Ndugai kukabili hoja sita za Ukawa


Wakati Spika Job Ndugai akionyesha nia ya kumaliza msimamo wa wabunge wa upinzani kususia vikao vinavyoendeshwa na naibu wake, kiongozi wa upinzani bungeni, atalazimika kujiandaa kukabiliana na hoja sita.


Wabunge wa upinzani walisusia takribani vikao vyote vya Bunge la Bajeti, wakidai Naibu Spika, Dk Tulia Ackson ametumwa na Serikali kukandamiza demokrasia, ana ubaguzi wa vyama na anakiuka kanuni za uendeshaji Bunge.


Waliamua kuanza kususia vikao hivyo siku ambayo Dk Tulia alikataa hoja ya mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nasari kutaka Bunge lisitishe kujadili bajeti na kuzungumzia sakata ka wanafunzi 7,802 wa Chuo Kikuucha Dodoma kutimuliwa bila ya kuwapa muda wa kujiandaa, hoja ambayo awali iliibuliwa kimakosa na mbunge wa Chemba (CCM), Juma Nkamia.


Kadri siku zilivyokwenda ndivyo hali ilivyozidi kuwa mbaya, huku Dk Tulia akiongoza vikao vyote vya asubuhi na jioni na ilifikia wakati wabunge wa upinzani, ambao walikuwa wakishinda kantini, walisusa hata kusalimiana na wabunge wa CCM.


Juzi Spika Ndugai alisema katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Azam TV kuwa ana nia ya kumaliza mgogoro huo na gazeti hili lilipomtafuta kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni, Freeman Mbowe kujua hoja ambazo wangependa zitatuliwe, alisema suala lao liko wazi.


“Kwa sasa nipo katika kikao ila hoja zetu kuhusu Naibu Spika zipo wazi kabisa na tuliziwasilisha Ofisi ya Spika na (mbunge wa Simanjiro, James) Ole Millya alieleza kila kitu kuhusu msimamo wetu,” alisema Mbowe jana.


Mbowe ambaye juzi alilieleza gazeti hili kuwa yuko tayari kwa mazungumzo, jana alisema msimamo wa wapinzani umebeba mambo hayo yaliyomo katika hoja waliyoiwasilisha kwa katibu wa Bunge kwa ajili ya kumwondoa madarakani Dk Tulia.


Msingi wa Hoja


Hoja hizo waliziwasilisha wakati Bunge la Bajeti likiendelea na kama alivyoeleza Ndugai juzi, hoja ya kwanza ni madai kuwa Naibu Spika ameweka maslahi ya CCM mbele kuliko Bunge, kinyume na Kanuni ya 8(b) ya Kanuni za Kudumu za Bunge.


Madai ya pili ni kutumia vibaya madaraka ya kiti cha Spika, kutokana na tukio la Mei 6 la kutoa uamuzi wa mwongozo ambao wanadai ulikiuka Ibara ya 12(2) ya Katiba ya Tanzania inayosema “kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake”.


Mwongozo huo ulitokana na madai kuwa mbunge wa Ulanga (CCM), Goodluck Mlinga alidhalilisha wabunge wanawake na upinzani aliposema kuwa ubunge wa viti maalumu unatokana na michepuko.


Wapinzani pia walidai katika hoja yao ya tatu kuwa Dk Tulia alivunja Kanuni ya 64 (1)(f) na (g) inayokataza mbunge kutumia lugha ya matusi kwa mbunge au mtu mwingine yeyote na kukataza matumizi ya lugha ya kuudhi au kudhalilisha watu wengine.


Wanaelekeza hoja hiyo kwenye kauli ya Dk Tulia aliyesema “Mheshimiwa Bwege, usionyeshe ubwege wako humu ndani” alipokuwa akiongea na mbunge wa Kilwa Kusini (CUF), Suleiman Said Ally Bungara ambaye ni maarufu kwa jina la Bwege.


Katika sababu ya nne, wapinzani wanasema Dk Tulia aliamua kwa makusudi kuvunja Ibara ya 63(2) ya Katiba kwa kutumia vibaya Kanuni ya 69(2) na 47(4) ya Kanuni za Bunge kumzuia Nassari na Bunge zima kutimiza majukumu yake ya kikatiba ya kuisimamia na kuishauri Serikali katika suala la kufukuzwa kwa wanafunzi wa kozi maalumu ya ualimu wa sayansi Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).


Hoja ya tano ya upinzani ni madai kuwa Naibu Spika aliongoza kikao cha Bunge Mei 26, mwaka huu, na bila ridhaa ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, akashiriki kufuta sehemu ya hotuba ya msemaji mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kinyume na kanuni ya 99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge.


Kwa mujibu wa mashtaka hayo, hoja ya sita ni kitendo cha Dk Tulia kukataa taarifa tofauti zilizowasilishwa na wabunge wanne wa upinzani, wakisema kuwa alikiuka kanuni ya 5(1) ambayo inataka kuzingatia mila na desturi na uamuzi wa maspika wa mabunge mengine yenye utaratibu wa kibunge unaofanana na utaratibu wa Bunge la Tanzania.


Hata hivyo, Ndugai alisema kwa uzoefu wake anaona matatizo mengi yaliyosababisha mgogoro huo ni mtazamo wa wapinzani kutokana na Dk Tulia kushika moja kwa moja nafasi ya Naibu Spika bila ya kuwahi kuwa mbunge, na hasa kutokana na kuteuliwa na Rais kuwa mbunge wakati wa mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa Bunge.

 Habari za Magazetiya Leo Jumanne August 16, 2016 bofya hapa

MANJI AJIUZULU YANGA bofya hapa





Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top