Nguvu zote kwa Mtibwa- Simba



WEKUNDU wa Msimbazi Simba wamejitapa kuendeleza makali katika mchezo ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mtibwa Sugar utakaochezwa keshokutwa.

Simba imetoa tambo hizo baada ya kushinda mabao 2-1 dhidi ya Ruvu Shooting katika mchezo wa juzi kwenye Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam. Simba sasa ina pointi saba sawa na Azam baada ya kushinda mechi mbili na kutoka sare moja.

Akizungumza juzi baada ya mechi hiyo Msemaji wa Simba, Haji Manara alisema muhimu kwao ni pointi na sio maneno ya vichochoroni na kwamba malengo yao ni kushinda kila mchezo.

“Tulisema Simba ni timu kubwa, tulipanga kupata pointi tatu kwa Ruvu na tumepata, na sasa tunaangalia mbele na kujipanga na Mtibwa Sugar ili kuendeleza makali yetu kwa kuhakikisha ni mwendo mdundo, haturudi nyuma,” alisema.

Manara alisema anaamini Kocha Joseph Omog ameyaona mapungufu ya timu yake katika mchezo uliopita dhidi ya Ruvu na kwamba atayafanyia kazi ili yasijirudie wakati ujao.

Manara alimtania msemaji wa Ruvu Shooting Masau Bwire kuwa asiilinganishe timu ya Simba na Ruvu kwani wao (Simba) wako juu akimtaka kutozungumza maneno ya uchochoroni na badala yake kusubiri matokeo ya uwanjani.

Kwa upande wa Bwire ambaye awali alijitapa timu yake itamkimbiza Simba kwa fimbo, alisema wamefungwa kwa bahati mbaya kwani siku hiyo hawakuwa na bahati huku akiendelea kutoa vijembe kuwa sio timu ya kutisha kama inavyotamba.

Alisema wanajipanga katika mchezo wao ujao dhidi ya JKT Ruvu akisema unaweza kuwa mgumu kwa vile kila mmoja atahitaji matokeo mazuri.

Kocha wa Ruvu Shooting Seleman Mtungwe alisema kufungwa huko kulitokana na makosa yao katika safu ya ulinzi na kwamba ni wazi kuwa aliumia kwa kuwa alijipanga akitarajia kupata pointi tatu.
 

Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top