Joseph Mungai Kuwagwa Leo Dar, Mwili wa Samwel Sitta Kuwasili Leo


Mwili wa aliyekuwa Waziri wa Elimu, Joseph Mungai unatarajiwa kuagwa Dar es Salaam leo katika viwanja vya Karimjee.


Akizungumza na waandishi wa habari jana, mtoto wa marehemu, William Mungai alisema ibada ya kuuaga mwili huo itafanyika katika viwanja hivyo saa 5.00 asubuhi.


Hata hivyo mtoto huyo wa marehemu hakutaka kuingia kwa undani kuhusu chanzo cha kifo cha baba yake, badala yake alisema familia iachwe iendelee kushauriana na daktari.


Alisema pamoja na hayo, kifo hicho kimewashtua kwa vile kimetokea ghafla na kwamba baada ya kuisha kwa ibada ya kuaga mwili huo, utasafirishwa hadi Mafinga, Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa kwa mazishi.


“Hadi sasa familia tunajua kwamba marehemu aliugua tumbo la kawaida na tulimpeleka hospitalini ambako alifariki dunia, tunaomba familia iachwe, kwa sababu bado tunashauriana na daktari wake.


“Tumekubaliana mwili wake uagwe kesho (leo) saa tano Viwanja vya Karimjee ambako pia historia yake yote na familia itasomwa,” alisema William.


Kifo cha Mungai kilitokea juzi jioni katika kile kilichoelezwa kuwa alianza kujisikia vibaya baada ya kunywa kiywaji katika hoteli moja iliyopo Msasani, ambayo aliizoea.


Mmoja wa waombelezaji waliofika nyumbani kwa marehemu jana ni pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)- Zanzibar, Salum Mwalimu ambaye alimwelezea Mungai kuwa aliunga mkono mabadiliko ya siasa.


“Hakuwa na kadi ya Chadema lakini alipenda mabadiliko, mwanaye William aligombea ubunge wa Mafinga kupitia Chadema na baba yake alimuunga mkono,” alisema.


Mbunge wa zamani wa Kwela, Chrisant Mzindakaya alisema amesikitishwa na kifo hicho ikizingatiwa wiki iliyopita walikuwa pamoja na walizungumza mambo mengi ya siasa.


“Hakuwa na kesho katika maisha yake, alilokuwa na uwezo wa kulifanya alilifanya siku hiyo hiyo, alikuwa na msimamo, hakukubali kuyumbishwa,” alisema Mzindakaya.


Wakati huohuo, mwili wa aliyekuwa Spika wa Bunge, Samuel Sitta unatarajiwa kuwasili leo ukitokea Ujerumani ambako alikuwa akitibiwa hadi mauti yalipomfika.


Taarifa zilizotolewa na msemaji wa familia ya marehemu, Gerald Mongella, zinasema mwili huo utawasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere saa 9.00 mchana na kupelekwa nyumbani kwake Msasani, Dar es Salaam.


“Ijumaa(kesho) saa tatu asubuhi ibada ya kuuaga mwili huo itafanyika katika viwanja vya Karimjee ambako ndugu na wakazi wa Dar es Salaam watapata fursa ya kuaga,” alisema Mongella.


Mwili wa Sitta utasafirishwa hadi Dodoma ambako utaagwa na wabunge na baadaye utasafirishwa kwenda Urambo kwa mazishi Jumamosi.


Sitta alifariki Novemba 07 mwaka huu katika Hospitali ya Technal University alipokuwa akipatiwa matibabu ya maradhi ya saratani ya tezi dume.
 

Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top