MECHI 3 VPL 2016/17 YANGA SC IMESHALETA TOFAUTI, HIVI NDIVYO LIGI ILIVYO…


Na Baraka Mbolembole

TIMU tano hazijapoteza mchezo hadi kufikia raundi ya nne ya ligi kuu Tanzania Bara (VPL) msimu huu. Mabingwa watetezi Yanga SC si tu hawajapoteza mchezo hadi sasa bali katika game zao 3 wamejitengenezea takwimu bora zaidi kuliko timu nyingine 15.

Yanga wamefanikiwa kufunga magoli 6 huku wakiwa hawajaruhusu goli lolote hadi sasa. Wana wastani wa magoli idadi ya juu zaidi ya vinara Azam FC na Simba SC ambao katika game zao nne zilizopita kila timu imefunga magoli 7 na kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara mbili.

Kwa maana hiyo, Azam na Simba wana wastani wa magoli matano kila timu katika michezo yao minne. Azam FC, Simba, Yanga, Stand United na Kagera Sugar ndiyo timu tano pekee ambazo hazijapoteza mchezo.

Huku, Yanga na Kagera zikibaki kuwa timu pekee ambazo hazijaruhusu goli katika nyavu zao. JKT Ruvu, Ndanda FC, Mbao FC na Majimaji FC hadi sasa zinabaki kuwa timu pekee ambazo hazijapata ushindi katika VPL 2016/17.

Timu hizo zinakamata nafasi tano za chini katika msimamo huku Majimaji ikiwa ndio timu iliyopoteza michezo mingi katika ligi. Timu hiyo ya mkoani Ruvuma imeshafungwa michezo minne. Mtibwa imeshapoteza michezo miwili sawa na timu timu za Mbao, Ndanda na Mwadui.

Stand kuwa miongoni mwa timu 5 zisizopoteza mchezo ni kama ‘mshangao’ kwani kila mtu wa mpira anafahamu kinachoendelea katika timu hiyo na mgogoro wa kiutawala jinsi ulivyo. Ligi bado ‘mbichi’ ila uelekeo unaweza kuanza kuonekana baada ya vigogo watatu kushuka uwanjani katika game za wikendi ijayo.

Azam FC itawavaa Simba na Yanga watasafiri hadi Shinyanga kuwavaa Mwadui FC, timu ambayo iliwasumbua sana msimu uliopita. Mbeya City wamekusanya alama 7 katika michezo minne na mchezo wao pekee katika uwanja wa nyumbani msimu huu walikumbana na kichapo kutoka kwa Azam.

Ila timu hiyo ya ‘Kizazi Kipya’ imetoa taswira mpya ya matumaini baada ya michezo minne ya mwanzo. Tanzania Prisons walipoteza game ya kwanza baada kucheza mechi 24 pasipo kupoteza katika uwanja wa Sokoine, bado inaonekana kuwa timu imara ambayo kama ilivyo kwa ndugu zao City wamepoteza game moja moja tu msimu huu, na zote zimechapwa Sokoine na Azam FC.

Kipigo cha 2-1 walichopata kutoka kwa timu ya Simba kina baki kuwa kipigo pekee cha Ruvu Shooting hadi sasa. Timu hiyo iliyorejea VPL msimu huu imekuja na kitu tofauti na ukiondoa kiwango cha waamuzi na kutazama mwelekeo wa timu ndani ya uwanja, ligi ya msimu huu ina mwelekeo mzuri.

Mabadiliko ya ovyo kwa ratiba yataharibu ligi. Kwa sasa waamuzi wameshaanza kutupiwa lawama, hii ina maanisha, watavuruga ligi, labda kwa mapenzi au rushwa. Game 3 VPL 2016/17 Yanga imeanza kujitofautisha, tazama ligi ilivyoanza…

Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top