Hatima ya shauri lililofunguliwa na Chadema dhidi ya Polisi kupinga amri ya kupiga marufuku maandamano na mikutano ya kisiasa itajulikana Juni 21, Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza itakapotoa uamuzi
kuhusu pingamizi lililowasilishwa na upande wa utetezi kuomba litupiliwe mbali.
kuhusu pingamizi lililowasilishwa na upande wa utetezi kuomba litupiliwe mbali.
Jaji Mohamed Gwae anayesikiliza shauri hilo, alifikia uamuzi huo baada ya kusikiliza hoja za mawakili wa pande zote za utetezi na mleta maombi.
Awali, Mawakili wa utetezi, Robert Kidando na Obadia Kajungu waliomba Mahakama kutupilia mbali maombi ya Chadema kuruhusiwa kufungua kesi yaliyowasilishwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, kwa madai kuwa hayajakidhi mahitaji ya kisheria.
Akifafanua, Wakili Kidando alidai mleta maombi hajataja baadhi ya vifungu muhimu ikiwamo kifungu cha 5(1)(2), vinavyoipa Mahakama mamlaka ya kisheria kusikiliza na kuamua maombi hayo.
Madai hayo yalipingwa na mawakili wa Chadema; Gasper Mwanaliela na John Mallya waliodai hoja za wajibu maombi hazina uhalali kisheria kwa sababu hati ya maombi yaliyopo mbele ya Mahakama yamekidhi mahitaji ya kisheria.
Wakili Mallya alidai kisheria, hati ya maombi inapaswa kuwa na vitu vitatu muhimu; hati ya kiapo, maelezo ya mleta maombi na ombi la shauri kusikilizwa kama inavyoelekezwa na kifungu cha 5(3).
Wakili Mallya aliomba Mahakama kutupilia mbali pingamizi la upande wa utetezi na kumpa nafuu mleta maombi, kesi yake kusikilizwa na kuamuliwa.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Jaji Gwae aliahirisha shauri hilo hadi Juni 21, Mahakama itakapotoa uamuzi huku akiuagiza upande wa utetezi kuwasilisha hati kinzani kujibu hoja za mleta maombi.
Katika maombi ya msingi, Chadema inaomba Mahakama kutamka kuwa amri ya polisi na utekelezaji wake ni batili, kwa sababu ni kinyume cha katiba na sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 1992.
HABARI KUU LEO BOFYA HAPA