Lipumba Amtaka Maalim Seif Aache Kudanganywa na Waganga wa Kienyeji

Mgogoro wa uongozi ndani ya Chama cha Wanachi (CUF) unaendelea kuzua mapya ambapo jana, Mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba alimvaa tena Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad.


Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Makao Makuu ya chama hicho zilizoko Buguruni jijini Dar es Salaam, Profesa Lipumba alimtahadharisha Maalim Seif akimtaka aachane na ‘waganga’ kwani watamdanganya.


Ingawa hakueleza ni waganga wa aina gani, Profesa Lipumba alimtaka Maalim Seif kukubali kuzungumza naye ili wamalize matatizo yao.


“Haiwezi kubadilika kwamba Mwenyekiti wa chama hiki nikiwa hai hadi mwaka 2019… Maalim waganga watakudanganya sana, watakudanganya sana,” alisema Profesa Lipumba.


“Katika hili lilitakiwa lisifike hapa, huna sababu, njoo tuzungumze, pokea simu yangu unajua namba yangu tuzungumze tuyamalize uje nikupangie kazi,” aliongeza.


Mchumi huyo alisisitiza kuwa hatakubali chama hicho kiuzwe kwa bei nafuu kwa vyama vingine vya kisiasa au kwa aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema akiungwa mkono na vyama vya upinzani vinavyounda Ukawa, Edward Lowassa.


Kwa upande wake Maalim Seif ameendelea kushikilia msimamo wake akieleza kuwa Profesa Lipumba ni msaliti wa chama hicho na ana lengo la kukivuruga.


Alisema kuwa yeye yuko tayari kukaa naye meza moja kwa lengo la kueleza hadharani kile alichokiita uongo wake na sababu halisi iliyomfanya ajiuzulu nafasi ya Uenyekiti siku chache kabla ya kuanza kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top