Na Baraka Mbolembole
NIMEPENDEZWA sana na usajili wa golikipa bora zaidi Tanzania katika ‘karne mpya,’ Juma Kaseja ambaye amejiunga na kikosi cha Kagera Sugar FC ya Bukoba.
Misimu mitatu ya mwisho katika soka la Tanzania Bara haikuwa mizuri kwa Kaseja.
Mara baada ya kumalizika kwa mkataba wake katika timu ya Simba SC msimu wa 2012/13, Kaseja-mshindi wa mataji 7 ya ligi kuu Bara alikaa nje ya uwanja kwa miezi 6 na baada ya kufunguliwa kwa dirisha dogo la usajili mwishoni mwa mwaka 2013, kipa huyo mwenye miaka 31 hivi sasa alijiunga na Yanga SC kwa mara ya pili mwezi Desemba.
Kushindwa kuudhibiti mpira uliokuwa ndani ya uwezo wake katika mchezo wa ‘Dar es Salaam-Pacha’ dhidi ya Simba na kumruhusu Awadh Juma kuifungia Simba goli la tatu katika mchezo wa Nani Mtani Jembe-2013 kuliwafanya baadhi ya wanachama na mashabiki wa Yanga kumlaumu hadharani na kusema walifungwa 3-1 na mahasimu wao hao kutokana na uwepo wa Kaseja katika kikosi chao.
Kaseja alirudishiwa mpira na mlinzi, Mbuyu Twite na alipojaribu kutaka kumpiga chenga Awadh ikashindikana na kiungo huyo wa Simba akaunasa mpira na kufunga goli la tatu.
Maisha ya kimpira ya Kaseja yalianza kuyumba baada ya mechi ile. June 2014, Yanga ilimsaini mkufunzi Mbrazil, Marcio Maximo ambaye alidaiwa kuwa na bifu na Kaseja tangu akiinoa timu ya Taifa-Taifa Stars.
Mkataba wa Yanga na Kaseja ulikuwa na kipengere kinachosema ni lazima laseja awe kipa chaguo la kwanza katika timu hiyo.
Maximo hakufanya hivyo, alikuwa akiwatumia makipa wake wote-Deogratius Munish, Ally Mustapha na hadi anatimuliwa baada ya kuisimamia Yanga katika mechi 7 za VPL, Mbrazil huyo alimtumia Kaseja katika mchezo mmoja tu jambo lililomkera kipa huyo mshindi wa Cecafa Challenge Cup 2010 akiwa na kikosi cha Tanzania Bara.
Kaseja alijiondoa Yanga na msimu wa 2015/16 alisajiliwa na Mbeya City FC ikiwa ni timu yake ya nne katika ligi kuu ya Tanzania Bara.
Mwaka 2001 akiwa na miaka 17, Kaseja alicheza ligi kuu Bara kwa mara ya kwanza akiwa na kikosi cha Moro United. Mwishoni mwa mwaka 2002 alisajiliwa na Simba SC ambako alidumu hadi June 2008 alipojiunga na Yanga kwa mara ya kwanza. June 2009 akarejea Simba alikocheza hadi June 2013.
Kaseja alicheza vizuri katika kikosi cha City msimu uliopita, lakini tangu kuanza kwa msimu huu mwezi Agosti mchezaji huyo hakuwa kikosini.
Sababu kubwa iliyomfanya Kaseja kutojiunga na City si ushindani wa namba bali kutolipwa stahiki zake ikiwemo pesa zake za usajili.
Kujiunga na Kagera Sugar wakati huu timu hiyo ikianza kunyanyuliwa upya na kocha kijana Mecky Mexime ni uamuzi mzuri sana.
Kaseja ni mchezaji anayependa kucheza, anajituma sana katika uwanja wa mazoezi, ni kingozi mzuri ndani na nje ya uwanja. Mecky amefanya chaguo zuri sana ambalo litasahihisha makosa ya mara kwa mara yaliyokuwa yalifanywa na David Baruhani na kipa aliyesimamishwa kwa madai ya kuihujumu timu hiyo, Hussein Shariff.
Ikiwa nafasi ya nne katika msimamo baada ya kukusanya alama 24(pointi 11 nyuma ya vinara Simba,) Kagera imeruhusu magoli 16 katika michezo 15.
Paul Ngwai, nahodha, George Kavila, Danny Mrwanda na sasa Kaseja, bila shaka kocha Mecky amekusanya wachezaji wazoefu ambao wanaweza kusaidiana na vijana kama Anthon Matogolo, Ibrahim Twaha, Mbaraka Yusuph, Edward Christopher na wengine kuimarisha kikosi cha mabingwa hao wa Tusker Cup 2006.
Naamini usajili huu wa Kaseja pale Kagera Sugar utamrejesha katika midomo yetu ‘Tanzania One’ bora zaidi katika miaka hii ya 2000.
Kaseja ataisaidia pia timu yake mpya kwa sababu ni mtu mwenye kujituma, mbinu za ushindi na uwezo wa kuwaunganisha wenzake na kuwafanya wawe wamoja.
Post a Comment
Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)