Mama Mwenye VVU Pamoja na mtoto wake wakutwa wamekufa mlimani

MKAZI wa wilayani Chato mkoani Geita, Rose Joseph (32) aliyekuwa na maambukizi ya virusi vya Ukimwi na mtoto wake mwenye umri wa miaka kati ya minne na mitano, wamekutwa mlimani wakiwa wamekufa katika mazingira ya kutatanisha katika kijiji cha Nafuba kilichoko ndani ya Ziwa Victoria wilayani Bunda mkoani Mara.


Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Nafuba, Zakaria Kachimu alisema tukio hilo liligundulika juzi saa 9:00 mchana katika eneo la mlima huo, baada ya wananchi waliopita katika eneo hilo kuona kwanza mwili wa mwanamke huyo.


Alisema baadaye wananchi walifanikiwa kumtafuta mtoto wake na kumkuta pia akiwa amekufa katika eneo lingine. 


Kachimu alisema mwanamke huyo alifika kisiwani hapo Julai 25, mwaka huu, akiwa na mtoto mdogo wa kiume aitwaye Kababu, akiwa anatafuta kazi ya kuhudumia kwenye mgahawa.


Alisema kuwa kulingana na afya ya mwanamke huyo kudhoofika, kila sehemu alikokwenda kutafuta ajira hiyo alikataliwa. Baada ya kukosa ajira hiyo mwanamke huyo alikwenda kwa jamaa yake ambaye pia ni mwanamke aliyeko kisiwani hapo na kuishi nyumbani hapo.


Baadaye mwanamke huyo alikwenda kutibiwa katika zahanati moja iliyoko kisiwani hapo na ikagundulika kuwa ana mambukizi ya virusi vya Ukimwi na kuambiwa aende katika Kituo cha Afya Kisorya kwa ajili ya kujiunga kwa kupewa dawa za kupunguza makali ya virusi vya Ukimwi (ARVs).


Hata hivyo ilielezwa kuwa mwanamke huyo hakwenda kwenye kituo hicho kama alivyoshauriwa na mganga wa zahanati hiyo.


Aidha, Ofisa Mtendaji huyo alisema siku ya tukio wananchi waliopita katika eneo hilo walikuta mwili wa mwanamke huyo katika mlima huo na kuamua kutoa taarifa, ambapo tena walianza kutafuta mtoto wake na kukuta pia akiwa amekufa katika eneo lingine.


Alisema kuwa chanzo cha vifo hivyo ni cha kutatanisha na kwamba huenda mtoto huyo alikufa kwa njaa.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Ramadhani Ng’anzi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo. Alisema upelelezi unafanyika kujua chanzo cha vifo hivyo.

Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top