Simba yakivaa kibonde, uchambuzi na matarajio ya wengi mechi ya leo, mteremko ama mlima?

VINARA wa Ligi Kuu Tanzania Bara Simba leo wana nafasi ya kuzidi kujichimbia kileleni katika msimamo wa ligi hiyo endapo itawafunga vibonde Majimaji ya Songea katika mchezo utakaofanyika kwenye
Uwanja wa Majimaji.

Simba wana nafasi kubwa ya kujiongezea pointi na hadi kufikisha 16 endapo leo watashinda, huku mabingwa watetezi Yanga wana pointi 10 wenyewe wakicheza kesho na Stand United mjini Shinyanga.

Yanga imecheza mechi nne wakati Simba na Azam FC kila moja imeshuka dimbani mara tano, hivyo Yanga wana nafasi kubwa ya kuifikia Simba endapo watakapocheza kiporo chao.

Wekundu hao wa Msimbazi ambao wameshinda mechi nne na kutoka sare moja watafikisha pointi 16 kama wataifunga Majimaji, ambayo tangu kuanza kwa ligi hiyo imefungwa mechi zote tano.

Hata hivyo, Simba wasitarajie mteremko kutoka kwa vibonde hao na wanaweza kujikuta waking’ang’aniwa na hata kufungwa, kwani Majimaji wanatafuta pakutokea baada ya kuanza vibaya.

Katika msimu uliopita, Simba iliifunga Majimaji kwa mabao 6-1 katika mchezo wao wa kwanza kwenye Uwanja wa taifa Oktoba 31 mwaka jana, kabla ya kutoka suluhu katika mchezo wa marudiano uliofanyika Mei 11 mwaka huu.

Kwa upande wa Azam FC wenyewe, leo watakuwa na kibarua kizito watakapocheza dhidi ya Ndanda FC katika mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.

Azam wako katika nafasi ya tatu wakati Ndanda wenyewe wako katika nafasi ya 11 na watataka kuutumia vizuri uwanja wao wa nyumbani ili kujiongezea pointi baada ya kushinda mchezo mmoja, sare miwili na kufungwa miwili.

Timu hiyo pamoja na unyoge wake, lakini pointi moja imezipata katika sare dhidi ya mabingwa watetezi, Yanga katika mchezo uliofanyika kwenye uwanja wao wa Nangwanda Sijaona.

Mtibwa Sugar wenye pointi tisa watataka kujiongezea pointi tatu wakati leo watakapokuwa wageni wa timu iliyopanda daraja ya Mbao FC ya Mwanza katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu Tanzania Bara. Mbao FC ina pointi nne na iko katika nfasi ya nne kutoka mkiani, hivyo inahitaji kugangamala ili ijiondoe katika nafasi hiyo ya chini.

Timu ya Prisons itaikaribisha Mwadui ya Shinyanga katika mchezo mwingine utakaofanyika kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine mjini Mbeya.

Kesho kutakuwa na mechi mbili kwa mujibu wa ratiba ya Shirikisho la Tanzania (TFF) wakati Yanga watakapocheza na Stand United huku African Lyon wakiwa wageni wa Kagera Sugar katika mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top