IJUE STORY YA MICHEL PLATINI EURO 1984


Katika jua kali la muda wa majira 1984, Michel Platini alikuwa kijana mdogo mwenye miaka 29. Ilikuwa rahisi kumtambua Platini kwa sababu ya nyusi zake kubwa na Afro lake jeusi ambalo kwa wakati huo ndilo lilikuwa fashion. Platini alikuwa ametoka kushinda Ballon D’or yake ya kwanza mwaka jana tu, baada ya kuibeba Juventus kuchukua ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya kwanza.

Wengi wakimtambua kama kiungo bora zaidi duniani, Platini alijitengenezea jina kama kiungo aliyeweza kufanya kila kitu uwanjani katika klabu za Nancy na Saint Ettiene kabla ya kwenda kuiteka Dunia na Bianconeri ama Juventus. Platini sasa alikuwa na kazi nyingine inamsubiri.

Ufaransa walikuwa wakijiandaa kuwa wenyeji wa Michuano ya Ulaya ambayo kwa wakati huo ilikuwa bado haijatunukiwa jina la Euro. Timu ya Taifa ya Ufaransa haikuwahi kushinda mashindano hayo katika historia yake. Huku taifa zima likitamani ushindi ndani ya ardhi yao mzigo wa mategemeo wote ulishushwa kwenye mabega ya Platini.

Miaka ya 80 ilikuwa mibaya kwa Ufaransa. Nchi ya Ufaransa ilikuwa ikikumbwa na matatizo ya Uchumi m-baya na ukosefu wa ajira vitu ambavyo vilichochea kuwepo na mgawanyiko baina ya wananchi wa nchi hiyo. Euro 1984 ilikuwa nafasi nzuri ya kuleta nchi pamoja na pia kufanya watu wasahau japo kwa muda matatizo yaliyokuwa yanaisumbua nchi hiyo. Kulikuwa na Presha kubwa kwa Les Bleus kuibuka Bingwa na kama kapteni na Nyota wa timu, uwezo wa Platini ndio ulikuwa chachu ya mafanikio ya Ufaransa.

Tangu mwanzo wa muongo huo, uelewano wa Platini na viungo wenzake katika kumi na moja ya Ufaransa Alan Giresse, Luis Fernandez na mzaliwa wa Sudan Jean Tigana ulipewa jina la “Magic Square” ama Mraba wa Ajabu na waandishi wa habari wa Ufaransa. Hadi hii leo safu ya kati hii ya Ufaransa ndiyo inayotumiwa na makocha wengi dunia nzima kama mfano wanapotengeneza timu zao.

Fernandez alicheza kama kiungo mkabaji aliyekuwa na kazi ya kulinda mabeki wake Patrick Battison na Maxime Bossis, Tigana alicheza kama kiungo wa box to tox mithili ya Yaya Toure na Giresse alicheza kama kiungo mtengenezaji. Viungo wote hao walichangia kitu kwenye timu hiyo lakini hakuna hata mmoja aliweza kufikia kiwango cha Platini ambaye jukumu lake yeye ni lilikuwa kufanya kila kitu wanachofanya wenzake kule mbele.

Wakati viungo wenzake walikuwa wamebobea kwenye idara fulani, Platini yeye alikuwa na uwezo wa kufanya kila kitu. Alikuwa fundi, alikuwa anaweza kupiga pasi popote uwanjani, na alikuwa ana jicho lilokuwa na uwezo mkubwa wa kuona pasi za mwisho. Alikuwa kiongozi uwanjani na kipenzi cha mashabiki, alikuwa hodari wa mipira ya adhabu na juu ya hayo yote alikuwa mfungaji mzuri wa magoli na ni magoli yake haya ambayo yaliweza kuipeleka Ufaransa hadi fainali.

Ufaransa walianza michuano hii juni 12 wakiwa kwenye kundi gumu lilokuwa na timu za Denmark, Belgium na Yugoslavia. Mechi ya kwanza ilichezwa uwanjani Parc des Princes huku Ufaransa wakimfunga Denmark kwa ushindi mdogo. Mechi ilikuwa bila-bila mpaka dakika ya 80 na mashabiki wa Ufaransa walikuwa wameanza kukasirikia, baada ya kazi nzuri ya Tigana upande wa kulia mpira ulimshukia Platini na aliweza kujipatia goli lake la kwanza la Euro 1984 na akashingilia kwa kukimbilia kwa mashabiki wake.

Baada ya kuibeba Ufaransa kupata ushindi katika mechi yao ya kwanza, Platini hakuishia hapo bali aliendelea kuonesha maajabu yake. Mechi ya pili ya Ufaransa ilikuwa dhidi ya Belgium na Platini aliweza kujipatia Hat-trick kirahisi kabisa katika ushindi wa 5-0 wa Ufaransa. Goli lake la kwanza lilikuwa zuri sana kwani aliweza kukusanya kijiji cha wachezaji wa timu ya Belgium kabla ya kuweka mpira kwenye neti.

Mechi iliyofuata ya Ufaransa ilikuwa dhidi ya Yugoslavia. Platini alifunga goli lake la tano la mashindano hayo na mguu wake wa kushoto la sita na kichwa na la saba na free-kick iliyopigwa na mguu wake wa kulia. Platini alifanya kitu ambacho washambuliaji wengi wanatamani kufanya alifunga “Perfect Hat-trick”. Japo Yugoslavia alimsumbua sana Ufaransa kwenye mechi hiyo ila wafaransa waliondoka kwenye mechi hiyo wakiamini kwamba wakiwa na Platini chochote kile kilikuwa kinawezekana.

Ilichukua masaa mawili kwa Ufaransa kumfunga Portugal katika nusu fainali. Mechi iliisha 1-1 baada ya dakika 90 za mchezo na katika dakika za nyongeza mshambuliaji wa Portugal Rui Jordao alifunga bao la kuitanguliza Portugal na kuiweka Ufaransa katika hatari ya kuaga mashindano. Lakini haya yalikuwa mashindano ya Ufaransa kwani Jean Francois Domergue alirudisha bao hilo dakika ya 114 na mchezo huu ulionekana kama unaenda mikwaju ya Penati, lakini Platini yeye alikuwa na mawazo mengine kabisa. Tigana alikimbia na Mpira winga ya kulia huku akikusanya rundo la mabeki kabla ya kumtengea mpira Michel Platini aliyepiga shuti juu ya neti la goli huku mabeki wa Ureno wakibaki kutoamini ni kimetokea.

Hatimaye Ufaransa walifika fainali yenyewe, Pambano la mwisho katika safari yao. Walicheza na Spain katika joto kali uwanjani Parc des Princes, uwanja ambao safari yao illianza wiki mbili zilizopita. Baada ya kipindi cha kwanza kigumu Platini aliweza kupenyesha free-kick kwenye mikono ya Kipa wa Spain Luis Arconada. Platini alishangilia kwa kupiga magoti huku akiachia mikono yake.Ufaransa walishinda mechi hiyo 2-0 ila kiukweli mechi hii ilikuwa ya Platini tu. Alipanda juu kupokea kombe lake na akalipiga busu moja kabla ya kulibeba juu.

Hadi hii leo bado anashikilia rekodi ya magoli mengi kwenye michuano ya Euro licha ya kwamba hakushiriki Euro nyingine yeyote zaidi ya ile ya 84. Alifunga magoli tisa kwenye michuano hiyo na aliipa Ufaransa ushindi kwenye kila mechi aliyocheza.

Timu ya Ufaransa iliyoshinda Euro 1984 ilibadilisha mpira milele, makocha wengi wamejaribu kuiga safu ya kati ya Ufaransa iliyojulikana kama the ‘Magic Square’ na safu ile imetumika kama mfano katika timu bora zaidi zilizowahi kutokea duniani.

Michuano ya Euro ya 1984 ilimuandika Platini daima kwenye historia ya mpira wa Ufaransa, Platini alihakikisha kwamba yeye ndiyo atakuwa kipimo ambacho viungo wote daima watalinganishwa .Platini alipokea shangwe kutoka kila upande na hakika wafaransa daima hawatosahau ushindi ule kwani Platini alibadilisha jinsi wafaransa wanavyouchukulia mchezo wa mpira milele.
Habari Kuu leo Bofya hapa
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top