Kesi ya kumtukana Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo, inayomkabili Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless lema na mke wake
Neema Lema (33), imeshindwa kusikilizwa maelezo ya awali.
Hatua hiyo ni baada ya Mbunge huyo kukwama kuletwa Mahakamani toka Mahabusu kwa sababu zisizojulikana.
Kukosekana kwa Mbunge huyo kuonekana Mahakamani, kulimlazimu Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha Agustino Rwezile kutoa amri ya kutolewa hati ya kumtoa Mahabusu mshitakiwa huyo na kumleta mahakamani hapo ili kesi hiyo isikilizwe maelezo ya awali.
Hata hivyo tangu amri hiyo itolewe saa nne asubuhi hadi saa saba mchana mshitakiwa hakuweza kuletwa mahakamani hapo, licha ya mke wake kuwepo mahakamani hapo.
Rwezile alimtaka wakili wa serikali kueleza sababu za kushindwa kumleta Lema Mahakamani wakati Mahakama imetoa amri.
Wakili wa serikali Fotunatus Mhalila alisema mshitakiwa ameshindwa kuletwa Mahakamani kutokana na sababu zisizozuilika , ila kwa sababu upelelezi umekamilika aliomba Mahakama ipange tarehe ya usikilizaji wa hoja za awali.
Majibu hayo yalipingwa vikali na Wakili wa utetezi, John Mallya ambaye alitaka kufahamu sababu za kutomleta Lema anazodai hazikuweza kuzuilika ni zipi na kwa nini zisitajwe mahakamani.
“Mheshimia hakimu hizo sababu zisizoweza kuzuilika ni zipi, Wakili wa seriali atueleze, tujue kama siyo amedharau mahakama licha ya kutakiwa kumleta mshitakiwa,” alisema.
Baada ya hoja hizo kutolewa Hakimu Rwezile aliendelea kusisitiza hati ya kumtoa Mahabusu itolewe ili aletwe Mahakamani leo katika kesi hiyo, ambayo itasikilizwa hoja za awali.
Awali katika kesi hiyo Godbless Lema na mke wake Neema, alisomewa mahitaka kuwa kati ya Agosti 20 Mwaka huu ndani ya Arusha,walimtumia ujumbe wa simu ya kiganjani Mkuu huyo wenye lugha ya matusi , huku wakijua ni kosa kisheria.
Ilidaiwa kuwa ujumbe huo ulitumwa kutoka 076415**47 namba 075655**18 kwenda namba 0766-75**75 ukidai, “Karibu, tutakuthibiti kama Uarabuni wanavyothibiti mashoga.” Washitakiwa walikana shitaka hilo na walipatiwa dhamana
Post a Comment
Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)