YANGA SC ITAVUNJA REKODI NYINGI, NA KUANZA ‘KIBABE’ CAF

YANGA SC itawachapa MO Bejaia katika mchezo wa kwanza na kufuta ‘mzimu mbaya’ wa miaka 20 iliyopita walipotandikwa 6-0 na Raja Casablanca ya Morocco.

Mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi usiku wa leo si rahisi kwa mabingwa wa
Tanzania Bara lakini timu ambayo imeshinda mara moja tu katika game zake kumi za mwisho haitaweza kuifunga Yanga ambayo imetoka kushinda taji la VPL na kombe la FA mwezi uliopita.

Wakati Yanga ikichezea kipigo cha bao 6-0 dhidi ya Raja mwaka 1999, kimesimama kama kipigo kikubwa zaidi katika historia Yanga kile walikutana nacho katika michuano ya Ligi ya mabingwa (sambamba na Simba SC 6-0 Yanga). Sasa si Morocco, ni Algeria ambako ‘jeshi la wanachi’ linataraji kuvunja rekodi mbalimbali si tu kwa klabu bali hadi kwa nchi.

Ushindi dhidi ya Bejaia usiku wa Jumapili utawafanya Yanga kuwa timu ya kwanza ya Tanzania na pengine Afrika Mashariki kuanza na ushindi katika mchezo wake wa kwanza wa hatua ya makundi katika michuano ya CAF.

Si hivyo tu, bali ushindi utawafanya mabingwa mara 26 wa Bara kuvunja ‘mwiko’ wa kutoshinda katika ardhi ya Mwarabu.

Wakati Simba ilipofanikiwa kucheza hatua ya makundi katika michuano ya ligi ya mabingwa mwaka 2003, mchezo wao wa kwanza tu katika hatua ya makundi dhidi ya Enyimba FC ya Nigeria walikutana na kichapo cha 3-0 ugenini (nusu ya 6-0 waliyopigwa Yanga na Raja, 1996.

MO BEJAIA IMESHINDA GAME 1 TU…

Rekodi ya game kumi za mwisho za MO Beijaia

J’mosi 09/04/16- Zamalek 2 – 0 MO Béjaïa

Ijumaa 15/04/16- MO Béjaïa 1 – 1 USM Blida

J’nne 19/04/16- MO Béjaïa 1 – 1 Zamalek

J’mosi 23/04/16 -JS Saoura 1 – 0 MO Béjaïa

J’mosi 30/04/16- MO Béjaïa 0 – 0 USM El Harrach

J’mosi 07/05/16- MO Béjaïa 0 – 0 ES Tunis

Ijumaa 13/05/16- DRB Tadjenanet 1 – 0 MO Béjaïa

J’nne 17/05/16- ES Tunis 1 – 1 MO Béjaïa

Ijumaa 20/05/16 -MO Béjaïa 2 – 0 MC Alger

Ijumaa 27/05/16- NA Hussein Dey 0 – 0 MO Béjaïa

Wamepoteza game 3 Zote (ugenini)

Wameshinda game 1 (nyumbani)

Sare 6 (nne nyumbani, 2 ugenini)

Wamefunga magoli matano (manne nyumbani, moja ugenini)

Wameruhusu magoli 7 (matano ugenini, mawili nyumbani)

Takwimu hizi zinaonesha namna timu hii ilivyo ya kawaida na si ya kutisha. Kitu kizuri Yanga wanaingia uwanjani wakiwa vizuri kisaikolojia, kiuchezaji, kiutawala na imekuwa katika maandalizi ya ‘vitendo uwanjani na nadharia darasani’ katika kambi ya wiki moja nchini Uturuki.

Amis Tambwe atafunga goli lake la kwanza CAF msimu huu, na hilo litatokea kwa kuwa mshambulizi huyo mfungaji bora wa VPL mara mbili anatambua ujio wa Obrey Chirwa raia wa Zambia ambaye amesainiwa kutoka FC Platnum ya Zimbabwe.

Ili kubaki kikosi cha kwanza, naamini Tambwe atajituma zaidi ya siku zote katika maisha yake Yanga na ‘mtu huyo mwenye target na goli’ atahitaji krosi tu kutoka kwa Mbuyu Twite na Deus Kaseke ambao wataanzishwa katika ‘wing na beki’ ya kulia. Au krosi kutoka kwa Oscar Joshua na Saimon Msuva ambao wanaweza kuanza upande wa beki 3 na wing namba 11.

Yanga ni lazima wacheze sana mipira ya krosi kwa kuwa wana wafungaji na wachezaji wazuri katika upigaji wa mipira ya vichwa.

Tambwe na Donald Ngoma wanaweza kushindana na walinzi imara na kushinda vita ya mipira ya juu na uwezo wao wa kumiliki mipira ya chini utakuwa faida kwa Haruna Niyonzima na Thaban Kamusoko ambao ni chaguo zuri katika eneo la kiungo.

Wachezaji hao wa kimataifa kutoka Rwanda na Zimbabwe ni wachezesha timu wazuri, si wapotezaji wa pasi mara kwa mara na silaha yao kubwa ya kujilinda ni kumiliki mpira. Wanapaswa kucheza katikati ya uwanja tu na kujitahidi kuilinda timu na kupiga pasi ndefu za kukimbiza katika wing au kwa washambuliaji wao wa kati.

Msuva, Kaseke au chaguo lingine lolote lile watapaswa kupiga ‘krosi pasi’ makini za mwisho na pia kurudi hadi katikati ya uwanja na kutafuta mpira unapokuwa katika miliki ya wachezaji wa Bejaia. Kushindwa kukaba vizuri, kupiga pasi mkaa, kujisahau kwa wings itakuwa ni pigo kwa viungo wa kati na kama hilo litatokea Yanga watakuwa hatarini.

DIDA, MBUYU, BOSSOU, KELVIN, OSCAR

Inaweza kuwa safu thabiti ya ulinzi ambayo kama washambuliaji hawatafunga wanaweza kuzuia pia wasifungwe goli/magoli. Waarabu wamekuwa wakitegemea zaidi mipira iliyokufa, krosi na mbinu za kujiangusha ili wapate mikwaju ya faulo za karibu.

Umakini ni silaha ambayo itawabeba sana Yanga lakini wanapaswa kucheza ‘kistaarabu’ zaidi katika ngome ili kuifanya timu ipate matokeo. Jinsi anavyocheza Bossou, kuondosha mipira wakati mwafaka wanapaswa wacheze hivyo pia na walinzi wengine.

Wakati mwingine ni heri mpira utolewe uwe kona kuliko kung’ang’ania kuupeleka mbele bila uelekeo sahihi kwa maana kufanya hivyo ni sawa na kujiweka katika presha na kupoteza mipira hovyo.

Dida atapaswa kupoteza muda ikiwa presha itakuwa kubwa kwa Yanga na muda huo unakuwa mzuri kwa wachezaji wengine kutengeneza vikundi na kujadili namna ya kujikomboa ikiwa Waarabu watatawala mchezo na kufanya mashambulizi mfululizo.

“Kama mtacheza vizuri na kushinda hilo ni bora, na kama hamtacheza vizuri kwa namna yoyote ile hakikisha unashinda mechi kwa namna yoyote ile,” Marehemu, Luis Aragones alisisita hivyo kwa wachezaji wake wakati akiinoa Hispania katika Euro 2008.
Credit:Dauda

Magazeti ya leo jumapili june 19, 2016 bofya hapa

Vibonzo:Katuni tano bora zaidi leo Jumapili June 19, 2016 bofya hapa


HABARI KUU LEO BOFYA HAPA
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top