TUNDU LISSU: Mpambanaji aliyeuanza uanaharakati utotoni, Soma makala ya mahojiano maalumu na Tundu Lisu

Mwandishi Godfrey Dilunga, alifanya mahojiano kuhusu masuala mbalimbali na Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA) ambaye pia ni mwanaharakati wa haki za binadamu, Tundu Lissu, jijini Dar es Salaam. Yafuatayo ndiyo yaliyojiri kwenye
mahojiano hayo.

Raia Mwema: Tuanze na historia yako kwa muhtasari.

Lissu: Niliishi maisha ya furaha sana ya utoto. Tangu nikiwa shule ya msingi ni kama vile nilikuwa mwanaharakati. Unajua shuleni kuna shughuli nyingi sana kama kuchota maji kwa ajili ya walimu, kulima mashamba ya walimu na kupanda. Nilikuwa nikiona haya mambo hayako sawa, lakini pia kuna suala la kuwahi shuleni.

Sikumbuki kwa miaka saba ya shule ya msingi, kama kuna siku nimewahi zile namba. Siku zote nilikuwa mchelewaji na nimechapwa kweli.

Raia Mwema: Ni ukaidi wa makusudi?

Lissu: Siwezi kusema ni makusudi, lakini tatizo ni kuamka alfajiri saa 11 ili saa 12 niwe shuleni. Kwa hilo nilikuwa rebel (muasi). Pia sikumbuki mahali ambako sikuwahi kubishana na walimu iwe primary school, secondary school, iwe chuo kikuu, siku zote imekuwa hivyo.

Lakini vile vile nilizaliwa katika familia ambayo mijadala ya kisiasa ilikuwa sehemu yetu. Baba yangu alisoma hadi darasa la sita, mama yangu hakusoma kabisa.

Kila jioni tunasikiliza kwanza taarifa ya habari na idhaa ya Kiswahili ya Ujerumani; baada ya hapo ni mjadala mpaka saa tano au sita, mjadala wa kisiasa kuhusu mwenendo wa mambo duniani. Nilikuwa mtoto mdogo sana, lakini nilikuwa na ufahamu.

Nafikiri nilikuwa miaka sita au saba hivi.

Wakati nikiwa darasa la kwanza (1976), nilikuwa nafahamu karibu viongozi wote duniani na miji mikuu mashuhuri.

Raia Mwema: Kutokana na ufahamu huo, ni viongozi gani hapa nchini walikuvutia wakati huo?

Lissu: Ni swali gumu kidogo. Si rahisi sana kusema nilivutiwa na Mwalimu Nyerere. Ukweli ni kwamba hapana, alikuwa sehemu ya mazungumzo ya kisiasa nchini. Siwezi nikasema nilivutiwa sana na Mwalimu.

Raia Mwema: Unaposikia jina la Julius Nyerere kwa sasa, unakumbuka nini?

Lissu: Ni hotuba za Mwalimu Nyerere kuhusu vita dhidi ya Uganda. Wakati huo nikiwa darasa la tatu mwaka 1978, nchi iko vitani tulichangishwa (familia) ng’ombe.

Baba yangu alitoa ng’ombe watatu kama sikosei ili kusaidia vita mpakani. Shuleni tuliimbishwa sana nyimbo kwamba Iddi Amini ni nyoka; ingawa baadaye nimekuja kugundua kwamba inawezekana kuna vitu vingine vingi hatukuambiwa kuhusu mgogoro wetu na Uganda.

Nakumbuka pia wakati huo tukiwa wadogo tulichimbishwa mahandaki. Nilikuwa na miaka 10, nilishangaa tunachimba (mahandaki) nje ya nyumba yetu halafu siyo marefu sana.

Lakini kuna kitu kingine kilichotafsiri mtazamo wangu kuhusu serikali ambao sio chanya sana. Nilipokuwa miaka kama sita hivi, nyumba yetu na wanavijiji wengine zilibomolewa halafu tukaachwa tu. Kina mama wanalia, kila mtu analia; halafu hawa watu wakavunja nyumba wakaondoka.

Raia Mwema: Hao wavunjaji walitumwa na nani?

Lissu: Unajua ukiwa na miaka 10 huulizi sana. Ni tukio ambalo haliwezi kuondoka katika kumbukumbu zangu kwamba; serikali inaweza kufanya vitu visivyo na akili (mantiki).

Sisi na wanakijiji wengine tumejenga nyumba, ingawa pengine hazikuwa nzuri sana wao (serikali) wametubomolea kwa jina la Operesheni Vijiji.

Baba yangu alikuwa Mwenyekiti wa Kijiji wakati huo, baadaye (watendaji wa serikali) wakaja na kamba za katani na wataalamu ili kupima namna ya kujenga nyumba za kisasa, wanaita maendeleo.

Kwa hiyo, wazee wanatembea na kamba ya katani wanapima namna ya kujenga nyumba za kisasa , zijengwe kwa mstari ulionyooka. Lakini hatimaye hawakutujengea wala kutusaidia chochote.

Hali hiyo ilinifanya niamini kwamba pengine serikali haina watu wenye akili sana kama nilivyokuwa nikifirikia mwanzoni.

Raia Mwema: Ukiwa katika umri wa utoto, unakumbuka nini enzi za nchi kufunga mikanda na baa la njaa lililowahi kutokea?

Lissu: Kuna njaa ya mwaka 1974 serikali ilileta chakula kudhibiti njaa hiyo, nakumbuka kuna kitu (chakula) kinaitwa burga ilikuwa sijaanza shule baadaye tukaletewa ugali wa muhogo. Sisi kwetu tunakula muhogo wa kuchemsha. Ilikuwa hali tofauti.

Raia Mwema: Tueleze safari yako kielimu, ilikuwaje…ngumu au nyepesi tu.

Lissu: Wakati wa Operesheni Vijiji ilitokea mvutano wa kuhama. Baba yangu pamoja na wazee wengine walisafiri kutoka kijijini Singida wakaja Dar es Salaam kulalamika.

Walilalamika kwamba tunatakiwa tuhame kwenye kijiji chenye mashamba makubwa. Wakaja kupiga kelele na serikali wakati huo iliwasilikiza.

Lakini ikaibuliwa hoja kwamba; tuhame (kijiji) kwa sababu hakuna shule. Wakati ule, hoja ya vijiji vya ujamaa ililazimisha kuwapo huduma za kijamii.

Sasa ili kukabili hoja hiyo na tusiweze kuhamishwa, kuna mzee mmoja alijenga nyumba yake mpya, akasema sitahamia ili iwe shule ya watoto. Kwa hiyo, tukaanza shule lakini shida walimu.

Mmoja wa wadogo zake baba yangu wakati huo alikuwa amemaliza darasa la saba, hana pa kwenda, wakasema atakuwa mwalimu. Kuna mama mwingine mjanja mjanja kijijini, naye wakamwambia atakuwa mwalimu.

Kwa hiyo, tukaanza darasa la kwanza Aprili 5, 1976. Shule za miaka ile zilikuwa zinaanza Januari, lakini ya kwetu tulianza Aprili, kwenye nyumba ya tembe sio ya bati, na walimu wasio na mafunzo yoyote.

Hatukuwa na vitabu, swali likawa tutaandikia nini? Wazee wakachanga hela wakamtuma mtu Dar es Salaam aende kumtafuta mtu anaitwa Abdallah Nungu, amueleze tatizo la vitabu shuleni.

Kwa hiyo, tukamsuburi kwa wiki mbili huyu bwana alete vitabu. Akarudi na boski kubwa la vitabu na vile vibao vya kuandikia, ingawa awali tulikuwa tukiandika chini (ardhini). Hivyo ndivyo tulivyoanza shule wengine.

Lakini hilo lilikuwa darasa la kwanza kwenye hiyo nyumba ya mzee. Tatizo likajitokeza ni darasa la pili litakaa wapi, kwa sababu ilibidi darasa la kwanza wengine waanze.

Nyumbani kwetu baba alijenga nyumba jirani na mdogo wake, lakini huyo mdogo wake hakuwa akiishi hapo kijijini alikuwa Moshi, nyumba yake haikuwa ikikaliwa.

Mzee akasema darasa la pili hilo hapo (nyumba ya mdogo wake). Kwa hiyo, darasa la pili tukahamia kwetu (nyumbani). Natoka mlango huu, naingia mlango wa pili niko darasani. Baada ya hapo, tukaanza ujenzi wa shule ambayo ikaitwa Shule ya Msingi Mahambe.

Raia Mwema: Serikali haikutoa mchango wowote katika hatua za awali za ujenzi?

Lissu: Hatukusaidiwa na serikali katika ujenzi. Ilikuwa asubuhi tunakwenda shule, saa nane tunaporudi (shule) tunabeba vibuyu na ndoo za maji pamoja na mama zetu kupeleka eneo la kufyatulia matofali; shughuli iliyokuwa ikifanywa na baba zetu.

Mwaka mzima tumefyatua matofali na baadaye kuanza ujenzi. Kule kwetu kuna Wakatoliki wengi, pale eneo la ujenzi (wa shule) kulikuwa na padre anapita kwenda kusalisha kijiji cha jirani kila Jumatano. Kila akipita anakuta ujenzi unaendelea na watoto wanasaidia.

Huyo padre anaitwa Charles ni mu-Irish, kila siku anapita pale anakuta watoto na wazazi wanafanya kazi, nadhani alikuwa akijiuliza kuna nini?

Siku hiyo akasimama. Alikuwa anatumia pikipiki kubwa….sijui ni kubwa (pikipiki) kweli au mimi ndiye nilikuwa mtoto na kuiona kubwa.

Akauliza, akaambiwa tunajenga shule. Akauliza serikali iko wapi? Akaahidi tukishamaliza ujenzi, ataleta mafundi kukamilisha kwa kuweka bati, ikaitwa Shule ya Wazazi.

Darasa la tatu tukaingia sasa kwenye darasa zuri na bora. Kuanzia hapo, kila mwaka nilipokaa pale shule ya msingi tulikuwa tunajenga darasa moja moja, hadi tulipomaliza mwaka 1979 tunaingia darasa la tano ndiyo kwa mara ya kwanza ikaitwa Shule ya Msingi Mahambe, na tutakaletewa mwalimu wa serikali.

Kwa hiyo, kati ya vyuo vikuu vyangu, chuo kikuu cha kwanza ni hicho….miaka minne ya kufundishwa na walimu wasio na mafunzo yoyote.

Siku hizi nikipita nikiwaambia watu shule niliyosomea na walimu walionifundisha, hawaamini. Tulifundishwa na wanakijiji kabisa wasio na mafunzo! Serikali ilipoanzisha mpango wa UPE wale walimu walijiendeleza, wakaenda vyuoni na wapo ambao wamekuwa waalimu wanataaluma.

Raia Mwema: Hayo ni ya shule ya msingi, tueleze ya sekondari, unakumbuka nini hasa?

Lissu: Cha kwanza nimetoka nje ya kwetu (Singida), nimeenda kusomea Ilboru Sekondari, Arusha. Pale (Ilboru) maisha yalikuwa mazuri na nilikuwa mdogo kuliko wengine wote (wanafunzi).

Sikuwahi kuwa kiongozi shuleni, na sikutaka uongozi. Viongozi wakati ule tuliwaita manyoka kwa sababu wanapeleka habari kwa walimu.

Lakini baadaye nilipoingia kidato cha tano na sita, Galanos Sekondari (Tanga), nilipewa uenyekiti wa Kamati ya Taaluma, lakini baada ya miezi sita hivi nikagombana vibaya sana na mwalimu wa taaluma, ikabidi nivuliwe madaraka.

Raia Mwema: Mlitofautiana katika jambo gani na mwalimu wa taaluma?

Lissu: Ni msimamo tu. Ilitokea kwamba mwaka 1988 niko kidato cha sita, sasa kidato cha nne na cha sita kila mwaka hufanya graduation (mahafali). Wakati huo, hasa Galanos na shule nyingi za sekondari, disko hazikuwa nyingi (mara kwa mara) kama sasa.

Kipindi cha kwenda kucheza disko ilikuwa wakati wa graduation. Sasa walimu wakaamua watoto wa kidato cha nne hawatakwenda kucheza disko. Mimi niko kidato cha sita, sasa tulipanga kwenda disko Korogwe Girls. Wakaamua (walimu) kidato cha nne hawatakwenda Korogwe Girls, badala yake waletewe taarabu.

Sikukubaliana, nikaandika makala inahoji uamuzi huo. Title yake naikumbuka hadi leo, inasema; “taarab for who’s benefit?” – taarabu kwa faida ya nani?

Halafu tukafanya mpango (wanafunzi) ikabandikwa kwenye mbao za matangazo shuleni, sikuandika jina langu halisi. Walimu wakauliza, wakapeleleza nani anaweza kuandika vitu kama hivi?….wakanikamata.

Nikatuhumiwa kuleta uchochezi, nikasimamishwa shule, baadaye walinirudisha. Lakini kwa ujumla miaka ya sekondari ilikuwa mizuri, hapakuwa na njaa kama wakati huu.

Raia Mwema: Baada ya kuhitimu kidato cha sita, nini kilichofuatia?

Lissu: Nikaenda JKT Mbeya, kwanza nilipelekwa Mafinga, lakini sikukaa tukapelekwa Mbeya operesheni yangu inaitwa; Operesheni ya Programu ya Chama, mwaka 1989.

Raia Mwema: Unakumbuka nini kuhusu enzi za JKT?

Lissu: Ninachokumbuka mjadala wa vyama vingi ulikuwa umeiva na CCM hawataki vyama vingi. Ilikuwa mwaka 1989/1990, kwa Katiba ya CCM wakati huo, kulikuwa kuna mkoa unaitwa Mkoa wa Majeshi, ulikuwa mkoa sawa na mingine katika chama.

Kwa hiyo, wakatuma wajumbe wao wa Mkoa wa Majeshi kutembelea kambi zote za jeshi na JKT Tanzania nzima, kueleza msimamo wa CCM.

Waliokuja Itende JKT kwetu nawakumbuka ni Omari Mahita wakati huo ni Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, Kanali Andrew Shija na mtu mwingine simkumbuki.

Nawakumbuka Kanali Shija na Omari Mahita kwa sababu walijenga hoja kwamba haya mageuzi (vyama vingi) hayatuhusu kwa hiyo tusishabikie yasiyotuhusu; eti yanayowahusu Wazungu, Ulaya Mashariki na kwingine.

Nakumbuka nilipambana vibaya sana na Omari Mahita kwenye huo mkutano. Nilisimama kuuliza maswali nikitambua kuwa kabla hawajaja, Mwalimu Nyerere alihutubia mkutano wa Baraza Kuu la Vijana wa CCM, Mwanza na akasema wanaodhani mageuzi ya Ulaya Mashariki hayatuhusu, ni wajinga.

Kwa hiyo, nikamuuliza RPC Omari Mahita nikamwambia kwamba Mwalimu Nyerere alisema wanaofikiri mageuzi ya Ulaya Mashariki hayatuhusu ni wajinga, na wewe umekuja na timu yako unatuambia haya mambo ni ya Wazungu hayatuhusu.

Sasa mjinga ni Mwalimu Nyerere aliyesema yanatuhusu au nyie ambao mnatuambia kwamba hayatuhusu?

Raia Mwema: Bila shaka ulitumbukia katika uhasama wa ghafla na meza kuu. Hali ilikuwaje?

Lissu: Omari Mahita ni mweupe sana, basi, ghafla akabadilika rangi akawa mwekundu. Ikawa makamanda kadhaa wakasimama tayari kumshughulikia huyu serviceman…maana nilishapita ukuruta. Wakasimama kutaka kumshughulikia anayetukana maofisa wa jeshi.

Lakini kanali Shija (marehemu sasa) akasimama akanitetea. Akasema; hoja ya serviceman ni sahihi kabisa, Mwalimu ndivyo alivyosema. Kwa hiyo, hatuwezi….kusema hayatuhusu. Maana yake tayari nilianza kusakamwa pale… akasema ni kweli hatuwezi kukwepa haya mawimbi na upepo. Shija akapiga siasa, na hatimaye akaniepushia kibano.

Raia Mwema: Kwa hiyo makamanda wenyewe kwa wenyewe walitofautiana mbele yenu?

Lissu: Walitofautiana na baada ya hapo, hakuna ofisa wa JKT aliyenigusa tena. Wengi baada ya hapo wakaamini mimi ni usalama wa taifa.

Maisha yakawa mazuri. Hakuna aliyenigusa kwa sababu kama nimezungumza vile na kanali wa jeshi, kwa sababu mkuu wa kambi mwenyewe hakuwa kanali, alikuwa luteni kanali, sasa mimi nimetetewa na Kanali Shija. Kwa hiyo nilikuwa nakula shushi (mambo mteremko).

Baada ya hapo nikaenda Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Miaka ile ulikuwa huendi chuo kikuu kama si mwanachama wa CCM na sehemu ya mafunzo unayopata JKT ni pamoja na itikadi ya CCM na mnapomaliza mafunzo mnakabidhiwa pia kadi za chama. Kwa hiyo, nilikuwa mwanachama wa CCM na hiyo ni muhimu watu wakafahamu.

Lakini nilikuwa mwanachama kwa sababu tu nilitaka kusoma. Ndivyo maisha yalivyokuwa na baada ya hapo. Nilipoingia chuoni kadi haikuwa na kazi sana kwangu. Siku ya kwanza chuo kikuu hadi naondoka, mijadala yote nilikuwa mstari wa mbele kabisa pamoja na kwamba sikuwahi kuwa kiongozi.

Raia Mwema: Katika mijadala yenu chuoni hasa ile mikubwa, hoja gani unakumbuka zilitikisa uongozi au hata nchi?

Lissu: Wakati huo, dunia na nchi ilikuwa ikibadilika, hatukuwa tayari tena kutawaliwa na mfumo wa chama kimoja, eti usipokuwa na kadi ya chama huendi chuo. Nikiwa mwanafunzi, uchangiaji wa gharama za shule ulianza wakati huo.

Nilikaa mwaka mzima nyumbani kabla ya kuingia chuo kikuu kwa sababu mwaka 1989 wanafunzi wa UDSM waligoma, chuo kikafungwa.

Pamoja na kwamba sikuwa sehemu ya huo mgomo wakati huo nilikuwa JKT, lakini madhara ya mgomo yalinigusa kwa kukaa nyumbani mwaka mzima. Nilipojiunga chuo mwaka 1991, tayari vuguvugu lilikuwa kubwa sana. Na upinzani dhidi ya uchangiaji gharama za elimu ulikuwa mkubwa sana.

Raia Mwema: Mliguswa vipi na tukio la kumdhalilisha Rais Mwinyi wakati ule chuoni UDSM?

Lissu: Chuo kilifungwa kutokana na tatizo hilo mwaka 1989. Ni tukio lililotugharimu ambao ndiyo tulitaraji kwenda kuanza masomo. Tulikaa nyumbani mwaka mzima.

Raia Mwema: Katika changamoto za mageuzi chuoni, baadaye ulijiunga na chama gani baada ya mfumo wa vyama vingi kuruhusiwa?

Lissu: Kama nilivyosema, nimezaliwa rebel , na hivyo haikuwa ajabu hata kidogo mimi kujiunga na chama cha upinzani ambacho kilivutia wasomi – NCCR-Mageuzi. Ilikuwa ni hatua inayotegemewa.

Nisingeweza kuwa CCM au CHADEMA kwa sababu kilikuwa chama kisichokuwa na msimamo mkali….hawa watu ni waoga, wanaogopa kuweka msimamo mkali. Ni kama chama cha kibepari hivi na mimi kimsimamo nimekuwa Mjamaa wa mrengo wa kushoto kabisa.

Raia Mwema: Uchaguzi wa kwanza baada kuruhusiwa vyama vingi mwaka 1992 ulifanyika 1995. Ulishiriki vipi uchaguzi huo?

Lissu: Ingawa jimboni kwetu (Singida Kusini wakati huo) mwanzo hapakuwa na uchaguzi wa vyama vingi, lakini ilikuwa sehemu ya changamoto kisiasa, hata wabunge waliokuwa wakichaguliwa walidumu kwa muhula mmoja tu.

Sasa ghafla tukawa na demokrasia pana zaidi – vyama vingi, lakini kwenye uchaguzi huo (1995) ikaelekea CCM itapita bila kupingwa. Kwa hiyo nikajitokeza kugombea ubunge jimbo la Singida Kusini.

Lakini wakati naanza mchakato wa kuwa mgombea, nikapata scholarship ya Serikali ya Uingereza kwenda kusoma Master’s (Uzamili). Nikaenda shule kuripoti, nikawaambia narudi nyumbani kujaribu ubunge, nikishindwa nitarudi.

Nikatoka Uingereza kuja kugombea ubunge mwaka 1995, nikiwa na miaka 27. Nikarudi shule baada ya kushindwa. Safari yangu ya kisiasa ilianza kujitokeza kipindi hicho.

Nikamaliza shule yangu mwaka 1997, nikaoa na nikahamia Dar es Salaam (kutoka Arusha alikokuwa akifanya kazi kama mwanasheria ofisi binafsi).

Raia Mwema: Katika harakati zako, tukio gani kubwa unakumbuka lilikutia msukosuko au kuibua katika jamii?

Lissu: Tukio la kwanza kubwa ilikuwa ni mradi wa ufugaji kamba delta ya Rufiji. Mradi wa Mzungu mmoja wa Ireland anaitwa Reginald Nolan. Alipewa na Serikali ya Mkapa hekta 20,000 ili atengeneze mabwawa ya kufuga kamba kwenye delta ya Rufiji katika maeneo ambayo yana vijiji karibu vinane, watu walima na kuishi, kuna msitu ya mikoko pale. Yote ile Reginald Nolan akapewa ili atengeneze mabwawa. Sisi kama watetezi wa mazingira kupitia Chama Cha Wanasheria wa Mazingira – LEAT, tulishikia sana bango mradi wa Rufiji.

Tulifanya kazi kubwa. Niliratibu kampeni ya kimataifa kwa kila njia, ikiwamo mitandao ya kimataifa ya wanaharakati kuupinga mradi huo.

Hatimaye, Benki ya Vitega Uchumi ya Ulaya (European Investment Bank) iliyokuwa itoe mkopo kwa Nolan ambao ungedhaminiwa na Serikali ya Tanzania, wakasema hawatatoa mkopo na kwa hiyo, mradi mzima ukasambaratika.

Niliwahi kushiriki mdahalo kwenye kituo cha televisheni nchini kuhusu mradi huo wa kamba, nikiwa mimi, mmiliki wa mradi na mwandishi wa habari wa siku nyingi, James Mpinga. Kwa mara ya kwanza ndipo nilipoanza kuonekana kwenye televisheni katika kipindi cha Hamza Kasongo Hour, Oktoba 1998.

Tuliwasambaratisha kila mahali. Tukapata nyaraka za Baraza la Mawaziri zilizosema mradi ni wa hovyo, lakini umepitishwa kinyemela.

Raia Mwema: Katika mchakato mzima wa harakati hizo, uliwahi kukumbwa na vitisho vya aina fulani?

Lissu: Vitisho vingi. Unaweza kufika ofisini ukakuta bahasha yenye ujumbe wa vitisho imepenyezwa chini ya mlango.

Baada ya hapo Machi, mwaka 1999, kuna kampuni moja wenye ginnery (kinu cha kuchambua pamba). Ni kampuni ya ki-Swisi. Wakaja ofisini kwetu (LEAT) wakaomba tuwafanyie utafiti juu ya madhara wanayoweza kupata kutokana na mgodi uliokuwa ukijengwa Geita. Walitaka kubaini kama shughuli za mgodi zitaathiri shughuli zao za kusafisha pamba.

Kwa hiyo, nikapewa hiyo kazi. Nikasafiri kwenda Geita, asubuhi yake (baada ya safari) wenyeji wangu wakanipeleka wanakojenga mgodi. Nikakuta vijiji vinabomolewa kwa magreda na mbele yake wametangulia askari wenye bunduki. Kijiji kile kilipitiwa na barabara, sasa upande wa pili wa barabara yuko Mkuu wa Wilaya, Halima Mamuya, OCD na maofisa wengi.

Mkuu wa Wilaya ya Geita ameshika kipaza sauti, anawaambia wanakijiji kwamba niliwaambia mlipwe fedha (fidia) mmekataa, sasa mtajua mtakwenda wapi.

Pale kwenye shimo kubwa lenye kina cha Kilomita kama tano wanakochimba dhahabu ndipo kilipokuwapo kijiji cha Mtakuja.

Nilishuhudia mgodi wa kwanza ukianzishwa kwa kuharibu kijiji ambako kulikuwa na makazi pamoja na mazao…mahindi yanayoelekea kukomaa, na wakati huo nchi ilikuwa imekumbwa njaa kwa sababu mwaka uliopita kulikuwa na mvua za el-nino.

Hali ile ilinikumbusha wakati wa operesheni vijiji ambako nyumba yetu na za wanavijiji pamoja na mashamba viliharibiwa. Nilishangaa serikali kuharibu mashamba ya chakula. Nikaandika ripoti yangu, nikawapelekea wenye kinu cha pamba na kupendekeza kwamba tunahitaji ginnery kukaa na wananchi kijiji ili kupambana na uhalifu huo.

Nikawaambia nyie mna hela, wanakijiji watawapa ile human element, idadi ya watu ambao wanaathiriwa. Ukizungumza athari, ukaonyesha watu wanabomolewa ina value kubwa sana katika mapambano. Kwa hiyo, wanakijiji mkiwaacha wakasambaratishwa, hata nyinyi hamtabaki.

Wakaniambia sisi ni wawekezaji, nikawaambia wenzangu katika LEAT kwamba ugomvi mkubwa katika miaka inayokuja ni ugomvi wa madini.

Kwa hiyo, kutoka Geita kwenda Bulyanhulu ni mwendo wa dakika 45. Katika kuchunguza makampuni ya madini yanafanya nini kwa wananchi, kitu cha kwanza utakachokutana nacho ni Bulyanhulu. Ndio eneo ambalo kulitokea maafa makubwa zaidi.

Mwaka 1999 nikapata nafasi kwenda Marekani kuwa mtafiti katika taasisi ya World Resource Institute kwa miaka mitatu. Nikawaambia World Resorce Institute nitafanya kwa sharti moja; kwamba kazi niliyoanza kuifanya katika LEAT ya madini niendelee nayo.

Nikaondoka kwenda Marekani Septemba 1999 na kwa miaka mitatu yote mnayojajua juu ya Bulyanhulu yalipatikana katika kipindi hicho. Karibu kila mwezi nilirudi Tanzania kuendelea kutafiti suala hilo la Bulyanhulu.

Tulipata ushahidi wa picha za video na nyingine unaothibitisha kwamba watu wengi waliuawa. Hizo picha ni za jeshi la polisi na kampuni yenyewe.

Tulikuwa kila tunapopata video hizo tunazitangaza hadharani. Mwaka 2001 tulifanya press conference kubwa Maelezo kuthibitisha kwamba tunao ushahidi wa picha za video zinazothibitisha mauaji hayo kutokea.

Nilikuwa mimi na Rugemeleza Nshala. Baada ya mkutano huo, mimi nikaondoka kurudi Marekani. Lakini huko nyuma, baada ya tarehe 23, Polisi wakavamia ofisi zetu za LEAT na nyumbani kwangu wakitafuta huo ushahidi. Na wakati huo Jeshi la Polisi likasema huyu mtu ametoroka, anatafutwa na Interpol, kwa hiyo akamatwe. Wenzangu baadaye walikamatwa.

Niliporudi Marekani walinikamata na kuniweka kituo kikuu cha polisi Dar es Salaam. Nilipokuwa kituoni humo nilifanya ujanja nikaingia na simu na nikafanya mahojiano na magazeti ya Canada na Marekani usiku kucha. Kesho yake ilikuwa sikukuu ya Krismasi. Nikafuatwa na polisi, nikaambiwa napelekwa mahakamani.

Raia Mwema: Tueleze kujiunga kwako na CHADEMA, kulikuwaje?

Lissu: Kujiunga na CHADEMA mwaka 2004 sababu ilikuwa Tarime na suala la kampuni za madini. Harakati za madini Tarime nilizianza mwaka 2003.

Wakati ule mtu aliyenipokea Tarime ni marehemu Chacha Wangwe. Nilimkuta ana kesi 10 za jinai wakati huo akiwa diwani wa CHADEMA. Akaniambia; wanataka kunifunga hawa…nikamwambia hawawezi, wanakutisha tu.

Alisumbuliwa sana, na Tarime ilikuwa inatisha kama ilivyo leo. Mbowe akanipigia simu akaniomba nisaidie kisheria kumtetea Wangwe, chama kitagharimia usafiri. Kwa hiyo, nikaanza kazi ya kuwapa huduma ya kisheria na katika kipindi cha miezi minne nimetoa gerezani watu 366 waliokuwa wanatumikia vifungo.

Siku moja Mbowe akaniambia nitafute watu wengine wanataaluma ili wajiunge na CHADEMA. Nikamuuliza kwa nini unafikiria mimi ni mwanachama wa CHADEMA? Alikuwa miaka yote anafikiria mimi ni mwenzao, kumbe mimi ni NCCR-Mageuzi.

Akauliza kwa nini si mwanachama wa CHADEMA? Nikamwambia hujawahi kunipa sababu za kwa nini niwe mwanachama wa CHADEMA. Kama unataka niwe, niambie tu.

Kwa hiyo, hivyo ndivyo nilivyoingia CHADEMA. Kwa maisha yangu kwa historia yangu na msimamo wangu, mimi ni mwanahakarati, na pengine Rais Kikwete hakosei sana anaposema vyama vingine ni vya wanaharakati.

Raia Mwema: Unazungumziaje nafasi yenu Bungeni, hasa ikizingatiwa suala la idadi na ubora wenu?

Lissu: Bunge kama unaelewa sawawa linakupa nafasi ya kuibua mijadala. Siku zote sasa nimeelewa kwamba Bunge si mahali pazuri pa kutatulia migogoro, lakini ni mahali pazuri pa kuzungumzia na ku-mobilise nguvu ya umma. Hayo matatizo ya kisiasa au kikatiba, hayatatuliwi bungeni isipokuwa yanazungumzwa.

Suala la wingi, kwa maana ya idadi au ubora wa wabunge, bila kujali idadi lina umuhimu wake.

Kwa mfano; inapofika wakati wa kupitisha sheria au bajeti, hatuwezi ingawa tunao wabunge bora zaidi na wajenga hoja wazuri. Kwa hiyo, hapo ‘ujinga wa wengi’ ndipo unaposhinda. Kama unaitumia nafasi hiyo bungeni vizuri, kama ambavyo tumekuwa tunafanya, hiyo itakuwa inatusaidia kujenga nguvu kubwa nje ya bunge. Inategemea unatumiaje hiyo fursa ya Bunge.

Raia Mwema: Ulikuwa Tarime hivi karibuni. Wako wanaohoji ulikwenda kutafuta nini wakati ni eneo lenye mbunge wake.

Lissu: Labda niwajibu hao wajinga wasiojua nilikuwa nafanya nini Tarime. Kwa historia yangu na Tarime, ilikuwa ni wazi ningeenda Tarime baada ya kutokea masuala haya (mauaji) na ndugu zao kukataa kuwazika hadi uchunguzi. Ningekuwa sio mbunge pia ningekwenda Tarime. Nina historia ndefu ya mapambano ya kudai haki Tarime.

Yaliyotokea yanafamika – tulikamatwa na kuwekwa kwenye selo Tarime, tumeshtakiwa. Ni hali halisi ya Tarime. Ni eneo la vita, ni janga la kitaifa kama nilivyoeleza baada ya kuachiwa kutoka gerezani.

Tarime ya leo ni mbaya kuliko Tarime ya 2003 nilipokwenda kwa mara ya kwanza ambapo mamia ya watu wa Nyamongo walikuwa gerezani. Tarime ya leo ni ya mauaji yanayofanywa na jeshi la polisi. tangu tuwashinde (CCM) uchaguzi. Mauaji ya kwanza Tarime yalifanyika Julai 20, 2005. Hadi kuua hawa wa juzi watano, sasa wamefikia watu 28 waliouawa kwa kupigwa risasi mchana kweupe.

Raia Mwema: Lakini kiini cha tatizo nini? Je, ni mwekezaji au jeshi la polisi?

Lissu: Tatizo ni mwekezaji, polisi na Serikali ya Tanzania. Kusingekuwapo mwekezaji, watu wasingeuawa.

Raia Mwema: Lakini kama tatizo ni pamoja na polisi au serikali kuna migodi mingine mauaji hayaendelei kama Tarime?

Lissu: Katika sekta ya madini unakuja na umwagaji damu. Bulyanhulu, Tarime, Geita, Nzega hakuna mahali ambapo wawekezaji wameweka mgodi wa dhahabu wa kisasa bila kuangamiza uchumi wa wenyeji, bila kuwaondoa kwa mabavu ya kijeshi.

Raia Mwema: Kifanyike nini?

Lissu: Ni mambo mawili ya kuchagua. Kwanza, je, tunataka huyo anayeitwa mwekezaji achume mali na inunuliwe kwa damu za Watanzania? Inunuliwe kwa Watanzania kukosa haki na kwa uchumi wa Watanzania kusambaratishwa? Au tuamue kwamba maisha ya Watanzania ni bora zaidi kuliko dhahabu.

Kwa maoni yangu, haiwezi bei ya dhahabu ikawa sawa na maisha ya mtu mmoja. Watanzania wameshauwa kwa risasi na kwa kunywa maji ya sumu yanayotokana na mwekezaji. Tarime imejaa vijana wanaoshitakiwa kwa kesi za ugomvi na mgodi, lakini sasa hivi wanashtakiwa kwa kesi za mauaji au uhalifu wa kutumia silaha!

Wakati nakwenda Tarime kwa mara ya kwanza, kesi zilizokuwa zikifunga watu zilikuwa uchochezi na kuvamia eneo la mgodi, lakini leo kesi za Tarime ni mauaji. Hata ukikamatwa kwa kurushwa jiwe ambalo halijampiga mtu yeyote, utashtakiwa kwa mauaji au uhalifu wa kutumia silaha!

Na unashtakiwa kwa hayo makosa mawili kwa sababu huwezi kupewa dhamana. Kwa hiyo, polisi wasipofanya upelelezi utafia gerezani.

Nilikamatwa Tarime nikakaa gerezani. Naweza kuthibitisha kuwa Tarime kuna watu zaidi ya 400 wanaokabiliwa na kesi za mauaji.

Sasa njoo huku ambako hakuna mgodi, leo biashara ya teksi Tarime mjini ni biashara ya mapolisi kwa sababu wafanyabiashara wa kawaida pale mjiini aidha wako gerezani wakikabiliwa kwa mauji au wengine wameuawa.

Selo niliyofungwa mimi Tarime inatumika kwa kitu kimoja tu, nimeambiwa kuna watu wengi sana wameuawa, wameumizwa sana. Kuna mtu mmoja amepigwa risasi tano miguuni kwenye kituo cha polisi na mkononi amepigwa risasi mbili, na mkono umekatwa.

Kuna watoto. Kuna mtoto wa miaka 12 selo niliyolala mimi. Bunge hili limepitisha sheria mwaka juzi, sheria ya mtoto inayosema mtoto wa miaka 18 hawezi kupata adhabu ya kifungo.

Huyu mtoto ana miaka 12 anakaa kwenye gereza na wafungwa watu wazima waliopatikana na hatia. Napeleka hoja binafsi bungeni kuomba iundwe kamati teule ya Bunge kuchunguza suala hili.
Credit:Raia mwema
 Audio:Mahojiano ya Tundu Lisu baada ya kutoka Mahakamani bofya hapa

Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top