Waliomzushia kifo Ndesamburo watiwa mbaroni

Polisi wamewatia mbaroni watu watano wanaodaiwa kusambaza taarifa kwenye mitandao ya jamii kuwa Mbunge wa zamani wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo amefariki dunia.


Miongoni mwa waliokamatwa na kuhojiwa na polisi na simu zao kushikiliwa kwa uchunguzi, ni wanachama wa Chadema na maofisa wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia).


Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Wilbroad Mutafungwa jana alisema kuwa, uzushi huo kuwa Ndesamburo amefariki dunia, ulisambazwa zaidi kupitia makundi ya WhatsApp.


“Tarehe 29/7/2016 mzee Ndesamburo alifika polisi na kutoa taarifa kuwa katika mitandao ya jamii kuna taarifa na picha yake, inasambazwa kwa kasi kuwa amefariki dunia,” alisema Mutafungwa na kuongeza: 


“Picha hiyo ilikuwa na maneno RIP (Rest in Peace), wakimaanisha apumzike kwa amani. Tulifungua jalada na kitengo chetu cha Cyber Crime (makosa ya kimtandao) kiliingia kazini.”


Alisema watu mbalimbali walihojiwa na polisi wanaendelea kazi hiyo pia watu watano walikiri kupokea ujumbe huo na kuusambaza.


Kamanda Mutafungwa alisema wanaendelea na uchunguzi wa kisayansi kumpata mtu aliyeanzisha ujumbe huo, ambao ulisababisha usumbufu kwa Ndesamburo na familia yake.


Wanaoendelea kuhojiwa ni Ofisa Usalama wa Kampuni ya Kilimanjaro Airport Development (Kadco) na msimamizi wa waongoza ndege wa Fast Jet Uwanja wa Kia.


Wengine ni wanachama watatu wa Chadema, ambacho Ndesamburo ni Mwenyekiti wake wa Mkoa Kilimanjaro. Katibu wa Chadema Mkoa Kilimanjaro, Basil Lema alithibitisha kuhojiwa kwa wanachama wake na kwamba, anaamini mwanzilishi wa taarifa hiyo ya uzushi hajakamatwa.


Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top