Sakata la kufukuzwa kutoka kwenye huduma Mchungaji JOHN MHINA wa kanisa la Anglikana Mtaa wa Mtakatifu Andrea Magomemi Dayosisi ya Dar Es Salaam, limechukua mkondo mwingine, kufuatia waamini wa kanisa hilo kuondoa katika madhabahu ya kanisa hilo kiti cha Askofu wa Dayosisi ya Dar Es Salaam, Askofu Dokta Valentino Mokiwa, wakipinga kitendo chake cha kumfukuza Mchungaji huyo kwa madai kuwa ni sababu binafsi na si za kitumishi.
Kwa mujibu wa wawalikishi wa Waamini hao ambao ni wazee wa kanisa hilo, kitendo cha Askofu Dokta Mokiwa, kumfukuza Mchungaji huyo, kinalenga kuficha ukweli na kupotosha mambo kufuatia mgogoro wa mkataba wa ujenzi ambao kanisa hilo limeingia na mwekezaji mmoja ndani ya eneo la kanisa hilo na kwamba mtumishi huyo ndiye anayefahamu kila kitu juu ya mkataba huo.
Wakati wa Ibada iliyoongozwa na Mchungaji aliyefukuzwa, JOHN MHINA, mzee wa kanisa, ARCHIE KILLO, alisoma maamuzi magumu yaliyochukuliwa na baraza hilo ikiwamo kupinga uhamisho huo mpaka pale mgogoro wa msingi utakapotatuliwa, kumzuia mchungani mpya kuhudumu mahala hapo, na kuomba rasmi kujiondoa kutoka Dayosisi ya Dar Es Salaam na kuwa chini ya Askofu Mkuu wa kanisa hilo, Dokta Jacob Chimeledya.
Katika hatua nyingine, Askofu wa Dayosisi ya Dar Es Salaam, Dokta Valentino Mokiwa, kupitia kwa Afisa habari na mawasiliano wa Dayosisi hiyo, YOHANA SANGA, amekiri kufahamu maamuzi yaliyofikiwa na kanisa hilo na kwamba mchungaji aliyepangwa kuchukua nafasi ya Mchungaji Mhina, atapangiwa mtaa mwingine, huku akimshutumu Mchungaji MHINA kwa kukaidi mara kadhaa wito wa kuwa na mazungumzo, hivyo iwapo mtaa huo utashikila msimamo wake, atapeleka suala hilo ngazi ya juu.
Post a Comment
Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)