NEC yatangaza ratiba ya chaguzi ndogo za Ubunge na Madiwani

Na Eliphace Marwa – MAELEZO

TUME ya Taifa ya Uchaguzi imetangaza ratiba ya uchukuaji wa fomu za kujaza nafasi zilizo wazi ya Mbunge na Madiwani katika maeneo mbalimbali hapa nchini.


Imesema kuwa inatarajia kuendesha Uchaguzi Mdogo katika Jimbo la Dimani , Mkoa wa Mjini Magharibi ,Tanzania Zanzibar kufuatia kifo cha Mbunge wa Jimbo hilo.


Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo jijini Dar es salaam na Tume hiyo, hatua hiyo itanatokana na vifungu vya 37(1)(b) na 46(2) vya sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na Vifungu vya 13(3) na 48(2) vya Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Sura 292.


Aidha ,Tume hiyo pia itaendesha Uchaguzi Mdogo wa kujaza nafasi za wazi za Udiwani katika kata 22 kwenye baadhi ya Halmashauri za Tanzania Bara zilizokuwa wazi kutokana na sababu mbalimbali.


Imezitaja Kata hizo Ng’hambi ya Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma, Ihumwa ya Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma, Kiwanja cha Ndege ya Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Igombavanu na Ikweha za Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa pamoja na Ngarenanyuki iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Meru Mkoani Arusha.


Kata nyingine ni Kijichi ya Halmashauri ya Manispaa ya Temeke Mkoani Dar es Salaam, Kata ya Kinampundu ya Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mkoani Singida, Isegehe ya Halmashauri ya Mji wa Kahama Mkoani Shinyanga, Kasansa Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe Mkoani Katavi, Malya na Kahumulo Mkoani Mwanza, Maguu na Tanga Mkoani Ruvuma pamoja na Kata ya Kimwani Mkoani Kagera.


Imeongeza kuwa Kata nyingine ni pamoja na Nkome Mkoani Geita, Kata ya Lembeni Mkoani Kilimanjaro, Mkoma ya Mkoani Mara, Duru ya Mkoani Manyara, Mwamtani ya Mkoani Simiyu, Misugusugu ya Mkoani Pwani pamoja na Mateves ya Mkoani Arusha.


Tume hiyo imesema kuwa zoezi la kutoa fomu za uteuzi litaanza Desemba 10 hadi 22 na kufuatia kwa zoezi la uteuzi wa wagombea siku ya tarehe 22 mwezi Desemba na Desemba 23 hadi Januari 21 mwakani itakuwa ni kipindi cha kampeni ambapo Januari 22 mwakani itakuwa siku ya kupiga kura.

Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top