Picha: Rais Magufuli alivyokutana na kufanya mazungumzo na muwekezaji Aliko Dangote Ikulu Dar es Salaam


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli jana tarehe 10 Desemba 2016, amekutana na kufanya mazungumzo na Mmiliki wa Kiwanda cha Saruji cha Dangote kilichopo Mtwara, Alhaji Aliko Dangote.

Katika mazungumzo hayo, Rais Magufuli alimhakikishia mfanyabiashara huyo kuwa serikali ya Tanzania itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji wote nchini katika kutimiza lengo lake la kuwa na Tanzania ya Viwanda.

Rais Magufuli alisema kuhusu kiwanda cha kuzalisha Saruji cha Dangote kilichopo Mkoani Mtwara hapakuwa na tatizo lolote ila kulikuwa na watu ambao walitaka kujinufaisha binafsi kupitia mradi huo kwa kufanya biashara za ujanja kitu ambacho serikali yake haikiruhusu.

Alimtaka Dangote kununua gesi moja kwa moja kutoka TPDC ambacho ni chombo cha serikali badala ya kutumia watu ambao wamekuwa na nia ya kutengeneza faida tu.

”Iwapo unataka maelezo yoyote ama lolote linalokukwamisha uwasiliane na viongozi wa serikali badala ya kuwasiliana na watu ambao wako kwa ajili ya kufanya biashara ya ujanja ujanja kwa lengo la kupiga dili ” alisema Rais Magufuli.

Dokta Magufuli alisema Dangote ametaka eneo dogo ambalo angelitumia kusafirishia saruji yake wakajitokeza watu ambao wametaka kumuuzia kwa shilingi bilioni 43 kitu ambacho hakina uhalisia wowote bali ni watu ambao wanataka kutengeneza faida kitu ambacho hakiwezekani.

Kwa upande wake mmiliki wa Kiwanda cha kuzalisha Saruji cha Dangote, Alhaji Aliko Dangote alishangazwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa amefunga kiwanda kwa sababu amekatazwa kuagiza makaa ya mawe toka nje ya Tanzania kitu ambacho amesema hakiingii akilini kwa sababu makaa ya mawe ya Tanzania ni rahisi na yana ubora kuliko kuagiza nje.

Katika kuthibitisha hilo, tayari Mfanyabiashara huyo ameingiza malori mapya 600 kwa ajili ya kusambazia saruji yake.

Aliongeza kuwa lengo la kufanya biashara hapa nchini mbali na kutengeneza faida pia ana lengo la kuisaidia serikali ya Tanzania kutengeneza ajira hivyo hana sababu ya kuagiza mali ghafi toka nje ya nchi ambazo zinapatikana nchini.

Alhaji Dangote alimuhakikishia Rais magufuli kuwa ataendelea kufanyakazi na Serikali ya Tanzania na kamwe hana nia yoyote ya kufunga kiwanda chake kama inavyodaiwa na baadhi ya vyombo vya habari bali ana mpango wa kuangalia fursa nyingine zaidi za uwekezaji hapa nchini kutokana na uwepo wa sera nzuri za uwekezaji chini ya Serikali ya Awamu ya Tano.



Mmiliki wa Kiwanda cha Saruji cha Dangote kilichopo Mtwara Alhaji Aliko Dangote akimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli mara baada ya mazungumzo yao Ikulu jijini Dar es Salaam.

Mmiliki wa Kiwanda cha Saruji cha Dangote kilichopo Mtwara Alhaji Aliko Dangote akizungumza mara baada ya kumaliza mazungumzo yake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam. Wakwanza kushoto ni Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo.


Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top