Yanga yakabidhiwa rasmi taji la ubingwa wa VPL


Yanga imekabidhiwa taji lao la ubingwa wa VPL msimu wa 2015-16 baada ya kufanikiwa kulitetea taji hilo ambalo walilitwaa msimu uliopita. Yanga imepewa kombe hilo ikiwa na pointi 74 huku ikiwa na mchezo mmoja mkononi baada ya kuifunga Ndanda FC kwenye uwanja wa taifa.


Ndanda walianza kupata goli kwa mkwaju wa penati Omary Mponda lakini bao hilo lilisawazishwa na Simon Msuva dakika chache baadaye. Donald Ngoma akaifungia Yanga bao la pili na kuiweka mbele klabu yake lakini Salum Minely akachomoa bao hilo na kuilazimisha Yanga kwenda sare kwenye uwanja wa taifa ambao Ndanda ndiyo walikuwa wenyeji katika mchezo huo.


Waziri wa Kilimo na Mifugo Mh. Mwigulu Nchemba ambaye alikuwa mgeni rasmi wa mchezo huo alilikabidhi kombe hilo kwa nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ baada ya kumalizika kwa mchezo kati ya Ndanda FC Yanga dhidi ya Yanga uliomalizika kwa timu hizo kutoka sare ya kufungana magoli 2-2.


Ubingwa huo unawafanya Azam FC kulikosa taji hilo ndani ya misimu miwili mfululizon wakati Simba wao wameendelea kulikosa taji hilo ndani ya misimu minne mfululizo.


Mambo muhimu kufahamu
Yanga wametwaa ubingwa wao wa ligi kwa mara ya 26 kwenye historia ya klabu hiyo

Ubingwa wa msimu huu ni wa pili mfululizo baada ya kuunyakua msimu uliopita na kufanikiwa kuutetea kwa mara nyingine.

Nadir Haroub ‘Cannavaro’ amenyanyua kombe hilo kwa mara ya pili akiwa kama nahodha wa kikosi cha Yanga. Msimu uliopita, Cannavaro alinyanyua ndoo hiyo kwa mara ya kwanza akiwa kama nahodha wa Yanga aliyerithi majukumu hayo kutoka kwa Shadrack Nsajigwa.

Donald Ngoma, Thabani Kamusoko, Vicent Bosou, Isoufour Boukabar, Paul Nonga, Geofrey Mwashiuya, Deus Kaseke, Haji Mwinyi, Benedict Tinoco na Matheo Anthony ni wachezaji ambao wametwaa taji hilo kwa mara ya kwanza baada ya kujiunga na Yanga msimu huu.
Yanga walitangaza ubingwa wakiwa na pointi 68 baada ya Simba kupoteza mchezo wao dhidi ya Mwadui, leo walikuwa wanakabidhiwa kombe hilo bila kujali kama wangefungwa, kutoka sare au kushinda dhidi ya Ndanda FC.

Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top