RC Arusha atumbua maofisa 3 Ngorongoro



SAKATA la matumizi mabaya ya fedha za umma, limeendelea kuwatafuna watumishi wa umma baada ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo kuwasimamisha kazi watumishi watatu wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro na wengine wanne akiwemo aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, John Mgalula kurudishwa Arusha, kujibu malipo ya fedha zaidi ya Sh milioni 628 zilizolipwa kinyume cha utaratibu.

Waliosimamishwa kazi ni Mweka Hazina Evance Mwalukasa, Mwanasheria wa halmashauri hiyo, Sembele Siloma na Ofisa Uchaguzi wa jimbo hilo, Khadija Mkumbwa.

Wanaotakiwa kurudi Arusha na kujibu tuhuma zinazowakabili ni aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Ngorongoro, Mgalula, Ofisa Mipango Aloyce Chambi, Ofisa Elimu Shule za Msingi, Natangiapo Mollel na Mhandisi Benjamini Maziku.

Gambo alichukua uamuzi huo juzi baada ya kukamilika kwa taarifa ya kamati yake, aliyounda yenye wajumbe watano iliyochukua wiki mbili na aliisoma taarifa hiyo mara baada ya kuzungumza na watumishi wa halmashauri na watendaji wa kata kwenye Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro.

Alisema Mweka Hazina na Mwanasheria, walishindwa kumshauri vizuri mkurugenzi kuwa malipo ya Sh milioni 135 zilizokuwa zikilipwa nje ya mwongozo na Sh milioni 20 zilizotumika katika manunuzi kinyume cha utaratibu.

Alisema mwanasheria huyo kwa mara nyingine, aliruhusu kiholela bila ya kufuata Sheria ya Manunuzi na Ugavi kulipa zaidi ya Sh milioni 180 kwa malipo ya magari 18 katika kipindi cha uchaguzi. Mbali ya hilo, kamati hiyo ya uchunguzi ilibaini kuwa watumishi wa halmashauri hiyo, walijilipa posho zaidi ya Sh milioni 20 kinyume cha utaratibu.

Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top