Huwa sizipendi tetesi za usajili. Japo nalazimika kuzifuatilia lakini ni kati ya mambo yanayoniudhi sana. Zinaniudhi kwa sababu huwa zinanikumbusha nilivyowahi kufanywa mjinga. Nilivyowahi kuamini Yann M’vila anakuja muda wowote. Arsena siyo timu yenye kawaida ya kusajili sana, lakini ni timu ambayo inaweza kushika namba moja kwa kuhusishwa na wachezaji wengi nyakati za usajili. Kumbuka mtu kama Arturo Vidal, mtu kama Julian Draxler, hata huyu Juan Mata, Hata yule Serge Auriel, Wote waliwahi kuonekana wamekaribia kabisa kutua Arsenal.
Achana kabisa na Gonzalo Higuain ambaye alionekana mpaka London akienda kufanya vipimo. Nazichukia sana tetesi lakini sina la kufanya, ni lazima tuongee. Ni lazima sasa tuicheze ngoma inaitwa Jamie Vardy. Amehusishwa kusajiliwa akitokea Leicester. Hizi habari siyo za uongo, ni kweli kabisa Arsenal wamepeleka ofa ya kumsajili kwa £20M. Ilikua ghafla na kinyume cha matarajio ya wengi. Wengi tuliamini kama kuna mtu tunamhitaji kutoka Leicester basi ni Riyad Mahrez kutokana na ukweli kwamba ana sifa zote za kuwa mchezaji wa Arsenal kutokana na uchezaji wake, lakini haikua hivyo.
Tumeenda kwa Vardy, Muingereza mwenye umri wa miaka 29. Sijui alikua wapi siku zote huyu mwanaume. Msimu wa 2014/15 alifunga magoli matano tu. Ghafla akaibuka kuwa mfungaji bora wa ligi msimu uliofuatia. Hii ni sawa na mtu anayepasua kuni kukuta sarafu katikati ya gogo. Maswali hayaishi kichwani. Vardy amekataa kufanya maamuzi yoyote mpaka atoke Ufaransa kwenye michuano ya EURO. Hii ina maanisha bado tuna muda mrefu wa kusubiri, na inanikumbusha jinsi usajili wa Artuto Vidal ulivyoyeyuka ghafla.
Ni ukweli usiopingika kuwa maisha ya Vardy kwenye soka yanaelekea ukingoni sasa. Sidhani kama tarehe kama hii mwaka jana Vardy aliwahi kudhani kuna maisha kama anayoishi hivi sasa.
Kuwa mfungaji bora wa ligi, kuichezea timu ya taifa ya Uingereza na kutakiwa na timu kubwa kama Arsenal.
Vardy ameisaidia Leicester na Leicester imemsaidia Vardy kupandisha thamani yake. Hata ule mkataba aliosaini Februari mwaka huu ambao unampa haki ya kusalia King Power mpaka mwaka 2019, kwake ilikua ni mafanikio makubwa. Kwa umri wake kupata mkataba unaompa mshahara wa £80,000 kwa juma ikiwa ni mara mbili ya ule aliokua akipokea kabla, ni lazima alienda kanisani kushukuru.
Sasa Leicester wanampa zawadi nyingine, kutakiwa na Arsenal. Vardy anatakiwa na Arsenal akiwa tayari alishakata tamaa ya kucheza timu kubwa. Mungu ampe nini?
Angekua yeye ni Shiza Kichuya angeshaweka dole gumba haraka sana, lakini Vardy ni Vardy. Ni meingereza, yupo chini ya mawakala wa KEY SPOTS MANAGEMENT navyeye ni kati ya bidaa zao chache muhimu.
Hawa ndiyo watu wa kati. Ndiyo hawa hawa wanaomsimamia Teo Walcott. Walikuwepo wakati Teo anagoma kusaini mkataba mpya eti mpaka ahakikishiwe nafasi ya kucheza kama Mshambuliaji wa kati.Wana bidhaa chache muhimu na Vardy ameibuka ghafla kuwa moja kati ya bidhaa zao za thamani. Hawa watu wanamiliki wachezaji wengi wa kawaida wa England kama Jordan Henderson, Phil Jones, Ryan Bertrand, James Morrison nk.
Hawa ndiyo waliochelewesha usajili wa Vardy na wanaweza kusababisha asije kabisa kwa sababu wapo kwenhe mpango wa kuongeza thamani yake zaidi.Vardy hawezi kukataa kujiunga na Arsenal, lakini ni lazima ahakikishe dili linakua zuri kwa kadri ya uwezo wake kwa sababu hatarajii kupiga dili nyingine kubwa siku za usoni. Umri wake haumruhusu kujipanga, unamruhusu kufanya.
Shida kubwa ipo kwenye huu mkataba wake wa miaka minne na Leicester. Unaonekana ni mnono na bado ni mbichi. Japo Arsenal wanaweza kumlipa zaidi ya £80,000 lakini mkataba wa Arsenal hauwezi kuwa wa miaka minne na si ajabu ukawa kama ule wa Granit Xhaka unaomtaka afikie kiwango fulani uwanjani.
Mawakala wake hawana uhakika huo. Hawana hakika kama Vardy anaweza kukonga nyoyo kiasi cha kuwawezasha kupata pesa kubwa hivyo ni lazima wahakikishe wanatoa macho kwenye mkataba mpya kama utakuwepo. Nani anajua kama Vardy atarudia kufunga mabao 24?
Kama anaweza kurudia kwa nini asiweze kurudia kufunga mabao matano kwa msimu mzima kama alivyofanya kwenye msimu wa 2014/15?
Napenda kuwaambia mashabiki wa Arsena wanaoshindwa kulala bila kufuatilia usajili wa Vardy kwamba waache kupoteza muda, watulie.Vardy anaweza kuja, au asije lakini yote hayo yatafahamika atakaporudi kutoka Ufaransa. Najua Arsene Wenger hajisikii vizuri kwa sababu alidhamiria kufanya usaliji bila kelele. Ameshindwa, na si ajabu thamani yake ikaendelea kuwa juu kama atafanya vizuri kwenye EURO, na hicho ndiyo KEY SPORTS MANAGEMENT wanakitaka.
Kinachotia moyo ni kwamba Vardy ni Mwingereza na mpaka sasa ni Arsenal pekee wameonesha nia ya kumhitaji. Waingereza huwa hawana ndoyo ya kucheza nje ya nchi yao, hivyo Vardy anaweza kuwa njiani. Tukutane Juma lijalo tujiulize ni mkono gani tumpe Teo Walcott?
Credit:Leonce