JE, WENGER AMEANZA KUBADILIKA?

Moja ya sifa ya watu watokao nchini Ufaransa ni tabia yao ya ubishi, kwenye lugha ya Kingereza kuna msemo usemao “ You can’t teach an old dog new tricks” ama huwezi kumfundisha mbwa mzee mbinu
mipya. Naamini wengi mtakubaliana nami kwamba msemo huu unaweza kutumika kuelezea tabia alizozionesha Arsene Wenger miaka hii ya karibuni.

Wenger ni kocha bora sana, na timu nyingi duniani zinatamani kumpata Wenger kama kocha wao, ila moja ya vitu vilivyomuangusha Wenger na kusabibisha kuwe na msuguano kati ya yeye na mashabiki wa klabu ya Arsenal miaka hii ya karibuni, ni ubishi wake kusikiliza maoni ya mashabiki na wadau wa klabu ya Arsenal na kufanya usajili katika nafasi zinazohitajika klabuni.

Timu ya Arsenal inapohitaji beki yeyeh usajili viungo, inapohitaji mshambuliaji yeye husajili beki. Mara nyingine Arsene Wenger hata hudiriki kutosajili kabisa na pale anaposajili mara nyingi husajili wachezaji wadogo ambao japo wanavipaji sana, bado hawajifikia kiwango cha kuweza kuanza kila wiki katika klabu kubwa kama ya Arsenal na kuiwezesha kugombania makombe makubwa.

Lakini habari zilizojitokeza wiki hii za klabu ya Arsenal kutaka kumsajili mshambuliaji wa Leicester Jamie Vardy zinaashiria kwamba Wenger ametambua makosa yake.

Hii ni aina ya usajii unaonikumbusha msimu wa mwisho wa Alex Ferguson pale alipomsajili mshambuliaji mwingine wa Arsenal Robin Van Persie. Ferguson aliuelezea usajili wa Van persie kama ‘’ndio usajili wangu mkubwa wa mwisho” na ‘’ndiye taa itakayoangaza safari yangu ya mwisho kama kocha wa Man United.”

Van Persie alisajiliwa kwa kiasi cha Paundi million 24 ambacho ni kiasi kikubwa sana kwa mchezaji aliyekuwa na miaka 29 tena mwenye historia kubwa ya majeruhi na ambaye alibakisha mwaka mmoja tu katika mkataba wake. Usajili huu ulikuwa na lengo moja tu, Ferguson alitaka kumaliza miaka yake 25 kama kocha wa Manchester United kama bingwa kwa mara nyingine.


Kilichotokea msimu huo kimebaki kama historia, Van Persie alifanikiwa kucheza msimu mmoja mwingine bora na klabu ya Man United ilifanikiwa kutwaa Ubingwa wa msimu huo huku Ferguson akitangaza kustaafu msimu huo. Nadhani Wenger ambaye ndiye kocha aliyemuuza Van Persie amelisoma somo hili na amelielewa vizuri.

Jamie Vardy 29 siye aina ya mchezaji ambayo Wenger husajili, Wenger hajawahi kulipa zaidi ya Paundi million 10 kwa mchezaji mwenye umri kama wa Vardy kwa hiyo usajili huu wa Vardy utaonesha kama Wenger ameamua kubadilisha “style” yake, ametambua kwamba muda ni sasa na si baadaye.Hana nafasi tena ya kubahatisha na kuomba mambo yote yamuendee sawa katika msimu.


Wenger yuko mwaka wa mwisho katika mkataba wake na Arsenal, na japo ndiye kocha aliyekuwa kazini muda mrefu zaidi barani Ulaya ila kiukweli akiwa na miaka 66 sidhani kama kutakuwa na “guarantee” ya mkataba wake kuongezwa.

Japo wenger aliweza kupunguza presha kidogo baada ya kuiwezesha Arsenal kumaliza nafasi ya pili kwenye ligi juu ya mahasimu wao wakubwa Tottenham, lakini bado maswali mengi yamebaki na bado kuna msuguano kati ya yeye na mashabiki wa klabu ya Arsenal. Wengine wamediriki hata kuomba kocha huyo aachishwe kazi.

Mashabiki wanaamini kwamba japo Wenger ni kocha aliyeweza kuiletea Arsenal mafanikio makubwa sana kuliko kocha yeyote, lakini hiki si kisingizio cha Wenger kufanya chochote kile anachojisikia hata kama kinaonekana dhahiri kabisa kama sio sahihi. Japo yeye mwenyewe amejitetea kwa kusema kwamba bado anahamu ya kushinda, inaonekana kwamba sasa hivi ametambua kwamba kutamani tena hakutoshi sasa hivi anahitajikushinda.

Msimu wa 2016/2017 utakuwa mgumu na wenye upinzani mkubwa, hatujapata kuona kwenye msimu mwingine wowote ule, makocha wakubwa kama Conte, Mourinho, Guardiola na hata Klopp wote wakichuana kugombania kuwa bingwa wa ligi hiyohiyo moja, lakini Arsenal wana timu nzuri iliyomaliza nafasi ya pili msimu uliopita na wameweza kuiboresha zaidi kwa kumsajili kiungo Granit Xhaka ambaye ataleta ukakamavu katika kikosi cha Arsenal.

Lakini moja ya tatizo ambalo linaogopesha mashabiki wengi wa Arsenal, ni ukosefu wa hamu ya kushinda ama udhaifu unaoneshwa na wachezaji wa Arsenal hasa pale presha inapozidi. Mara ngapi tumepata kuona Arsenal kuanza mechi vizuri ila baadaye kujipiga risasi wenyewe kwenye mguu na mwishowe kujiharibia kabisa. Mechi kati ya West Ham, Chelsea na Man United na hata Swansea msimu uliopita ni mifano mizuri kabisa ya hili.

Mshambuliaji mahiri wa zamani wa Arsenal Ian Wright hivi karibuni akiongea na CNN alisema “kocha yeyote duniani anahitaji wachezaji wake kujituma na wawe na hamu ya kushinda kama ile waliokuwanayo wachezaji wa Leicester , ningeambiwa nichukue kitu kwa wachezaji wa Leicester ningechukua hivyo vitu viwili ningechukua umoja wao na hamu yao ya kushinda.”

Wenger yeye kaamua kwenda hatua moja mbele zaidi ya Ian Wright, Wenger kaamua kusajili mchezaji wa Leicester kabisa. Vardy ni mchezaji mwenye tabia ya kushinda hata kabla ya msimu huu, alishafanikiwa kutwaa makombe mengine na klabu yake hii ya Leicester na klabu zake za zamani za Halifax na Fleetwood.

Nahisi wenger anaomba kwamba Vardy ataweza kuleta kitu kipya kwa Arsenal ile njaa na hamu ya kushinda ambayo wachezaji wengi wa Arsenal hawana. Labda hii ndiyo sababu kwanini Wenger ameamua kupuuzia kabisa maneno ya waandishi wa habari kwamba Vardy si mchezaji ambaye atafaa mfumo wake wa pasi fupifupi hadi golini kwani Vardy amezoea kucheza mpira wa Counter-Attack na ndiyo magoli yake mengi yanapotokea.

Labda Wenger ataamua kubadilisha mfumo wake wa kucheza pia mbona vitu vya ajabu zaidi vimetokea duniani.

Ila kitu kimoja ni cha hakika, kitendo cha Wenger kutaka kumsajili mshambuliaji bora wa ligi tena kutoka kwa timu pekee iliyomaliza juu yake kwenye ligi kinaasharia kwamba Wenger sasa yuko serious.

Msimu uliopita moja ya vitu vilivyoiangusha Arsenal ni ukosefu wa mshambuliaji mwenye kasi mwenye uwezo wa kumaliza pasi nzuri za mwisho za Mesut Ozil hasa pale winger wao Alexis Sanchez alipoumia, Jamie Vardy atakuwa suluhisho la tatizo hili na kama ArseneWenger ataweza kusajili beki wa kati mwingine pamoja na Jamie Vardy basi Arsene Wenger anaweza kumaliza msimu ujao kidedea kwa mara nyingine tena.

Wenger alipoulizwa juu ya kitendo cha kustaafu kwa Sir Alex Ferguson alisema “nilishaona dalili misimu kadhaa iliyopita, hata kabla ya msimu kuanza alishatoa dalili kubwa kwamba huu ndiyo msimu wake wa mwisho”, Je usajili huu unaweza kuwa moja ya dalili kwamba Wenger naye anategemea kustaafu hivi karibuni?……Mda utasema
Credit:Dauda
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top