Taarifa: Makamu wa Rais, atoa onyo kwa watendaji waochochea uharibifu wa mazingira


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amekutana na kufanya mkutano wa kazi na watendaji wa ofisi yake ya Idara ya Mazingira kujadili kwa kina namna ya kukabiliana na hali tete ya uharibifu wa mazingira unaoendelea nchini.


Katika mkutano huo uliofanyika leo, Ikulu, Dar es salaam ambao ulihudhuriwa pia na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira January Makamba, Makamu wa Rais ameawaagiza watendaji wa idara hiyo waache kukaa ofisini na badala yake waende kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kukabiliana na uharibifu wa mazingira katika maeneo mbalimbali nchini.


Alisema hali ya uharibifu wa mazingira ikiachwa iendelee kama ilivyo inaweza ikasababisha madhara makubwa kwa jamii na Taifa kwa ujumla, hivyo ni muhimu kwa makundi yote wakiwamo wataalam wa mazingira na wadau wa maendeleo kuelekeza nguvu zao katika kukabiliana na tatizo hilo.


Alisema baadhi ya watendaji wamekuwa ni sehemu ya uharibifu wa mazingira na kuonya wataobainika kufanya vitendo hivyo watachukuliwa hatua kali ili kukomesha tabia hiyo.


Baadhi ya watendaji waliotoa taarifa kuhusu hali ya mazingira nchini wamekiri kuwa hali ya uharibifu wa mazingira siyo nzuri hasa kwenye mikoa ya Dodoma, Shinyanga, Manyara, Geita, Singida na Kilimanjaro.
Inakadiriwa kuwa takribani hekta 400,000 za misitu zinaharibiwa kila mwaka hali ambayo inapelekea baadhi ya wanyama kutoweka.


Watendaji hao wameiomba serikali iongeze bajeti ya kutosha ili waweze kukabiliana na tatizo la uharibifu wa mazingira ikiwemo utoaji wa elimu kwa wananchi.


Makamu wa Rais ametumia siku ya mapumziko ili kujadiliana na kuweka mipango na mikakati ya kukabiliana na uharibifu wa mazingira nchini. Mkutano huo wa kazi unaendelea tena hapo kesho.


Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
Dar es salaam
20/8/2016
 

Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top