Mechi ya watani wa jadi yamalizika kwa sare uwanja wa taifa, dondoo muhimu za mechi

Kichuya atuliza presha Simba
 




Shiza Ramadhani Kichuya ameifungia Simba bao la kusawazisha katika mechi ya watani wa jadi iliyomalizika kwa sare ya kufungana goli 1-1 uwanja wa taifa.

Yanga walitangulia kupata bao kupitia Amis Tambwe lililofungwa dakika ya 27 kipindi cha kwanza. Goli hilo lilizua tafrani kwa wachezaji wa Simba kumzonga mwamuzi wa mchezo huo Martin Saanya hali iliyopelekea kumuonesha kadi nyekundu nahodha wa Simba Jonas Mkude.



Mashabiki wa Simba walianzisha vurugu kwa kung’oa viti na kuvirusha uwanjani hali iliyopelekea polisi kutumia mabomu ya machozi kuleta utulivu ndani ya uwanja.



Kipindi cha kwanza kikamalizika Yanga wakiwa mbele kwa goli 1-0 huku Simba wakiwa pungufu kufuatia Mkude kuoneshwa kadi nyekundu.



Zikiwa zimesalia dakika tatu mchezo kumalizika, Simba walipata kona ambayo ilipigwa na Kichuya na kutinga moja kwa moja wavuni.

Dondoo muhimu
Mkude ni mchezaji wa pili wa Simba kuoneshwa kadi nyekundu katika mechi mbili za mwisho za Simba vs Yanga, Mechi ya iliyopita ya Simba vs Yanga Abdi Banda alioneshwa kadi nyekundu kipindi cha kwanza katika mchezo ambao Yanga walishinda 2-0.
Amis Tambwe amefunga magoli matatu katika mechi tatu mfululizo za mwisho za Simba vs Yanga. Alifunga goli moja katika kila mechi za msimu uliopita kabla ya kufunga kwenye mchezo wa leo.
Simba na Yanga zilikuwa zinakutana kwa mara ya 93 katika historia ya ligi kuu Tanzania bara, sare ya mchezo huo inafanya timu kutoka sare katika jumla ya mechi 33. Yanga inaongoza kwa kushinda mechi 35 ikiwa imefunga magoli 102 wakati Simba imepata ushindi katika mechi 25 na kufunga magoli 89.
Simba imeendeleza rekodi ya kutopoteza mchezo msimu huu, imecheza mechi saba na kufanikiwa kushinda mechi tano na kutoka sare mara mbili. Yanga imecheza mechi sita, imeshinda mechi tatu, imetoka sare mara mbili na kupoteza mchezo mmoja.
Simba bado inaongoza ligi ikiwa na pointi 17 ikifuatiwa na Stand United ambayo inapointi 12 huku Yanga wakishika nafasi ya tatu kwa pointi zao 11.
Juma Mahadhi, Vicent Andrew ‘Dante’ ni wachezaji wa Yanga ambao wamecheza kwa mara ya kwanza Kariakoo derby wakati kwa upande wa Simba walikuwa ni Janvier Bokungu, Method Mwanjale, Shiza Kichuya, Mzamiru Yassin, Laudit Mavugo, Fredrick Blagnon na Mohamed Ibrahim.
Kichuya amefunga magoli matano kati ya 13 ambayo tayari Simba imefunga hadi sasa huku Amis Tambwe akiwa ndio mfungaji mwenye magoli mengi hadi sasa, amefunga magoli manne kwenye mechi sita alizoichezea Yanga.
Simba ndiyo inaongoza kwa kufunga magoli mengi kwenye ligi hadi sasa ikiwa imeshazamisha kambani jumla ya magoli 13 wakati Yanga wao wamefunga magoli 9 huku wakiruhusu kufungwa magoli mawili.
 
 
 


 

Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top