Mvutano umeibuka kati ya Naibu Spika, Dk Tulia Ackson na wasemaji wa kambi ya upinzani walipokuwa wakisoma maoni yao kuhusu miswada iliyowasilishwa bungeni baada ya kusoma utangulizi uliokuwa nje ya hoja.
Katika Bunge la Bajeti lililoisha Juni mwaka huu, upande wa Kambi ya Upinzani Bungeni uliingia kwenye mgogoro na Dk Tulia, hali iliyosababisha wabunge kutoka vyama vinavyounda Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi) kutoka bungeni kila Naibu Spika alipokuwa akiendesha vikao.
Jana, ilikuwa mara ya kwanza tangu wabunge wasusie vikao vinavyoendeshwa na Dk Tulia kukubali kuwapo ndani ya Bunge, hatua iliyotokana na viongozi wa dini kuingilia kati sakata hilo.
Tangu kuanza kwa Mkutano wa Nne wa Bunge la 11, imepitishwa miswada miwili huku wapinzani wakisoma utangulizi wa maoni kueleza jinsi wanavyobanwa kufanya shughuli za siasa.
Hata hivyo, jana ilikuwa ni tofauti baada ya Dk Tulia kuwabana wawasilishaji wa miswada ya Sheria ya Uanzishaji wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, ambao ulisomwa na Dk Godwin Mollel na aliyesoma Muswada wa Uanzishaji Baraza la Watalaaluma wa Kemia ni Ester Matiko.
Katika maoni yao, Matiko na Dk Mollel walieleza jinsi Polisi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), wanavyowapiga na kuwakamata wananchi wanaojadili masuala ya siasa. Dk Mollel alipinga watu kunyimwa haki ya kutoa maoni, kufanya mikutano ya hadhara na maandamano. “Tupinge unyama unaondelea dhidi ya Watanzania wenzetu,” alisema Dk Mollel.
Hata hivyo, kabla ya kumaliza kile alichokuwa akitaka kusema Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Ajira, Kazi, Vijana na Walemavu), Dk Abdallah Posi aliomba mwongozo kwa kutumia kifungu namba 68 (1) akitaka msemaji kujielekeza katika hoja kama kinavyotaka kifungu 86.
Baada ya Dk Tulia kutoa mwongozo wa kutaka kuacha kusoma maneno ya utangulizi huo, Dk Mollel alitii na kuendelea na hoja iliyokuwa mezani.
Hali ilizidi kuwa mbaya baada ya Matiko kuingia kusoma maoni ya kambi hiyo kuhusu Muswada wa Sheria ya Uanzishwaji wa Baraza la Wanataaluma wa Kemia.
“Watanzania wote wenye mapenzi mema tupinge vyombo vya dola vinavyotumika kufanya shughuli za siasa,” alisema Matiko.
Licha ya Dk Possi kuomba mwongozo wa Spika, Matiko aliendelea kusoma maneno ya utangulizi ambayo aliambiwa asiyasome.
Wakati mvutano huo ukiendelea, baadhi ya wabunge wa upinzani walisimama kupinga uamuzi wa Dk Tulia wakitaka wasemaji hao kuendelea kusoma utangulizi.
Hata hivyo, Dk Tulia aliwataka kukaa chini huku akimtaja Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee kwa zaidi ya mara mbili akimsihi kukaa hali aliyokubaliana nayo.
Post a Comment
Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)