Bakhresa amkuna Dk Magufuli, ampa eka 10,000


Rais John Magufuli 

Rais Magufuli amesema alikuwa akikataa mialiko mingi kuhudhuria shughuli za wafanyabiashara, lakini ameamua kuanzia na Bakhresa kwa sababu maalumu.


Akizungumza kwenye uzinduzi wa kiwanda cha Bakhresa Products Limited kinachomilikiwa na mfanyabiashara Abubakar Bakhresa, amesema sababu hiyo maalumu inatokana na ukweli kuwa anamiliki viwanda kama ambavyo sera zake za kutaka Tanzania iwe nchi ya viwanda zinavyotaka.


Pia amesema viwanda vinavyomilikiwa na Bakhresa vinazalisha ajira kwa wapigakura wake na kwamba bilionea huyo ni mzawa.


Amesema Bakhresa ni mwaminifu na analipa kodi, akiweka bayana kuwa kwa mwaka jana pekee alilipa Sh54 bilioni.


Ili aendelee kuzalisha ajira zaidi, Rais amemtaka Bakhresa kuanzisha kiwanda cha sukari ambacho pia kitasaidia kupunguza uhaba wa bidhaa hiyo, ombi ambalo mfanyabiashara huyo alilikubali kwa kupiga makofi na hapo hapo akaahidiwa neema nyingine.


“Nitakupa eka 10,000 za ardhi kwa ajili ya kulima miwa na kuanzisha kiwanda cha sukari, tena kitakuwa karibu na Dar es Salaam,” amesema Rais.


Rais Magufuli amempongeza Bakhresa kwa kuwa mfano mzuri kwa wafanyabiashara wengine kwa sababu ametoa ajira kwa watu wengi na analipa kodi serikalini.


Rais Magufuli alisema ametoa ardhi hiyo ili Bakhresa alime miwa na kuzalisha sukari badala ya kuagiza nje.


“Kama kuna mtu yeyote anataka kuwekeza na anapata changamoto zozote anione, mimi ndiye mwenye dhamana. Nitakwenda popote kufuatilia ilimradi mtu huyo aanzishe uwekezaji wake,” amesema Rais wakati wa uzinduzi wa kiwanda hicho cha kusindika matunda kilichopo Mkuranga mkoani Pwani.


Mkurugenzi wa makampuni ya SSB, Bakhresa amesema waliomba kuunganishiwa umeme wa megawati 10, lakini hadi sasa hawajaunganishwa na hivyo kusababisha gharama za uzalishaji kuwa juu kwa sababu wanatumia jenereta.


Mbali na suala la umeme, Abubakar amesema changamoto nyingine ni wingi wa taasisi za udhibiti wa bidhaa ambao unasababisha urasimu katika utoaji wa huduma na ni vyema kuwa na taasisi moja ambayo itashughulikia udhibiti wa bidhaa ili kuondoa urasimu huo. 






Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top