Kiwango kimerudi- Pluijm


 

KOCHA Mkuu wa Yanga, Hans van Pluijm amesema kikosi chake kimerudi katika kiwango chake na sasa ni mwendo wa ushindi katika mechi zake zilizobaki.

Yanga ilipata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Mtibwa Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania bara uliochezwa juzi kwenye Uwanja wa Uhuru.

Mabao ya Yanga katika mechi hiyo yalifungwa na Obrey Chirwa, Simon Msuva na Donald Ngoma na la Mtibwa likifungwa na Haruna Chanongo. Huo ni ushindi wa kwanza kwa Yanga baada ya kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Stand United na kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Simba katika mechi zilizopita.

Akizungumza baada ya mechi hiyo, Pluijm alisema kiwango walichoonesha wachezaji wake kama wataendelea nacho ni wazi kuwa wataikaribia Simba inayoongoza kileleni.

“Ushindi huu mnono unaonesha kuwa tumerudi ni lazima tuendelee kujiandaa asilimia 100 kwa kila mchezo wetu kuendeleza ushindi, lengo letu ni kuikaribia Simba kileleni na kuwa rahisi kutetea taji letu,” alisema.

Alisema kikosi chake kilicheza vizuri na kwa ushirikiano uliowezesha kutumia vyema nafasi walizopata katika kufunga.

Kuhusu Chirwa kufunga kwa mara ya kwanza tangu ajiunge na timu hiyo msimu huu, Pluijm alisema siri ya mafanikio ni kwa sababu alimuandaa kisaikolojia na kumhimiza kucheza kwa kujiamini. “Nilimuandaa Chirwa na kumhimiza kujiamini anapokuwa uwanjani na hilo limefanikiwa kwake,” alisema.

Ushindi wa Yanga umeisogeza nafasi moja kutoka nafasi ya tano hadi nne ikiishusha Mtibwa Sugar iliyokuwa ikishika nafasi ya tatu.

Yanga sasa imefikisha pointi 14 katika michezo saba iliyocheza, nyuma ya Kagera Sugar yenye pointi 15 katika michezo tisa iliyocheza, Stand United ikishika nafasi ya pili kwa pointi 19 katika michezo tisa na Simba inayoongoza kileleni kwa pointi 20 katika michezo minane iliyocheza.

Mchezo ujao Yanga inatarajiwa kucheza na Azam FC keshokutwa, mchezo ambao unatarajiwa kuwa mgumu kwani Azam imekuwa haifanyi vizuri kwenye mechi zake na imetoka kupoteza juzi ya Stand United, hivyo itataka kushinda.
 

Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top