Treni Yanusurika Kuchomwa Moto na Wananchi, Vioo 30 vya Mabehewa Vyapasuliwa, 17 Watiwa Mbaroni


TRENI ya abiria inayofanya safari zake kati ya Kituo Kikuu cha Reli na maeneo ya Pugu Dar es Salaam maarufu kama ‘Treni ya Mwakyembe’ nusura ichomwe moto juzi, baada ya wananchi kudai kuchoshwa na usumbufu wa shirika hilo.


Wananchi hao walitaka warudishiwe nauli zao kwa kile walichodai Shirika la Reli Tanzania (TRL) limeshindwa kuwa na ratiba inayoeleweka.


Tukio hilo lilitokea juzi saa 3:00 usiku eneo la Majumbasita, baada ya treni hiyo kukaa kituoni hapo kwa muda mrefu bila kuambiwa kuambiwa chochote.


Hali hiyo iliwafanya abiria kuvamia kituo kidogo cha mawasiliano kilichopo eneo hilo wakitaka warejeshewe nauli zao vinginevyo wangekichoma moto pamoja na mabehewa ya treni hiyo.


Mwandishi aliwashuhudia abiria wakitaka kuingia ndani ya kituo hicho huku wakiwalazimisha wafanyakazi waliokuwapo wawarudishie fedha zao za nauli.


Purukushani hiyo iliyodumu kwa takribani saa mbili ilimalizika kwa abiria hao kuvunja vioo vya mabahewa ya treni vipatavyo 30.


Wafanyakazi kuona hivyo walijifungia ndani ya kituo hicho huku polisi waliokuwa wakisindikiza treni hiyo wakitimua mbio kunusuru maisha yao.


Baadhi ya abiria walisema tangu Ijumaa iliyopita wamekuwa wakipata usumbufu kwa kukatishiwa tiketi huku treni ikichelewa na wakati mwingine kutoonekana kabisa.


Walisema jambo hilo limekuwa likiwasababishia hasara na kuwalazimu kutafuta usafiri mwingine na kuchelewa kufika kwenye majukumu yao.


Kufuatia kukithiri vitendo vya uharibifu wa miundombinu ya reli na treni vinavyofanywa na baadhi ya wananchi, Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) kupitia kwa Mkurugenzi Mtendaji , Masanja Kadogosa imetoa onyo kwa wananchi kutofanya vitendo hivyo.

“Tukio hili si mara ya kwanza kujitokeza, lilijitokeza tarehe 24, 26 na 28 mwezi wa 10 na Novemba 7 Katika matukio hayo kulitokea uharibifu wa miundombonu na kujeruhi baadhi ya wafanyakazi wa TRL akiwemo Mustapha Omary ambaye ameshonwa nyuzi 8 katika hospitali ya mnazi mmoja,” amesema.

Amesema kutokana na uharibifu huo, watuhumiwa 17 wanashikiliwa na jeshi la polisi na kwamba upepelezi ukikamilika watachukuliwa hatua za kisheria.

Kadogosa amedai kuwa, wahusika wa fujo na uharibifu huo ni makondakta wa dalala kwa lengo la kutisha wananchi kutoutumia usafiri wa treni.

“Kuna watu wa daladala wanafikiri wataendelea kufanya fujo ili wananchi waone kuwa usafiri wa treni si salama wapande magari yao, sisi hatulazimishi wananchi kuutumia usafiri wetu ila kutokana na ubora wa huduma zetu wanakuja wenyewe. Pia hatusitishi kutoa huduma kwa sababu ya fujo zao sababu tutawatesa abiria wetu zaidi ya 21,000,”

Naibu Kamishna wa Polisi na Kamanda wa Reli, Simon Chillery amesema jeshi la polisi linaendelea kufanya uchunguzi ili kubaini wengine waliohusika.
 
 

Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top