo ya wazi na beki wa Prison dakika za majeruhi.
Mpaka filimbi ya mwisho inapulizwa, Yanga waliibuka kifua mbele kwa ushindi wa bao 1-0. Matokeo hayo yanaifanya Yanga kuendelea kuwa mbabe wa Prisons baada ya kuibuka na ushindi katika michezo mingi waliyokutana hivi karibuni.
Post a Comment
Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)