Kocha Mkuu wa Yanga, Hans-van-der-Pluijm
KOCHA Mkuu wa Yanga, Hans-van-der-Pluijm amesema silaha kubwa ya kuwaangamiza Stand United katika mchezo wa kesho ni kucheza kwa
kujiamini, kujituma kwa umakini.
Yanga itacheza na Stand United kwenye Uwanja wa CCM Kambarage mkoani Shinyanga ikiwa ni mchezo wao wa pili katika ukanda huo, baada ya mwishoni mwa wiki iliyopita kuifunga Mwadui FC mabao 2-0 katika uwanja huo huo.
Akizungumza na gazeti hili jana Puijm alisema mchezo huo una umuhimu mkubwa kwao ili kujiongezea pointi, ambazo zitawasogeza karibu na wapinzani wao Simba walioko kileleni wenye pointi 13.
“Mchezo huu ni muhimu kwetu, tunawafahamu Stand United ni timu nzuri na kwa kutambua hilo tunawaheshimu, lakini hatuwaogopi kwa hiyo ni lazima tupambane tukijua tunataka nini,” alisema.
Kocha Pluijm alisema maandalizi yake yamekamilika na wako tayari kwa mchezo huo, akijivunia kuwa asilimia kubwa ya wachezaji wake wote wako imara kasoro mmoja ambaye ni Geofrey Mwashiuya kwani ni mgonjwa.
Pluijm alisema anasikitika kukosekana kwa mchezaji huyo kijana anayesumbuliwa na majeraha ya goti kwa muda mrefu, na tangu kuanza kwa michuano ya ligi hakuwahi kucheza.
“ Kwa bahati mbaya, Mwashiuya bado ni majeruhi wa goti, najua anajisikia vibaya kwa kukaa nje muda mrefu, namtakia apone haraka ili kujiunga na wenzake katika michezo inayoendelea, naamini siku sio nyingi ataanza mazoezi,” alisema.
Post a Comment
Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)