Tume ya Uchaguzi nchini Gambia imemtangaza mgombea wa upinzani, Adama Barrow, kuwa mshindi wa uchaguzi wa rais uliofanyika Jumapili na kuna taarifa kuwa tayari Rais Yahya Jameh amekubali kushindwa.
"Ni jambo la kipekee kwamba mtu ambaye ametawala nchi hii kwa kipingi kirefu kama hiki amekubali kushindwa," mwenyekiti wa tume ya uchaguzi, Alieu Momar, aliwaambia waandishi wa habari muda mchache kabla ya kutaja rasmi matokeo ya uchaguzi huo mjini Banjul hivi leo (Ijumaa, Novemba 2).
Tume hiyo ya uchaguzi inasema Barrow amepata asilima 45.5 ya kura, huku Jammeh akipata asilimia 36.7.
Jammeh, ambaye mara moja alikuwa amesema kuwa angelitawala kwa miaka bilioni moja Mungu akipenda, alikuwa akijaribu kuwania wadhifa huo kwa mara ya tano kupitia chama chake cha Alliance for Patriotic Reorientation and Construction (APRC).
Televisheni ya taifa ya Gambia ililiambia shirika la habari la AFP kwamba Jammeh angelitoa taarifa yake baadaye kumpongeza Barrow.
Barrow, mwenye umri wa miaka 51, alikuwa ni mfanyabiashara asiyejuilikana sana lakini akateuliwa na muungano wa upinzani kupambana na Jammeh aliyekaa madarakani kwa miaka 22, akijikuta kuwa ana ufuasi mkubwa uliokuwa haukutazamiwa.
Barrow kuongoza serikali ya mpito
Ikiwa kweli Rais Jammeh atatangaza kushindwa, Barrow anatazamiwa kuhudumu muhula wa miaka mitano akiongoza serikali ya mpito kuelekea mageuzi rasmi ya kidemokrasia kwenye koloni hilo dogo la zamani la Uingereza, maarufu kwa fukwe zake.
Meneja wa kampeni wa Jammeh, Yankuba Colley, alisema hakuwa akijuwa chochote kuhusiana na tangazo la mwenyekiti wa tume ya uchaguzi, lakini alikuwa na hakika kuwa kama raia wa Gambia wameamua rais huyo aondoke, basi ataondoka.
"Ikiwa watu wa Gambia wametoa hukumu yao, yeye ni muumini mzuri," aliliambia shirika la habari la AFP, akiongeza kuwa: "Ni matokeo mabaya lakini mtu ninayemjuwa mimi atakubali vyovyote yatakavyokuwa."
Timu ya Barrow ilithibitisha tangazo la Tume ya Uchaguzi.
Uchaguzi huo wa Alhamis ulikumbwa na kuzimwa kwa huduma za Intaneti, hatua iliyosababisha lawama kali kutoka makundi ya haki za binaadamu na Marekani.
Lakini matokeo ya awali asubuhi ya Ijumaa yalikuwa mazuri kwa Barrow, baada ya kuutwaa mji mkuu, Banjul, ambao awali ulikuwa ngome madhubuti kwa Jammeh.
Barrow alishinda takribani asilimia 50 ya kura kwenye majimbo matatu ya Banjul kwa mujibu wa tume ya uchaguzi, ikilinganishwa na asilimia 43 za Jammeh.
Vikosi vya usalama vilimiminwa kwa wingi mitaani, kukiwa na wasiwasi kwamba huenda Jammeh asingekubali matokeo ya kura hiyo. Hadi nyakati za alfajiri, wanajeshi, polisi na maafisa wa vyombo vyengine vya usalama walionekana kwenye vizuizi vya barabarani, huku raia wakisalia majumbani mwao kufuatilia matokeo
Post a Comment
Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)