MKUU wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP), Ernest Mangu, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju
, hawakutokea kwenye mkutano ulioandaliwa na Tume ya Haki na Utawala Bora jijini Dar es Salaam jana.
Mkutano uliokuwa na lengo la kumaliza mvutano ulioibuka kati ya vyombo vya dola na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Mvutano huo unatokana na amri ya Rais John Magufuli, ya kupiga marufuku kufanyika kwa maandamano na mikutano ya vyama vya siasa hadi mwaka 2020.
Rais Magufuli, hata hivyo, ameruhusu viongozi waliochaguliwa kama madiwani na wabunge kufanya mikutano kwenye maeneo waliyopigiwa kura.
Kupinga amri hiyo, Chadema kimeamua kuitisha maandamano na mikutano ya wanachama na wafuasi wao nchi nzima yatakayofanyika, Septemba mosi, mwaka huu katika operesheni waliyoipa jina la `Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania’ (Ukuta).
Baada ya kuibuka kwa mvutano huo, uliosababisha Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu kukamatwa na Jeshi la Polisi na kufunguliwa mashtaka ya uchochezi, tume hiyo iliwaita IGP Mangu, Kinana, Masaju, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, Katibu Mkuu wa Chadema, Vincent Mashinji na Mkurugenzi wa Taasisi ya Demokrasia (TCD), Daniel Loya.
Hata hivyo, IGP Mangu, Kinana na Masaju hawakuhudhuria mkutano huo kutokana na kile kilichoelezwa kuwa walitoa udhuru.
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bahame Nyanduga, alisema jijini jana kuwa wametoa mapendekezo matatu ambayo yanapaswa kufuatwa na pande zote zinazovutana.
Alisema mapendekezo yao yamelenga kutoa nafasi kwa mahakama kuamua kesi zilizofunguliwa.
Nyanduga aliyataja mapendekezo hayo kuwa ni Jeshi la Polisi na Chadema kusitisha matumizi ya lugha au maneno yenye viashiria vya uvunjifu wa amani, haki za binadamu na utawala bora kwa kuwa lugha hizo hazikidhi matakwa ya sheria.
Alisema wamependekeza Jeshi la Polisi linapaswa kutokutumia maneno "tutawashughulikia wote watakaokaidi amri" kwa kuwa tume inaamini kuwa matumizi ya maneno hayo yanaweza kusababisha matumizi mabaya ya mamlaka ya jeshi hilo.
“Ni katika mazingira haya, tume imepata wasiwasi kuwa endapo matamko haya yataachiwa yaendelee, yana viashiria vya machafuko na uvunjifu mkubwa wa haki za binadamu unaoweza kutokea,” alisema Nyanduga.
Alisema pendekezo lingine ni Chadema kurekebisha msamiati wa mikutano wanayopanga na kuondoa neno udikteta katika mikakati yao ya kisiasa.
Akifafanua kuhusu pendekezo hilo, Nyanduga alisema Tanzania ni nchi yenye taasisi za kidemokrasia na inaheshimu utawala wa sheria na ndiyo sababu Chadema wamekwenda mahakamani.
Alisema Chadema na Jeshi la Polisi wanapaswa kuheshimu mahakama na kuacha kutoa matamko ambayo yanaendelea kuongeza joto kuhusu uwapo au kutokuwapo maandamano na mikutano ya Septemba Mosi, mwaka huu.
Nyanduga alisema pendekezo la tatu ni Chadema kusitisha maandamano yake ili kutoa nafasi kwa mahakama kufanya kazi yake kwa umakini bila shinikizo la muda kuanzia sasa hadi Septemba Mosi.
Alisema kutozingatiwa kwa mapendekezo hayo kutasababisha kutokea kwa uvunjifu wa haki za binadamu na jambo hilo likitokea, wahusika wote watawajibishwa.
Alisema tume ina mamlaka ya kujadili hoja hizo mbili kwa kuzingatia mamlaka iliyonayo chini ya Ibara 130 (1) (g) na (h) ya Katiba ya nchi, kuhusu kutoa ushauri na kutafuta maelewano kati ya viongozi wa serikali na Jeshi la Polisi kwa upande mmoja na uongozi wa Chadema.
Nyanduga aliongeza kuwa mkutano wa jana ulikuwa na lengo la kuzungumzia tamko la Jeshi la Polisi la kuzuia mikutano na maandamano ya vyama vya siasa isiyo ya kiutendaji na tamko la Chadema kuhusu Ukuta.
“Ofisi ya AG, IGP na CCM tuliwaalika, lakini walitujibu kuwa hawataweza kuhudhuria kwa kuwa wana udhuru, hivyo tulikutana na Chadema, Ofisi ya Msajili na TCD (Kituo cha Demokrasia Tanzania), na kukubaliana kutafanyika kikao kuhusu umuhimu wa kudumisha amani nchini,” alisema Nyanduga.
Julai 27, mwaka huu, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alitangaza kuzinduliwa kwa Operesheni Ukuta kwa lengo la chama hicho kufanya mikutano nchi nzima ifikapo Septemba Mosi mwaka huu, baada ya amri ya Rais Magufuli na Jeshi la Polisi kuzuia kufanyika kwa mikutano ya kisiasa na maandamano nchini.
Mashinji Afunguka
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Mashinji, alipotafutwa ili kueleza juu ya mapendekezo ya tume, alisema anashangaa kuambiwa kwamba kuna masuala yaliyojadiliwa kwa kuwa kikao hakikufanyika jana.
“Mbona hicho kikao hakijafanyika? "alihoji. "Kulikuwa na mvutano kwamba kifanyike ama kisifanyike kwa sababu akidi haikutimia, nashangaa kusikia kuna maazimio yamepitishwa.
“Hiyo inaonyesha kabisa ni njama za hao watu ili ionekane kuna kikao kilifanyika, kikao kisingeweza kufanyika kwa sababu hawakuwapo Kinana, IGP, wala AG,” alisema Dk. Mashinji.
Alisema anachojua yeye ni kwamba, wao wanaendelea kama kawaida na maandalizi yao ya mikutano ya hadhara na maandamano nchi nzima hiyo Septemba 1, mwaka huu.
Ajira Zaidi bofya hapa
Post a Comment
Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)