CCM Yaijibu CUF kuhusu Ushindi Dimani, Yatoa siri mbili za ushindi wa kata 19 kati ya 20


Baada ya Chama cha Wananchi (CUF) kudai kuwa uchaguzi wa marudio uliofanyika Januari 22, 2017 ulikiuka sheria na taratibu za uchaguzi katika baadhi ya vituo hasa vya jimbo la Dimani, na kwamba ndio sababu ya mgombea wake Abdulrazak Khatib Ramadhan kushindwa katika uchaguzi huo.


Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeibuka na kujibu tuhuma hizo za CUF huku ikiilaumu kwa kushiriki kuuvuruga uchaguzi wa awali wa mwaka 2015.


Wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam, Katibu wa Uenezi na Itikadi CCM, Humphrey Polepole ameishauri CUF kutafuta chanzo cha kushindwa kwake, kwani CCM haijashiriki kwa namna yoyote ile kupora ushindi huo.


“Matokeo ya Dimani yamedhihirisha CUF ilikua tatizo tangu uchaguzi uliopita, 2015 CCM ilipata kura 4400, CUF 2300, 2017 CCM imepata kura 4860 sawa na 78% CUF wamepata 1200 anguko la zaidi ya 50%,” amesema na kuongeza.


“CUF wanamtafuta wa kumuwekea lawama, sisi tunasema kushindwa kwao na kura zao kupungua lazima kuna mchawi ndani yao wenyewe hasa Zanzibar, wamtafute huyo mchawi sisi tumewapa ushauri ili wajiweke sawa.”


Aidha, Polepole ameeleza siri mbili za ushindi wa kishindo wa kata 19 kati ya 20 katika uchaguzi mdogo wa marudio nchi nzima, ambapo amesema kuwa utendaji wa Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli pamoja utekelezaji wa ahadi alizoahidi katika kipindi cha kampeni za uchaguzi Mkuu wa 2015 ndio sababu ya wananchi kuchagua wagombea wa CCM kwa kishindo.


“Rushwa, Ufisadi, ni adui wakubwa wa serikali ya awamu ya tano, pia inatekeleza ahadi zake zinazogusa wananchi moja kwa moja ikiwemo elimu bure kuanzia Darasa la kwanza hadi kidato cha nne,uboreshwaji wa huduma za kijamii, utilewaji mikopo kwa kina mama na vijana, ujenzi wa viwanda ambapo hutoa fursa za ajira kwa wananchi wanyonge,” amesema.


Ameongeza kua “Hizo ni siri mbili kubwa zilizotufanya tushinde kata 19 na jimbo la Dimani kwa kishindo.”


“Baadhi ya wanasiasa wanatutisha kwamba 2020 tutakutana tutaachia madaraka, kama wanatutabiria giza, kwetu CCM tuna mwanga mkubwa unaotupa hamasa ya kufanya kazi zaidi ili kuwaletea watanzania mabadiliko ya haraka,” amesema.


Amesema mwelekeo wa CCM kwa sasa ni ujenzi wa chama hicho ikiwa pamoja na kufanya uchaguzi wa viongozi ili kupata viongozi bora, wazalendo, wanaochukia rushwa na ufisadi, ubadhirifu pamoja na watakao kuwa tayari kusikiliza wananchi na kuwatumikia.

Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top