SAIKOLOJIA : Fahamu mambo yanaweza kukufanya uzungumziwe vizuri



Moja ya kipimo cha mafanikio ya mtu katika maisha yake ni kusemwa vizuri na watu kwa kuwa hiyo ndiyo ishara ya upendo walionao kwake. Je, kama ungeombwa kuorodhesha tabia zako ambazo unafikiri zinaweza kuwafanya watu wakuseme vizuri ungeweza
kuandika ngapi? Je, unaweza vile vile kuandika zile ambazo zinaweza kukufanya usemwe vibaya? Kama hujawahi kufanya hivyo hebu jaribu siku 

Je, unajua jinsi unavyosemwa na watu katika jamii? Wanakusema vizuri au vibaya? Hili ni moja kati ya changamoto zinazotukabili katika maisha kwa kuwa watu huwa hawapendi kuwambia wenzao uso kwa uso tabia zao nzuri au mbaya. Hupenda kusema mahali ambapo mhusika hayupo. Mara nyingi maelezo ya jinsi jamii inavyowaona watu hutolewa siku ya mazishi yao.


Moja ya kipimo cha mafanikio ya mtu katika maisha yake ni kusemwa vizuri na watu kwa kuwa hiyo ndiyo ishara ya upendo walionao kwake. Je, kama ungeombwa kuorodhesha tabia zako ambazo unafikiri zinaweza kuwafanya watu wakuseme vizuri ungeweza kuandika ngapi? Je, unaweza vile vile kuandika zile ambazo zinaweza kukufanya usemwe vibaya? Kama hujawahi kufanya hivyo hebu jaribu siku moja.


Kwa kuwa kila mmoja wetu anapenda kupendwa, kuthaminiwa na kusemwa vizuri tunakabiliwa na swali moja kubwa. Tufanye nini katika maisha ili tuwe na mvuto na upendo kwa watu na tusemwe vizuri jamii?


Kuna mambo mengi mema tunayoweza kufanya ili tuwe na mvuto na sifa nzuri kwa watu na kuwafanya watuseme vizuri. Jambo la kwanza ambalo ni muhimu kuliko yote ni kujenga ujamaa na udugu au urafiki ambao huleta maelewano na ushirikiano. Mara nyingi nimewahi kusikia mtu akisema, “Amenipita bila kunisalimu!” Anayesema hivyo huwa hafikirii kuwa na yeye pia ana makosa kwa sababu amemtazama mtu huyo akipita hadi akatoweka bila kumsalimu. Wote wana makosa.


Huenda yule aliyesemwa na mwenzake naye amesemwa hivi, “Nimepita ananitazama tu bila kunisalimu! “Fanya juhudi kila mara uwe wa kwanza kujenga mazingira ya maelewano.


Katika makala hii tutataja mambo saba miongoni mwa mengi ambayo wanafalsafa husema yanasaidia kumfanya mtu aelewane na watu. Haya yalibuniwa na mjasiriamali maarufu huko Marekani Benjamin Fairless.


Jizoeze kuwa na tabia na mwenendo unaopendwa na watu


Hayati Shaaban Robert aliwahi kusema, “Tabia nzuri ni vazi analotakiwa mtu kulivaa kila anapotoka hadharani “Binadamu anapaswa kuwa na tabia nzuri katika jamii ili akubalike na kupendwa. Tabia nzuri hujumuisha mambo mbalimbali kama vile ucheshi, wema, huruma, heshima, uadilifu, ukarimu au upole.


Kuwa wa kwanza kuweka mazingira yanayojenga ujamaa na udugu


Watu husema, “Hali gani ndiyo mwanzo wa kujuana.” Kuwa na tabia ya kujitambulisha na kuwatambua watu wengine na kuwasalimu kwa majina yao kila mnapokutana. Salamu ya ucheshi na tabasamu huwa njia ya haraka ya kujenga uelewano na ushirikiano. Hali hii hujenga msingi wa mazungumzo na kutendeana wema.


Kubali kuwa kuna tofauti na upungufu baina ya binadamu


Katika kuishi na kujenga uhusiano na watu hatuna budi kutambua kuwa binadamu hutofautiana katika utimilifu wa tabia, huwa ana haki ya kukosea na kila mmoja huwa ana haki ya kutofautiana na wengine. Kwa kanuni hizi za kibinadamu, kila tunapojaribu kujenga urafiki na maelewano tusiwachukie au kuwanyanyapaa watu kwa kuwa wanapendelea mambo yanayotofautia na yale tunayoyapenda sisi, mradi hayahusiani na uhalifu.


Hata hivyo, siyo lazima sisi tupende yale wanayoyapenda wengine bali tusiwachukie kutokana na yale wanayoyapenda. Tena vyema tukumbuke kuwa watu huwa hawapendi kuambiwa wamekosa. Wala tusihangaike kuwafanya watu wabadili tabia zao ziwe kama zetu ili kuwafanya marafiki zetu. Tukumbuke kuwa watu wote tukiwa na tabia zinazofanana dunia itapooza.


Tusiwapime watu ubora wao kwa mtazamo hasi


Tunapochunguza ubora wa watu katika kujenga urafiki tusiwachunguze sifa zao kwa mtazamo hasi bali tutumie mtazamo chanya. Kwa mfano watu wawili wanaweza kutaja sifa za mtu mmoja wakatofautia tu kwa sababu mmoja amezitazama kwa mtazamo chanya na hasi. Kwa mfano, mtu mwenye mtazamo chanya atasema, “Fulani ni mpole sana. Anapoongea na wageni huwasikiliza kwa makini bila kuwakatiza mpaka wanapofika mwisho. Kisha ndipo yeye hutoa maoni yake.” Mwenye mtazamo hasi husema hivi,” Fulani ni mtu asiye mcheshi. Hapendi wageni na wanapokuwa wakiongea yeye hukereka akanyamaza kimya na kuwaacha waongee pekee yao.


Tujifunze kutoa takrima ya mazungumzo


Hakuna kitu ambacho humfanya mtu ajihisi ameheshimiwa kama anapopewa nafasi ya kusema na akasikilizwa. Kama utataka kuwa na marafiki wengi hasa miongoni mwa watu wa hali ya kawaida, hautawafurahisha zaidi kuliko kuwapa nafasi ya kuongea na wewe ukawasikiliza huku akiwafurahia na kuwawekea mazingira yatakayo wafanya awe huru kuongea.


Kila wakati wafanye watu wajihisi wako katika hadhi ya juu


Moja katika tabia mbaya tunapofanya jitihada ya kujenga urafiki na ushirikiano ni kujifanya watu wakuone uko juu kuliko wao. Jenga tabia ya kuzungumza na watu huku ukiwafanya wajione mko sawa na unawaheshimu na kuwathamini. Tabia hii huwafanya wakuone unawajali na kufanya upendo wao kwako uchanue.


Wakati mambo yanapoharibika usiwalaumu wengine


Katika maisha kila siku kila tatizo linapotokea tumezoea kumtafuta wa kumlaumu. Mara nyingi tunawasikia watu wakisema, “Isingekuwa fulani nisingekuwa hivi! “Hakuna jambo linaloharibu upendo kama kulaumiana. Ili uwe na maelewano mazuri na watu epuka kabisa kutupia lawama mtu au watu. Tunapokuwa na tabia nzuri na upendo kwa watu tunakuwa wepesi kubebeka. Lakini tunapokuwa na tabia mbaya na mwenendo usiopendeza katika jamii watu wanasita kutupatia vyeo au wadhifa katika maisha. Kwa hakika tunakuwa wazito wala hatubebeki kwa urahisi.



Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top