Watumishi hewa wasepa na Sh5 bilioni za ‘benki’


 Kama ulidhani watumishi hewa walikuwa wanaisababishia hasara Serikali pekee hukuwa sahihi.


Athari za watumishi hao ambao hadi Septemba 14, mwaka huu walifikia 17,201 wamesababisha hasara kubwa serikalini katika malipo ya mishahara na stahiki nyingine na katika maeneo mengine.


Septemba mwaka huu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki alisema mjini Dodoma kuwa katika mchakato huo, wamegundua mikopo mingi imetolewa visivyo kwa watumishi wengi hewa.”


Akihutubia katika sherehe za Siku ya Wafanyakazi Duniani, Mei Mosi mwaka huu, Rais John Magufuli alisema watumishi waliokuwa wamebainika hadi wakati huo, walikuwa wakilipwa zaidi ya Sh11.63 bilioni kwa mwezi ikiwa ni mishahara bila kujumuisha stahiki nyingine za mwajiriwa wa umma.


Athari za jinamizi hilo la watumishi hewa serikalini limesambaa hadi katika sekta binafsi na moja ya taasisi zilizoathirika kwa kiwango kikubwa ni Bayport Financial Services, taasisi inayojihusisha na shughuli za mikopo na bima.


Hilo ndilo lililoikumba taasisi hiyo imebaini kuwa wateja wake 2,000 waliokopa zaidi ya Sh5 bilioni wamo kwenye kundi hilo la watumishi hewa.


Vijana wa mtaani wanapenda kutumia neno kusepa wakimaanisha kutoweka na hilo ndilo limeikumba Bayport baada ya watumishi hewa hao kutoweka.


Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bayport, John Mbaga alisema jana kuwa taasisi yake imeathirika kutokana na ukaguzi huo wa watumishi hewa unaoendelea kufanyika nchini.


“Siyo sisi tu, taasisi nyingi za fedha zimekumbwa na hili. Baadhi ya benki kubwa zimepoteza fedha nyingi zaidi yetu,” alisema Mbaga.


Licha ya kupoteza kiasi hicho cha fedha, wastani wa mikopo isiyolipikia katika taasisi hiyo umeongezeka kutoka asilimia tano mpaka saba, lakini aliwatoa wasiwasi wateja wake kwamba huduma zinaendelea kama kawaida.


Pamoja na hayo, Mbaga alipongeza juhudi za Serikali kufanya ukaguzi huo ambao umetoa picha halisi ya wateja wa kweli wa taasisi hiyo ambayo wiki hii inatimiza muongo mmoja tangu ianzishwe.


Ofisa Mkuu wa Operesheni wa Bayport, Ally Abdallah alisema taasisi hiyo inaendelea kujiimarisha ili kuwafikia Watanzania wengi zaidi na kuwakomboa kiuchumi kwa kuwapatia mikopo isiyohitaji dhamana kama zilivyo benki za biashara.


“Tunayo matawi 82 nchini kote. Tunatarajia kuyaongeza ili kuhudumia wateja wengi zaidi. Tunatoa mikopo ya viwanja pia na tungependa wengi wanufaike nayo,” alisema Abdallah.


Alibainisha kuwa hadi sasa Sh3.5 bilioni zimetolewa kwa ajili ya viwanja na tayari wateja 300 wamekabidhiwa hatia zao.


Akizungumzia soko la mikopo na huduma za fedha kwa ujumla, Mbaga alisema Watanzania wameanza kuelewa umuhimu wa mikopo na kutoshangazwa na riba inayotozwa na taasisi za fedha na benki mbalimbali nchini.


“Tunawataka wateja wetu wakope kwa sababu ya uwekezaji. Wasitumie mkopo kwa ajili ya sherehe au kitu kingine kama hicho,” alisema.




Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumatano October 12, 2016 bofya hapa

Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top