Rais Magufuli Kuwa wa Mwisho Kuhamia Dodoma


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Rais John Magufuli atakuwa wa mwisho kuhamia Dodoma na kupokewa na watumishi wa Serikali.


Rais Magufuli akihutubia Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM Julai 23 mwaka huu, mkoani hapa alitoa tamko la Serikali kuhamia Dodoma ikiwa ni utekelezaji wa uamuzi ulitolewa mwaka 1973.


Akizungumza Jumatano wiki hii, katika kipindi cha Safari ya Dodoma kilichoandaliwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Majaliwa alisema utaratibu wa kuhama umepangwa kutekelezwa kwa awamu sita.


Alisema awamu ya kwanza itaanza mwezi huu hadi Februari mwakani, ikiongozwa naye, mawaziri wote, makatibu wakuu, naibu katibu mkuu na idara angalau moja.


“Awamu ya pili itaanza Machi hadi Agosti, 2017. Katika kipindi hicho makatibu wakuu watapendekeza na kuomba fedha bungeni kwa ajili ya kazi hiyo,” alisema.

Kwa utaratibu wa Bunge, mikutano ya bajeti huanza Aprili hadi Julai ili kujadili na kuidhinisha mapato na matumizi ya Serikali ya mwaka mpya wa fedha.


Majaliwa alisema awamu ya tatu itaanza Septemba hadi Februari, 2018 na zitaendelea nyingine, ya mwisho ikiwa mwaka 2020.


Akizungumzia miundombinu, Majaliwa alisema Dodoma ina barabara za kutosha, nyingi zikiwa za lami na hata zisizo za lami zinapitika vizuri.


Majaliwa alisema kuna barabara ya kuunganisha mikoa mingine kama vile Singida, Morogoro na Iringa, hivyo kuwafanya watu kuingia na kutoka mjini hapa kwa urahisi. Kwa upande wa masoko, alisema yapo makubwa yenye vyakula vya kutosha.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu), Jenista Mhagama hivi karibuni alisema ujenzi wa makazi, uzio na ofisi binafsi za waziri mkuu umekamilika.


Mhagama alisema kilichobaki ni kazi ya uboreshaji wa mandhari ya eneo la makazi hayo yaliyoko Mlimwa, mjini hapa na barabara za kuunganisha kati ya makazi hayo na nyingine kubwa.


Alimwagiza Mkuu wa Mkoa wa


Dodoma, Jordan Rugimbana kuhakikisha mandhari ya eneo hilo yanaboreshwa ikiwa ni pamoja na kupanda maua.


Rugimba pia alipewa jukumu la kusimamia ujenzi wa barabara zinazounganisha makazi hayo na nyingine zilizopo maeneo hayo.
 

Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top