Na Jacquiline Mrisho-Maelezo
SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi imewaasa vijana waliomaliza shule kuacha kujibetweka bali watumie elimu waliyoipata kujitafutia ajira ili kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira nchini.
Kauli hiyo imetolewa jana Jijini Dar es Salaam na Kaimu Kamishna wa Elimu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Nicholaus Bureta wakati wa ufunguzi wa mkutano wa vijana wa Afrika unaojadili changamoto zinazowakabili vijana katika nyanja mbalimbali za maendeleo.
Bureta alisema kuwa Serikali inatoa elimu bora ili kuhakikisha vijana wanapata uwezo na maarifa yatakayowasaidia kujiajiri hata wasipopata nafasi za kuajiriwa katika taasisi na ofisi za umma pamoja na kuitumia elimu hiyo katika kupambana na vitendo vya rushwa.
“Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 inatutaka tuwe na watanzania walioelimika na wenye mtazamo chanya ambao utahakikisha jamii yetu inabadilika kufikia uchumi wa kati hivyo vijana msikae kusubiri ajira bali mjifunze jinsi ya kujiajiri kutokana na elimu mliyoipata mashuleni”, alisema Bureta.
Kwa upande wake Afisa Habari wa Umoja wa Mataifa (UN), Stellah Vuzo aliwapongeza vijana hao kuamua kukusanyika kuchangia mawazo yao juu ya matatizo yanayowakabili kwani vijana wana nafasi kubwa ya kuhakikisha malengo mbalimbali yanatekelezeka.
Aidha, aliongeza kuwa Umoja wa Mataifa umemteua balozi kijana ambaye anashughulikia ajira za vijana hivyo aliwaomba vijana walioshiriki katika mkutano huo kuyafikisha mawazo hayo kwa balozi huyo ili yaweze kupatiwa ufumbuzi.
Naye Mkuu wa Utafiti kutoka Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (PCCB), Daniel Pundu alisema kuwa tatizo la rushwa haliwezi kuisha endapo vijana hawatashirikishwa hivyo amewasisitiza vijana kushirikiana na Serikali kuchukua hatua za kupambana na rushwa ili kuhakikisha rushwa inaondoka.
“Tunajua kuwa vijana ndio nguvu kazi ya Taifa na ndio sababu tunawasisitiza kupambana na rushwa, kwa kulitambua hilo Serikali imeanzisha vilabu vya wapinga rushwa katika shule za sekondari na vyuo vikuu vikiwa na lengo la kuhakikisha vijana wanahusika kwenye mapambano hayo”, alisema Pundu.
Nafasi zaidi za kazi bofya hapa
Like page yetu ya facebook upate habari kwa urahisi na haraka zaidi BOFYA HAPA
Post a Comment
Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)