TCRA Yapiga Marufuku Uuzwaji wa Samsung Galaxy note 7 Hapa Nchini



MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imepiga marufuku uingizaji na usambazaji wa simu za mkononi za Smartphone Samsung
Galaxy note 7 kwa kuwa zina matatizo ya betri.


TCRA pia imewataka wananchi ambao tayari wanatumia simu hizo kuzizima na kuzirudisha haraka katika maduka walikozinunua.


Meneja Mawasiliano wa TCRA, Innocent Mungy, amewataka watanzania wajihadhari kuitumia simu hiyo kwa kuwa Kampuni ya Samsung yenyewe imeiondoa sokoni.


“Simu hiyo tayari Samsung wenyewe wamesema ina matatizo ya betri na mara mbili sasa imelipuka,” amesema Mungy.


Amewaomba watu wenye simu za aina hiyo kuzirudisha madukani haraka wabadilishiwe ama kurudishiwa fedha zao.


“Hata kama uliletewa zawadi kutoka nje ya nchi nawaomba warudishe huko kuepuka matatizo yanayoweza kujitokeza,” amesema Mungy.


Hivi karibuni simu aina hiyo iliyothibitishwa na kampuni hiyo kuwa ilikuwa salama, ilishika moto kwenye ndege nchini Marekani.


Simu hiyo inadaiwa kushika moto ikiwa mikononi mwa abiria aliyekuwa kwenye shirika la ndege la Southwest Airlines.

Shirika hilo liliwaondoa kwa dharura abiria waliokuwa kwenye ndege iliyokuwa imepangiwa kusafiri kutoka Louisville, Kentucky, hadi Baltimore, Maryland muda mfupi kabla ya kupaa.

Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top