Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Atembelea Kiwanda Cha Chuma Na Kiwanda Cha Kuunganisha Magari Na Trekta Mkoani Pwani


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameliegiza Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha lifanye maamuzi ya kupima ardhi haraka na kutenga maeneo kwa ajili makazi na viwanda ili kujiandaa na uwekezaji mkubwa.


Ametoa agizo hilo jana mchana (Jumamosi, Novemba 19, 2016) wakati akizungumza na wananchi na viongozi mbalimbali wa Serikali na wa Mkoa wa Pwani mara baada ya kukagua kiwanda cha kutengeneza magari ya zimamoto na matrekta cha Equator SUMA JKT Limited kilichopo Ruvu JKT, wilayani Kibaha mkoani Pwani.


“Jiji la Dar es Salaam limejaa, na Kibaha mjini pia hawana ardhi ya kutosha kwa kimbilio pekee hivi sasa ni Kibaha Vijijini. Baraza la Madiwani fanyeni maamuzi, pimeni ardhi na mtenge maeneo ya makazi, viwanda na taasisi za elimu ili mkipata wawekezaji iwe rahisi kuwapa maeneo,” alisema.


Waziri Mkuu alisema ujenzi wa kiwanda hicho utakuwa mkombozi kwa taasisi nyingi na halmashauri nyingi nchini kwani zilikuwa zinashindwa kumudu bei ya kununua magari ya zimamoto.


“Baadhi ya Halmashauri nyingi zilikuwa zinanunua gari moja kwa sh. milioni 500 na hiki ni kiasi kikubwa mno kwa hiyo kiwanda hiki kitakuwa mkombozi kwa taasisi nyingi na halmashauri zetu,” alisema.


Alisema maeneo mengi nchini yanahitaji magari ya zimamoto lakini yalikuwa yanashndwa kumudu bei za magari hayo.


Aliyataja maeneo hayo kuwa ni viwanja vya ndege, bandari, taasisi zilizo chini ya TAMISEMI kama vile shule za sekondari za bweni, Majiji, miji mikuu, Manispaa na Halmashauri za Wilaya.


Alisema ameguswa kukuta kiwanda hicho pia kina uwezo wa kutengeneza matreka na zana za kilimo (farm implements) kwani asilimia kubwa ya Watanzania ni wakulima na wanategemea jembe la mkono.


“Kupitia kiwanda hiki, matrekta mengi yataunganishwa na nina imani bei itakuwa ya chini ili wananchi waweze kumudu.”


Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Equator SUMA JKT Ltd, Eng. Robert Mangazini alimweleza Waziri Mkuu kwamba asilimia 80 ya ujenzi wa kiwanda hicho imekamilika na kwamba hivi sasa wako kwenhye hatua ya kufunga mitambo. Hata hivyo, alisema wanaisubiri iwasili kutoka India.


Alisema kiwanda hicho kikikamilika kitaweza kuunganisha matrekta 3,000 kwa mwaka na magari ya zimamoto 100 na kubainisha kuwa faida za kuunganisha magari hayo hapa nchini ni kuwa na uwezo wa kuzalisha vipuri ndani ya nchi.


“Tukiweza kuzalisha vipuri hapa nchini kwa asilimia 60, umiliki wa magari haya na matrekta utakuwa ni wa Tanzania na siyo wa kampuni za nje tena. Pia tutakuwa tumefaulu kuhamisha teknolojia kwa vijana wetu,” alisema.


Alisema hadi sasa vijana 60 wamekwishapatiwa mafunzo na wako tayari kuanza kazi mara uzalishaji utakapoanza Machi, 2017.


Kuhusu teknolojia ya utengenezaji wa magari ya zimamoto, Eng. Mangazini alisema kiwanda hicho ni cha pili kujengwa barani Afrika cha kwanza kikiwa huko Bassa, Afrika Kusini.


Mapema, akisoma risala mbele ya Waziri Mkuu, mwakilishi wa Equator SUMA JKT Ltd. Kapteni Farijala Mkojera alisema kiwanda hicho kinamilikiwa kwa pamoja na kampuni ya Equator Automech Ltd ambao wana hisa asimilia 70 na SUMA JKT inamiliki asilimia 30 ya hisa za kiwanda hicho.


Akizungumzia ujenzi wa kiwanda hicho, alisema hadi sasa wamekwishatumia sh. bilioni 1.5 na kwamba hadi ujenzi utakapokamilika, wanatajia kuwa wametumia sh. bilioni mbili. “Ujenzi ukikamilika, tunatarajia kuajiri wafanyakazi 200 katika fani mbalimbali,” alisema.


Alisema wakianza uzalishaji, mbali ya magari ya zimamoto na matrekta, wataweza pia kuunganisha mabasi na zana za kilimo kama vile combine harvesters.


“Tutakuwa tumefanikiwa kuhamisha teknolojia kutoka Russia (magari za zimamoto) na India na Poland (matrekta). Tuna uhakika wa soko hapa nchini katika Jumuiaya za EAC na SADC,” alisema.


Waziri Mkuu amerejea Dodoma mchana huu.


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU 
 

Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top