Na Baraka Mbolembole
AZAM FC na Simba SC zimekuwa na ‘mwanzo mwema’ kabisa katika ligi kuu Tanzania Bara ( VPL 2016/17) na kila timu ipo katika ‘mchakato’ wa kurudisha taji hilo linaloshikiliwa na Yanga SC kwa misimu miwili mfululizo. Timu hizo mbili (Azam na Simba) zitavaana Jumamosi hii katika mchezo wa mzunguko wa tano katika ligi.
Azam wanashikilia usukani wakiwa na alama kumi sawa na Simba lakini tofauti inakuwapo kutokana na ‘herufi’ kwani kila timu ina wastani wa magoli matano baada ya michezo minne. Timu zote mbili zimefunga magoli 7 na kuruhusu magoli mawili mawili katika nyavu zao.
Vikosi
Vikosi vya timu hizo vyote vipo katika ari nzuri na vimejaza wachezaji wa aina tofauti, wapo wale wenye ujuzi wa kuuchezea mpira na wale wenye kutumia mabavu. Nguvu kubwa ya timu hizo ipo kwenye safu ya kiungo. Wakati kiungo cha Azam FC kikitarajiwa kuongozwa na Himid Mao, Muivory Coast, Kipre Bolou, Mnyarwanda, Migi na Frank Domayo.
Hadi sasa, nahodha wa Simba, Jonas Mkude ameonekana kuwa staa wa nafasi ya kiungo katika kikosi cha Mcameroon, Joseph Omog. Mwinyi Kazimoto alicheza kwa kiwango kizuri vs Mtibwa Sugar, Shiza Kichuya na Muzamiru Yassin wanaweza pia kuanzishwa kwa pamoja katika safu ya kiungo.
Hernandez hana matokeo mabaya hadi sasa na mkufunzi huyo raia wa Hispania alionesha ni namna gani ana uwezo wa kuusoma mchezo wakati kikosi chake kilipotoka nyuma na kusawazisha magoli mawili kisha kushinda kwa mikwaju ya penalti dhidi ya Yanga katika mchezo wa Ngao ya Jamii mwezi uliopita.
Amekisaidia kikosi chake kuzishinda Mbeya City FC na Azam FC katika uwanja wa Sokoine, Mbeya wiki iliyopita. Tatizo pekee ambalo linaweza kumwangusha kocha huyo mbele ya Omog ni upangaji wa kikosi.
Na nafasi ya kiungo kwa sasa inaonekana kuimarika zaidi kwa maana, Himid, Migi, Bolou, Domayo, Yahya, Salum Abubakary wote wapo katika kiwango bora huku Ramadhani Singano akiwa na uhakika wa kuanza katika moja ya nafasi za kiungo wa pembeni.
Azam wana nguvu kuliko Simba na ikiwa watacheza mchezo wa mashambulizi wakitokea kati mwa uwanja watakuwa na nafasi kubwa ya kushinda mechi kwa kuwa Simba si wepesi katika kiungo na beki ya kati.
Michezo minne ya mwanzo ya Omog imekuwa na matokeo ila atahitaji, Mkude aache kupiga ‘pasi mkaa,’ Kazimoto asichoke mapema ili asipoteze game ya kwanza akiwa kocha wa Simba.
Pasi nyingi sana za Simba hupotezwa katikati ya uwanja na aina yao ya mchezo wa pasi fupifupi itakuwa faida kubwa kwa Azam ikiwa wataendelea kucheza kwa umakini mdogo na kupoteza mipira ovyo katikati ya uwanja. Azam wako vizuri, na wana uwezo mzuri wa kupiga pasi ndefu timilifu.
SAFU ZA MASHAMBULIZI vs ULINZI
Bila shaka Azam FC watakuwa na uwezo wa kufunga magoli mawili au zaidi katika pambano hili. Nahodha wao, John Bocco amefunga magoli 6 katika game 14 walizokutana katika VPL na amewahi kufunga magoli matatu kwa mpigo ‘ Hat-trick’ wakati timu hizo zilipokutana katika mchezo wa robo fainali katika michuano ya Cecafa Kagame Cup 2012.
Bocco amekwisha funga magoli matatu hadi sasa katika VPL lakini hajafunga katika mipambano ya Mbeya. Aliikomboa timu yake dakika za mwisho vs African Lyon katika game ya ufunguzi msimu huu na kutengeneza sare ya kufungana 1-1, akafunga mara mbili katika ushindi vs Majimaji FC.
Bocco atafunga kwa msaada wa golikipa wa Simba, Muivory Coasta, Vicent Anghban ambaye hatulii golini na amejenga mazoea ya kutoka na kuwa mbali na lango lake. Mzimbabwe, Method Mwanjali na kijana, Novatus Lufunga watakuwa na kazi ya ziada kumlinda mshambulizi huyo mrefu mwenye shabaha.
Simba imekuwa ikitegemea walinzi wa pembeni kupandisha mashambulizi, kama Azam watagundua mbinu za kumzima mlinzi wa kushoto, Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ basi wataimaliza kabisa Simba. Sijaona ubora wa safu ya ulinzi ya Simba katika game zao zilizopita. Baada ya game hii nitawaambia nachokiona.
Mrundi, Laudit Mavugo ameshafunga magoli matatu katika game nne zilizopita katika VPL, Ibrahim Ajib amefunga mara mbili na wawili hao kwa mara nyingine waanzishwa katika safu ya mashambulizi. Shomari Kapombe atarudishwa katika beki ya kulia ili kutoa nafasi kwa David Mwantika na mmoja kati ya Aggrey Morris ama Muivory Coast, Paschal Wawa katika beki ya kati.
Itakuwa ni jaribio la kweli la safu ya mashambulizi ya Simba. Golikipa, Aishi Manula atakuwa na nafasi ya kufuta makosa mengi ya walinzi wake na umakini wake utaisaidia Azam FC kushinda game hii. Kabla ya mechi mshindi upande wangu atakuwa ni Hernandez na nakiona kipigo cha kwanza cha msimu kwa Simba.
Post a Comment
Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)