Mali za Yusuf Manji Hatarini Kukamatwa, Kuuzwa


Siku moja baada ya mfanyabiashara Yusuf Manji kuhama kwenye jengo la Quality Plaza, uongozi wa kampuni ya udalali ya Yono umesema kinachosubiriwa ni mfanyabiashara huyo kulipa deni au kukamatwa kwa mali zake.


Akizungumza jana, Mwenyekiti wa Bodi ya kampuni hiyo, Stanley Kevela alisema Manji alipewa siku 14 zilizoanza kuhesabiwa tangu Jumamosi ili kulipa deni.


Alisema endapo siku hizo zitamalizika bila kulipwa, mali za mfanyabiashara huyo zitakamatwa ili kufidia deni la Dola 6.1 milioni za Marekani (zaidi ya Sh13 bilioni) anazodaiwa.


Kevela alisema fedha hizo ni gharama ya kupanga kwenye jengo hilo ambalo ni mali ya Mfuko wa Pensheni wa Watumishi wa Umma (PSPF).


Alisema baada ya kukamilika kwa mchakato huo, kampuni italikabidhi jengo hilo kwa PSPF kwa ajili ya shughuli nyingine.


Mfanyabiashara huyo alipotafutwa jana ili kuzungumzia suala hilo, simu yake ya mkononi haikupatikana.


Mkurugenzi wa kampuni ya Yono, Skolastika Kevela alisema kazi ya kuondoa mali za mpangaji kwenye jengo hilo ilikamilika juzi.


“Kampuni zote zimeshaondoa vifaa na milango ya jengo hilo imefungwa kwa kufuli za kampuni yetu. Tutalisimamia jengo hadi tutakapowakabidhi PSPF,” alisema.


Uamuzi wa Manji kuhamishwa kwenye jengo hilo ulitolewa na Mahakama kutokana na kushindwa kulipa kodi ya pango ambapo alipewa masaa 24 ya kuondoa vitu vyake.

Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top