Bossou afunga bao la kwanza VPL, Yanga ikizisambaratisha mbao za Mwanza

Yanga SC leo ni kama wamewajibu wapinzani wao Simba baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Mbao FC kutoka jijini Mwanza, mchezo uliofanyika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam. Ikumbukwe jana watani wao wa jadi walipata ushindi kama huo dhidi ya Mwadui FC huko mkoani Shinyanga.

Kipindi cha kwanza kilianza kwa kila upande kuwa mgumu huku wakicheza kwa kuviziana, hali iliyopelekea mchezo kuwa mgumu kwa pande zote.



Yanga ambao leo kwa mara ya kwanza walikuwa chini ya kocha Hans Van der Pluijm aliyerudi baada ya kubatilisha maamuzi yake ya kujiuzulu, safu yao ya ushambuliaji ilianza chini ya Amisi Tambwe na Obrey Chirwa.

Mpaka kipindi cha kwanza kinamalizika, milango ya timu zote ilikuwa migumu baada ya timu zote kutoshana nguvu.

Kipindi cha pili Yanga waliingia kwa kasi kubwa wakitafuta bao la mapema ili kujiweka katika mazingira mazuri, hasa baada ya watani wao Simba kushinda ugenini dhidi ya Mwadui FC.

Dakika ya 50 Yanga walipata bao la kwanza kupitia kwa beki wake Mtogo Vincent Bossou baada ya kuunganisha mpira mzuri wa adhabu ndogo uliopigwa na Haruna Niyonzima aliyekuwa nahodha katika mchezo wa huo.

Yanga waliendelea kulisakama lango la Mbao FC na kufanikiwa kupata bao la pili dakika ya 57 baada ya makosa ya kipa wa Mbao Emmanuel Mseja kushindwa kuudaka mpira uliorushwa na Mbuyu Twite.

Dakika ya 65 Yanga walifanya mabadiliko kwa beki wao wa kulia Hassan Kessy kwenda benchi na Thabani Kamusoko kuchukua nafasi hiyo.

Amissi Tambwe ambaye kwenye mchezo wa leo alifichwa kwa muda fulani wa mchezo, aliifungia Yanga bao la tatu baada ya kupata pasi nzuri kutoka kwa Simon Msuva dakika ya 76.

Kipa wa Yanga Deogratius Munishi alipewa kadi ya njano dakika ya 88 baada ya kuchelewesha muda kwa makusudi.

Matokeo ya leo yanaibakisha Yanga katika nafasi ya pili wakiwa na alama 27 nyuma ya vinara mahasimu wao Simba wenye alama 32.
 

Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top