Mbunge wa Jimbo la Ubungo Kubenea asema hata mahusiano ya kimapenzi baina ya UKAWA na CCM yasitishwe kwa muda

MBUNGE JIMBO LA UBUNGO KUBENEA

Sakata la wabunge wa Ukawa kususa vikao vya Bunge vinavyoongozwa na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson limefika pabaya baada ya baadhi ya wawakilishi hao kuanza kutowasalimia baadhi ya wabunge
wa CCM.

Hatua hiyo ilikuwa dhahiri jana baada ya Ukawa kutangaza kuwa hawatashirikiana na wabunge wenzao wa chama tawala katika shughuli za kawaida za kijamii, kama vile michezo na kutumia kantini ya Bunge, wakisema wenzao wameanza kuwabagua.

“Kusalimia ni jambo la utamaduni wetu. Nilikuwa namsalimia mbunge wa kike wa Ukawa, lakini hakujibu. Lakini, nikajua ni sababu ya wao kufunga mdomo na plasta, nikamtania au kwa sababu ya plasta hujibu ili isije kudondoka hakuitikia,” alisema Lugola.

Alisema ameshtushwa na hali ilipofikia na hajui sababu za msingi za wabunge wa Ukawa kufanya vitendo hivyo, kinyume na udugu na utamaduni wa Watanzania.

Mbunge huyo machachari, alisema Kubenea alimziba mdomo Msigwa kwa mkono ili asizungumze chochote.

Naye mbunge wa  Sumve (CCM ) Richard Ndassa  alisema jambo wanalolifanya wabunge wa Ukawa siyo jema na halina tija kufanywa na wawakilishi hao wa wananchi.

“Sisi ni wabunge, hivi inapofikia kususa kuongea na wabunge wenzako, hatima yake nini?” alisema.

“Mimi nilienda kuwasalimia kama kawaida ambavyo huwa tunafanya kwa wabunge awe CUF, CCM au Chadema, sasa unavyosusa una maanisha nini,” alilalamika Ndassa.

Alisema kitendo cha kutosalimia ni cha juu sana na kwamba iwapo Ukawa wanashauriwa na mtu basi inawapasa kuchuja mambo mengine, likiwamo hilo la kuwasusa wabunge wenzao.

Juzi Mbunge wa Vunjo (NCCR-Mageuzi), James Mbatia wakati anawaongoza wabunge wa Ukawa kutoka bungeni aliwatuhumu wabunge wenzao wa CCM kuwa wanawabagua

Naye Mbunge wa Ubungo Saed Kubenea   alisema;   “Leo  tumekubaliana hatutashiriki katika michezo na wabunge wa CCM, hilo tumeanza leo asubuhi kwenye mazoezi katika viwanja mbalimbali, hivi sasa tunatafakari hata kutafuta uwanja wetu.


“Tukikutana katika uwanja mmoja, sisi tutatumia upande mmoja na wao watatumia upande mwingine, hatuchanganyani, hata salamu leo kuna mmoja kanisalimia nimekwepesha mkono wangu,”
  
Kubenea alisema hata katika mechi zinazoandaliwa kwa ajili ya timu ya wabunge UKAWA hawatashiriki katika kipindi hiki cha wiki mbili zilizobakia za bajeti.
“Si katika michezo tu, hata katika mahusiano, tumekubaliana kama kuna wabunge wana mahusiano ya kimapenzi na wabunge wa CCM yasitishwe kwa muda wa wiki mbili mpaka tutakavyoamua vinginevyo,” alisema Kubenea. 

Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top