Amis Tambwe atupia magoli haya VPL



Na Baraka Mbolembole

MSHAMBULIZI wa klabu ya Yanga SC, Mrundi, Amis Tambwe alifunga goli lake la tatu msimu katika ushindi wa Mwadui FC 0-2 Yanga.

Tambwe ameshatwaa mara mbili tuzo ya ufungaji bora wa ligi kuu Tanzania Bara katika misimu mitatu iliyopita alianza kufungua akaunti yake ya magoli wiki iliyopita alipofunga mara mbili katika ushindi wa Yanga 3-0 Majimaji FC hadi sasa amefikisha jumla ya magoli 58 katika ligi kuu pekee.

Alifunga jumla ya magoli 19 katika msimu wake wa kwanza ambao alishinda tuzo ya ufungaji bora akiwa na kikosi cha Simba SC msimu wa 2013/14.

Msimu wake wa pili alianza kwa kufunga katika sare ya Simba 2-2 Coastal Union mwezi Septemba 2014, lakini hadi anajiunga na Yanga kama mchezaji huru mwishoni mwa mwezi Desemba 2014 mshambulizi huyo hakuwa amefunga goli lolote.

Mambo yalianza kumnyookea tena kwani alifanikiwa kufunga jumla ya magoli 14 akiwa Yanga na kufikisha magoli 15 kufikia mwisho wa msimu wa 2014/15.

Msimu wake wa pili alimaliza katika nafasi ya pili ya ufungaji nyuma ya mchezaji mwenzake wa Yanga, Saimon Msuva ambaye alishinda tuzo hiyo baada ya kufunga magoli 17. Msimu uliopita (2015/16,) Tambwe alishinda kwa mara ya pili tuzo ya ufungaji bora baada ya kufunga jumla ya magoli 21.

Mrundi huyo ni hatari kwa mipira ya kichwa na amekuwa na shabaha ‘isiyokwisha’ anapopiga shuti golini. Baada ya kusainiwa kwa Mzambia, Obrey Chirwa ilidhaniwa labda utakuwa mwisho wa kutamba kwa Tambwe lakini tayari ameonesha bado ana njaa ile ile tu.

Huyu ni mshambuliaji-mfungaji bora zaidi katika ligi ya Tanzania Bara katika kipindi cha miaka 16 iliyopita. Ni mfungaji ambaye si rahisi kupatikana, ana mwendelezo bora katika ufungaji msimu hadi msimu. Amis Tambwe anasimama pekee na magoli yake 58 VPL.
 

Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top