Wizara ya Mambo ya Nje yatoa kauli juu ya taarifa za Tanzania kujitoa katika matumizi ya Viza ya Pamoja ya Utalii katika Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.



Mchakato wa kuanzisha Viza ya Pamoja ya Utalii katika Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Ndugu wanahabari:
Wiki iliyopita baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya jamii ya hapa nchini na nje ya nchi iliandika taarifa kuhusu Tanzania kujitoa au kugomea
utaratibu wa visa ya pamoja ya utalii (Single Tourist Visa) wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kufuatia taarifa hiyo, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imekuwa ikipokea simu nyingi kutoka kwa watu mbalimbali wakiwemo waandishi wa habari kutaka kufahamu ukweli wa jambo hilo.

Hivyo, Wizara imeona itoe taarifa rasmi kufafanua namna ya mchakato wa uanzishwaji wa viza ya pamoja ya utalii ndani ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki unavyoendelea.

Suala la Uanzishwaji wa Viza ya Pamoja ya Utalii kwa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki bado liko katika majadiliano ya Nchi Wanachama kupitia Vikao vya Sekta ya Utalii na Wanyamapori.


Katika kufanikisha azma hii, Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Maliasili na Usimamizi wa Wanyamapori uliofanyika tarehe 1 Novemba 2008 liliunda Kikosi Kazi kwa ajili ya kufanya utafiti kwa lengo la kubainisha mahitaji na utayari wa Nchi wanachama juu ya kuanzisha Viza ya Pamoja ya Utalii. Utafiti uliofanyika mwaka 2010, ulibainisha masuala muhimu yafuatayo ya kuzingatiwa kabla ya kuanzishwa kwa Viza ya Pamoja ya Utalii:

a)Kurazinisha (harmonization) sheria za Viza za Nchi Wanachama;
b)Idara ya Uhamiaji kuanzisha Mfumo wa kudhibiti Usalama;
c)Utoaji wa Viza kuwa wa kielektroniki;
d)Kuwepo kwa mfumo wa ukusanyaji na ugawanyaji wa mapato pamoja na namna ya kulipa;
e)Kuwepo kwa maafisa uhamiaji katika kila ofisi za ubalozi;
f)Kujenga uwezo wa watumishi kwenye suala la mfumo wa kieletroniki wa utoaji wa viza ya pamoja ya Utalii.

Kufuatia matokeo ya utafiti huo, Mkutano wa 5 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Utalii na Usimamizi wa Wanyamapori uliofanyika mwezi Julai 2013 jijini Bujumbura, Burundi pamoja na mambo mengine uliagiza kuundwa kwa kikosi kazi ambacho kitajumuisha wataalamu kutoka Taasisi za Uhamiaji, Utalii, Fedha, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Tehama, Usalama, na Sheria katika nchi wanachama ili kuandaa mpango kazi na kushughulikia masuala yote ambayo yatajitokeza kuhusiana na uanzishwaji wa Viza ya Pamoja ya Utalii. Hata hivyo, kabla ya utekelezaji wa maagizo hayo, Nchi za Uganda, Kenya na Rwanda zilianzisha Viza ya Pamoja ya Utalii baina yao nje ya vikao vya Jumuiya.

Ni vema ikaeleweka kwa umma wa Watanzania na Afrika Mashariki kwa Ujumla kuwa kwa kuzingatia Mfumo wa Maamuzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambao ni wa kukubaliana kwa pamoja (consensus) hakuna Mfumo wowote wa uanzishwaji wa Visa ya Pamoja ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ulioanzishwa.

Hii inamaanisha kuwa hakuna Visa ya Pamoja ya Utalii katika Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyokubalika. Kwa mantiki hiyo, taarifa zilizotolewa na vyombo vya habari hazina ukweli wowote na zilikuwa na lengo la kuichafua Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inawawahakikishia umma wa Tanzania kuwa itaendelea kuheshimu maamuzi ya vikao halali vya Jumuiya na kushiriki katika majadiliano ya kuanzisha visa ya pamoja ya utalii ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 18 Oktoba 2016. 

Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top